USIWE NA SHINGO NGUMU

Uncategorized No Comments

USIWE NA SHINGO NGUMU

Watu wenyewe shingo ngumu ni watu wa namna gani?

Hii ni sifa mojawapo ya watu wenye shingo ngumu.

1.Siku zote wanampinga Roho Mtakatifu

Matendo ya Mitume 7:51 “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.”

Katika siku hizi za mwisho..kumekuwa na watu wengi wa namna hii, ambao wanampinga Roho Mtakatifu. Na watu hawa sio watu wasiomjua Mungu kabisa..hapana ni watu wa kidini, watu ambao wana majina ya kuwa wakristo lakini ni wakristo jina, watu ambao wamezoelea kusikia injili kila siku (wana wa ufalme), wanasikia kabisa sauti ya Roho Mtakatifu akiwashuhudia waache njia zao za uovu na uvuguvugu, lakini kama baba zao walivyofanya, na wao ni vivyo hivyo wanafanya.

Bwana Yesu alitoa mfano huu kwa watu wa namna hii wanaompinga Roho Mtakatifu.

Mathayo 22:1-9 Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,

[2]Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.

[3]Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja.

[4]Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.

[5] LAKINI HAWAKUJALI, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;

[6]nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.

[7]Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.

[8]Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.

[9]Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.

Hebu tafakari hilo neno ”HAWAKUJALI” kwa maana nyingine walifanya shingo zao kuwa ngumu, kwanini?

Ni kwasababu walialikwa waende kwenye karamu, wakapokea mwaliko.. lakini baadaye wakakusudia kutoshiriki kwasababu zao wenyewe, hawakujali huo mwaliko.. mfano dhahiri wa watu wa kizazi hiki ambao kila siku wanasikia sauti ya Roho Mtakatifu akiwaalika wapokee wokovu wa kweli.. lakini hawajali, wanafanya shingo zao kuwa ngumu.

Ndugu unapoisikia Injili wakati huu ya kukualika kwenye ufalme wa mbinguni, inayokuambia utubu na uache dhambi na rushwa, na utapeli, na wizi, na ukahaba na wewe unaanza kusema siwezi kuacha kufanya hivyo vitu kwa wakati huu au kubadilika sasa..na umesikia kabisa sauti ya Roho Mtakatifu akikushudia kuwa watu wa jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu, lakini hutaki kuelewa..basi fahamu kuwa unashingo ngumu na Bwana anasema..

Isaya 3:16-24 BWANA akasema tena, Kwa sababu binti za Sayuni wana kiburi, na kuenenda na shingo zilizonyoshwa, na macho ya kutamani, wakienenda kwa hatua za madaha, na kuliza njuga kwa miguu yao;

[17]Basi, kwa hiyo, Bwana atawapiga binti za Sayuni kwa pele za utosini, na BWANA ataifunua aibu yao.

[18]Siku hiyo BWANA atawaondolea uzuri wa njuga zao, na kaya zao;

[19]na pete za masikio, na vikuku, na taji zao;

[20]na dusumali, na mafurungu, na vitambi, na vibweta vya marashi, na matalasimu;

[21]na pete, na azama,

[22]na mavazi ya sikukuu, na debwani; na shali, na vifuko;

[23]na vioo vidogo, na kitani nzuri, na vilemba, na utaji.

[24]Hata itakuwa ya kuwa badala ya manukato mazuri kutakuwa uvundo, na badala ya mishipi, kamba; na badala ya nywele zilizosukwa vizuri, upaa; na badala ya kisibau, mavazi ya kigunia; na kutiwa alama mwilini kwa moto badala ya uzuri.

Unaposikia sauti ya Roho Mtakatifu inakushudia kuwa mwanamke hapaswi kuvaa mavazi yawapasayo mwanamume (suruali) kwa maana ni machukizo kwa Mungu (kumb.22:5), na wachukizao sehemu yao ni ziwa la moto kulingana na biblia (ufunuo 21:8), na wewe bado unaendelea kufanya hayo machukizo.. hujali, unasema Mungu haangalii mavazi.. tambua kuwa unashingo ngumu na kama ukiendelea kushupaza hiyo shingo mwisho wake itavunjika na hautapata dawa..utakuwa tu unasubiria jehanum ya moto.

Mithali 29:1 Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.

Tubu dhambi zote unazozifanya kwa siri na kwa wazi acha kushupaza shingo usije ukavunjika ghafula, kumbuka hakuna dawa…biblia inasema mtu ameandikiwa kufa mara moja tu na baada ya hapo ni mauti soma Waebrania 9:27, kumbuka sio toba, au maombi ni hukumu.

Saa ya wokovu ni sasa na wala sio kesho au baadaye!!

Acha kuuchezee huu muda, ambao wenzako waliokuzimu wanatamani hata dakika moja tu watengeneze mambo yao na Mungu wanakosa.. unayo nafasi sasa ya kufanya hivyo, pale ulipo tubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi ulizokuwa unafanya kisha tafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa mwili wote na kwa jina la Bwana Yesu kwa ajili ya ondoleo la dhambi na Bwana mwenyewe atafanya yaliyosalia kwa kupitia Roho wake Mtakatifu. Nawe utakuwa umeanza mwendo mpya na Bwana, hata kufikia karamu yake kuu aliyowaandalia watu wake tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.

Tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho acha kufanya shingo ngumu, Yesu Kristo yupo mlangoni!! Kuna hatari kubwa iko mbele yako usipokubali leo kutii hii injili na kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi kabisa.

Basi ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Kumbuka..

>Kwa Yesu lipo tumaini la uzima wa milele.

>Kwa Yesu Unapata utulivu wa nafasi na faraja. Alisema.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

✓Kwa Yesu zipo Baraka.

✓Na kwa Yesu upo msahama wa kweli:

Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.

Kwa hiyo unapokuja kwake leo hii kwa kumaanisha, ujue kuwa hiyo mizigo ya dhambi uliyonayo haijalishi ni mingi kiasi gani ataitua mara moja, haijalishi uliuwa watu wengi namna gani, haijalishi ulizini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, haijalishi ulikwenda kwa waganga mara nyingi namna gani..Ikiwa tu upo tayari leo kumkaribisha Yesu moyoni mwako basi ataitua, na kukusamehe kabisa kana kwamba hakuna chochote ulichowahi kumkosea..Na atakupa amani.

Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..

Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..

Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Hongera kwa kuokoka.

Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namna uzionazo chini ya makala hii.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *