Naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake.

Siku za Mwisho No Comments

Naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake.

Mathayo 24:17-18 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;

[18]wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.

Katika nyakati tunazoishi kila mtu anafahamu kuwa tunaishi ukingoni kabisa mwa siku za mwisho, lakini cha kusikitisha ni kwamba pamoja na kuwa watu wengi wanafahamu na wanashudia kuwa hizi ni siku za mwisho kweli kweli, ni wachache tu ndio wapo tayari kwenda kumlaki Bwana mawinguni, wengi bado wameshikilia kuupenda ulimwengu.

Lakini Bwana alisema katika injili ya Luka 12:32 “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.”

Ni wazi kuwa ni watu wachache sana watakaonyakuliwa siku ile parapanda ya mwisho itakapolia, mtu mmoja alimuuliza Bwana akamwambia..

Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,

[24]Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba WENGI watataka kuingia, wasiweze.

Zingatia hilo neno “wengi”, Bwana Yesu alifananisha tena siku ya kuja kwake mara pili kuwanyakua watu wake na siku za Nuhu na Lutu, tunafahamu kuwa kipindi cha Nuhu ni watu 8 tu ndio waliokolewa, na kipindi cha Lutu ni watu 3 tu ndio walifanikiwa kuokoka…na ndivyo itakavyokuwa katika siku ya unyakuo, ni watu wachache sana ndio watanyakuliwa..biblia ipo wazi katika hilo.

Hivyo ikiwa umeokoka kweli kweli yaani umeacha ulimwengu na matendo yote ya giza na umebatizwa ubatizo sahihi na ukajazwa Roho Mtakatifu..basi fahamu wewe ni bibi arusi wa Kristo, na moja ya hizi siku tutamwona Bwana mawinguni. Hivyo tunapaswa kumngoja Bwana na kumtazamia wakati wowote pasipo kugeuka geuka nyuma kabisa.

Ni heri ubaki kushikilia imani mpaka mwisho hata kama unapitia dhiki na majaribu mbali mbali, huu si wakati wa kuangalia nyuma..Bwana amekaribia kurudi kweli kweli na anataka aje akute imani ile tuliyokuwa nayo mwanzoni, ikiwa na maana mwanzoni ulikuwa unahudhuria mikesha ya maombi kila mara, ulikuwa haupitishi week bila kufunga na kuomba, siku haipiti bila kufungua biblia, siku haipiti bila kuzungumza na Mungu, ulikuwa unapenda kufanya kazi ya Mungu, ulikuwa unajuhudi katika kushuhudia habari njema, ulikuwa unauchukia ulimwengu, huo mwendo uliyoanzanayo hupaswi kupunguza hata kidogo kwa wakati huu, hiyo ndio maana ya “aliye juu ya dari asishuke chini na aliye shambani asirudi nyuma.”

Bwana anatuambia tena tumkumbuke mke wa Lutu (Luka 17:32), unajua kilichomfanya mke wa Lutu kugeuka na kuwa jiwe la chumvi, ni kwasababu alishuka juu ya dari kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake,

Mke wa Lutu anamwakilisha MKRISTO ambaye alishaokolewa huko nyuma, kumbuka Mke wa Lutu mwanzoni aliitika kabisa wito wa kutoka Sodoma, kwa kuyatambua maovu yote yaliyokuwa yanatendeka kule, kwamba wale watu walikuwa wanastahili hukumu , kwa kujua hilo aliamua kabisa kuyaacha mambo ya Sodoma na kuondoka, Lakini baadaye katikati ya safari alianza kujiona anavutiwa na mambo ya nyuma kuliko ya mbele, akianglia mbele haoni majumba, mali, wala raha, akiangalia nyuma anaona fahari, mali, starehe, karamu, mashamba, n.k. Hivyo akaanza kushawishika kidogokidogo kuyafikiria na kuyatamani aliyoyoaacha nyuma Hivyo matokeo yake akageuka, akaangamia na kuwa jiwe la chumvi.

Ndugu yangu mkumbuke MKE WA LUTU. Kumbuka dunia ya leo hii imejaa maovu ya kila namna, hivyo usitazame wimbi la watu wengi wanafanya nini, usitazame kwasababu vijana wote wanafanya anasa na wewe ufanye, kwasababu wanawake wote wanavaa vimini na wewe uvae kwasababu watu wote wanazini na wewe uzini, Biblia ilishatabiri katika siku za mwisho watakatifu watakuwa wachache, na upendo wa wengi utapoa, kama zilivyokuwa katika siku za Nuhu na siku za Lutu, Hivyo ukiwa wewe ni mkristo na umeacha mambo ya ulimwengu huu, zidi kujitakasa, maana siku si nyingi Mungu atauteketeza huu ulimwengu kabisa na watakaopona ni watakatifu ambao watakuwa ni wachache sana, mimi na wewe tuwe miongoni mwao….

Lakini ikiwa hujampokea Yesu, ni heri tu ukafanya maamuzi sahihi katika wakati huu ambao bado mlango wa neema upo wazi, usiendelee kukawia kawia na kushikilia dhambi na ulimwengu maana ipo hatari kubwa itakayowakuta watu wote waliokataa neema ya Mungu sasa ambayo inapatikana bure. Hivyo tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa kisha tafuta ubatizo sahihi yaani wa kuzamishwa kwenye maji mengi na Kwa jina la Yesu Kristo ili upokee kipawa cha Roho Mtakatifu, kumbuka tena muda ambao umepewa kufanya maamuzi ni leo na sio kesho maana haujui kesho.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *