KANISA NA SIKU ZA HATARI
Shalom: Jina kuu la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).
Kabla hatujaendelea mbele kujifunza ujumbe wa Roho Mtakatifu, hebu kwanza turudi shule, bila shaka umewahi kusoma soma la biolojia(sayansi), sasa kuna jambo nataka tujikumbushe linalohusiana na ule mzunguko wa mwanamke (hedhi), hatutaingia sana ndani ila kuna jambo moja nataka tuone, kwa kawaida mzunguko ule unakuwa na siku 28 mpaka 32 kutegemeana na mwanamke kwa mwanamke, na ndani ya hizo siku..kuna siku ambazo ni salama, siku za hedhi na siku za hatari, kama tunavyoona hapo juu kwenye huo mduara. zile siku za hatari ndio siku ambazo mwanamke anaweza akabeba mimba ikiwa atakutana na mwanamume katika hizo siku, hivyo mwanamke ambaye bado hajawa tayari kuwa na mtoto au hajafikia muda sahihi wa kuwa na watoto anatakiwa kuwa makini na hizo siku..huo ni kulingana na ushauri wa wataalamu, hapaswi kabisa kufanya kosa katika hicho kipindi.
Sasa, turudi katika mambo ya rohoni, tunajua kuwa mwanamke kibiblia anawakilisha kanisa, ndio maana kwenye kitabu cha ufunuo kuna wanawake watatu wametajwa ambao wanafunua makanisa matatu. Hebu tusome..
Ufunuo12:1 Na ishara kuu ilionekana mbinguni; MWANAMKE aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili
Kulingana na biblia huyo mwanamke ni taifa la Israeli ambalo ni kanisa la jangwani, lakini hebu tuangalie mwanamke mwingine..
Ufunuo wa Yohana 17:1,3 Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;
[3]Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona MWANAMKE, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
Bila shaka huyo mwanamke ni kanisa la shetani ambalo linafanya kazi ya kuwaua watu wa Mungu kimwili na kiroho akishirikiana na huyo mnyama..ndio maana ni kahaba analizinisha kanisa la Kristo uzinzi wa rohoni.
Na mwanamke wa mwisho ambaye anatajwa kama bibi arusi tunamsoma katika sura ya 19.
Ufunuo 19:7-8 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na MKEWE amejiweka tayari.
[8]Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.
Hilo ni kanisa safi la Kristo, mimi na wewe, ikiwa umeokoka we ni mke wa Yesu Kristo Bwana wetu.
Hivyo.. mwanamke katika biblia anawakilisha kanisa, ndio maana Mtume Paulo alisema kwa Ufunuo wa Roho maneno haya katika…
Waefeso 5:24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.
Na tena.. sehemu nyingine anasema..
2 Wakorintho 11:1-2 Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami.
[2]Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ILI NIMLETEE KRISTO BIKIRA SAFI.
Sasa, baada ya kujua hayo..turudi kwenye kiini cha somo letu, kama vile tulivyojifunza kuwa mwanamke anapaswa kuwa makini sana katika zile siku zake za hatari ikiwa hana haja na mtoto kwa wakati huo, hali kadhalika biblia inasema.. siku za mwisho kutakuwako na nyakati za hatari, hivyo kanisa kama mwanamke aliye katika siku zake..linapaswa kuwa makini sana katika nyakati hizi.. kwasababu ni nyakati za hatari.
2 Timotheo 3:1-4 Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.
[2]Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,
[4]wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
Ni dhahiri kuwa kila mtu anafahamu kuwa hizi ni siku za mwisho, hivyo tunaishi katika nyakati za hatari kama maandiko yalivyotabiri kuwa siku za mwisho kutakuwako na nyakati za hatari.
Na ni kwanini ni nyakati za hatari, ni kwasababu ya hali za watu wa siku za mwisho, kwamba watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
Hivyo kutokana na hali hizo.. hatari nyingi sana zitatokea duniani ikiwemo magonjwa mabaya, mauwaji, njaa, uhalifu, vita, maadili kuporomoka, na mambo mengi mabaya ambayo yatailemea dunia na hatimaye kuifikisha mwisho wake kabisa, kwahiyo hatari hizi ni dalili zinazotuonyesha kuwa ule mwisho umekaribia.
Hivyo ni wakati ambayo Kanisa linapaswa kuwa makini sana kwani ni nyakati za hatari na hatari kubwa zaidi kwa kanisa ni pale itakaposhindwa kujizuia na mambo ya kidunia, ni pale itakapoacha kumtegemea Mungu na kutegemea fedha na kupenda, ni pale ampapo watu waliokoka watakuwa watukanaji, wakali, wasaliti, wasiopenda mema, watukanaji, wasengenyaji,..n.k hiyo ndio hatari kubwa.
Kumbuka watu wanaozungumziwa hapo ni waumini/watakatifu wa siku za mwisho, kwasababu watu wengine wa kidunia hawajawahi kumpenda Mungu, siku zote wanakiburi, siku zote wanapenda anasa, siku zote wanachuki, siku zote ni wasaliti, watukanaji..n.k
Nyakati za hatari kwa kanisa ni matendo ya giza kupata nafasi ndani ya kanisa.. mfano ulevi, uzinzi, uasherati, usengenyaji, upendo wa kumpenda Mungu kupungua au kutokuwepo kabisa, mavazi ya ukahaba kwa wanawake ndani ya kanisa la Mungu mfano vimini, suruali, fashion, mapambo ya kidunia ndani ya kanisa…hiyo ni hatari sana, Na sababu ya hayo yote ni kanisa kushindwa kujizuia..kama vile mwanamke aliye katika siku zake akashindwa kujizuia na kwenda kufanya uasherati, vilevile kanisa kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu.. kumbuka kanisa ni mimi na wewe tuliyookoka kwa kumwamini Bwana Yesu ipasavyo.
Hivyo ikiwa umeokoka kweli kweli, basi fahamu we ni sehemu ya kanisa la Kristo, hivyo unapaswa kuwa makini sana.. ili usije ukaingia kwenye hatari hii ya kuwa mlevi wa vitu vya kidunia mfano ushabiki wa mipira, magemu, movies za ajabu ajabu zisizo na maana, kumbuka hizi ni nyakati za hatari.. Ukifanya tu kosa kidogo kuna uwezekano ukakosa unyakuo…huko ndiko kupata mimba usioitarajia.
Kama binti wa kikirsto..tambua we ni sehemu ya kanisa takatifu la Mungu.. hivyo jitunze na ulimwengu, kaa mbali na fashion ambazo hazina utukufu kwa Mungu, kaa mbali na mapambo hayo ya kidunia kama hizo hereni, bangili, kucha bandia, lipustick, mekaups, nywele bandia, na mapambo yote ya nje, mapambo yako ni upole, utu wema, kiasi, upendo, uvumilivu na saburi.
Kijana uliyeokoka we ni sawa na mwanamke aliye katika siku zake, kuwa makini sana na hayo makundi, kuwa makini sana na huo mwenendo wako usije ukaingia katika hatari.. maana hizi ni siku za hatari, jizuie na vitu vya kidunia usije ukaharibu ukristo wako.
Lakini ikiwa bado hujaokoka, basi fahamu kuwa neema hii unayopata leo hii, ambayo inakuhubiria kila siku, fahamu kuwa haitakuwepo daima..ni heri ukaipokea hii neema ili usije ukajuta milele.
Kuna hatari kubwa iko mbele yako, usidhani dunia ina usalama kama uonavyo..mambo mabaya na ya kustaajabisha yanakuja mbeleni.. vilevile we mwenyewe hujui siku ambayo utaiaga hii dunia kwa mara ya mwisho, je siku ukiondoka katika hiyo hali yako ya kuvuta sigara, siku ukianguka na huo uzinzi unaoufanya kila week, hiyo pombe na madawa ya kulevya unayoitumia.. siku ukifa utaenda kuwa mgeni wa nani? Biblia inasema..
“.. mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.” (Mhubiri 11:3)
Ikiwa na maana, ukifa leo, hali yako ya mwisho ambayo umeondoka nayo ndiyo itakupa picha kuwa utaenda kulalia upande gani? Ni uzimani au mautini, na mtu ameandikiwa kufa mara moja.. baada ya kufa ni hukumu.. soma Waebrania 9:27, hakuna nafasi ya pili baada ya kufa au baada ya unyakuo.
Hivyo saa ya wokovu ni sasa, tunaishi ukingoni mwa nyakati za hatari na hatari kubwa zaidi inaijia dunia.
Mwamnini Bwana Yesu na utubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kabisa kuziacha na kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu sawa sawa na Matendo 2:38.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.