Kwanini ni lazima kuzaliwa mara ya pili?

Biblia kwa kina No Comments

Kwanini ni lazima kuzaliwa mara ya pili?

Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”

Hapo maandiko yanatupa jibu la moja kwa moja kwamba mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuona ufalme wa Mungu. Ndio maana ni lazima kuzaliwa mara ya pili.

Sasa, kabla hatujaona kuzaliwa mara ya pili kukoje? Hebu tuone ni kwasababu gani hatuwezi kumuona Mungu pasipo kuzaliwa mara ya pili.

Kama tunavyojua kuwa Mungu aliye umba mbingu na nchi ni mtakatifu sana na kwakwe hakuna harufu ya dhambi, sasa hapo mwanzo Mungu alipomuumba mwanadamu, mwanadamu alikuwa mkamilifu (hakuwa na dhambi kabisa kwasababu aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu), hivyo mwanadamu alikuwa anaonana na Mungu uso kwa uso na kuzungumza.. ilikuwa ni desturi ya Mungu kumtembelea mwanadamu pale Edeni bustanini na kuzungumza naye. Lakini kama tunavyojua mwanadamu alikosa uaminifu na hivyo akaenda kinyume na maagizo ya Mungu na hiyo ikawa dhambi kubwa kwake… hivyo ikasababisha Mungu kujitenga na mwanadamu kwasababu tayari mwanadamu ameshachafuka..na kama tulivyoona kuwa Mungu ni mtakatifu na hakuna harufu ya uchafu kabisa kwake…kuanzia ule wakati na kuendelea mwanadamu hakuweza kumuona Mungu tena kama hapo kwanza…na kibaya zaidi ule uzima wa milele uliondolewa kwake.

Hivyo vizazi vyote vya Adamu vilivyofuata baada ya pale havikuwa na ukamilifu, kila mwana wa Adamu aliyetokea duniani kwa kuzaliwa kupitia tumbo la mwanamke..anazaliwa na asili ya dhambi kutoka kwa Adamu (mwanadamu wa kwanza) ambaye alitenda dhambi na kusababisha watoto wake wote waliozaliwa kuwa na dhambi mbele za Mungu. Maandiko yanasema..

Warumi 5:12 Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;

Sasa kwa namna hiyo hakuna mtu aliyeweza kumuona Mungu aliye mtakatifu, na hapo ndipo linalokuja suala la kuzaliwa mara ya pili na pasipo kuzaliwa tena siwezi/hauwezi kumuona Mungu kwasababu tu wana wa Adamu aliyetenda dhambi. Ni sharti tuzaliwe mara ya pili na kufanyika wana wa Mungu ili tuweze kumuona Mungu.

Sasa, tunazaliwaje mara ya pili? Je tunarudi tumboni na kuzaliwa tena? Hilo jambo halipo kabisa. hebu turejee maneno ya Yesu Kristo mkuu wa uzima.

Yohana 3:3-7 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

[4]Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

[5]Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

[6]Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

[7]Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

Umeona maana ya kuzaliwa mara ya pili? Maana yake tunazaliwa kwa maji na kwa Roho. kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa maji na kuzaliwa kwa Roho ni kumpokea Roho Mtakatifu ambaye ndiye Roho wa Mungu.

Kumbuka mpaka hayo yote yafanyike..yaani kubatizwa na kupokea Roho wa Mungu ni lazima kwanza kumwamini Yesu Kristo ambaye ndiye Baba wa wote wanaozaliwa mara ya pili. Kama vile tulipozaliwa mara ya kwanza tunaitwa wana wa Adamu ambaye ndiye baba wa wote wanaozaliwa mara kwanza.. Vivyo hivyo kuzaliwa mara ya pili tunaitwa wana wa Yesu Kristo (wakristo).

Yesu Kristo ni Adamu wa pili, yeye hakuzaliwa kwa mbegu ya mwanadamu bali alifinyangwa kwa mikono ya Mungu mwenyewe kama vile Adamu alipofinyangwa kwa viganja vya Mungu. Je tunalithibitishaje hili..tusome maandiko,

Mathayo 1:18 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

Yesu alizaliwa kwa uweza wa Roho na wala sio kwa ile mbegu ya Adamu wa kwanza ambaye alianguka kwenye dhambi, hivyo Yesu Kristo hakuzaliwa na dhambi na aliishi pasipo kutenda dhambi hata moja, sehemu fulani alisema..

46 “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?” (Yohana 8:46)

Sasa, baada ya kufahamu hayo..bila shaka umeelewa ni kwanini hatuna budi kuzaliwa mara ya pili, unapomwamini Yesu na kwenda kubatizwa kwa usahihi na Roho Mtakatifu akaingia ndani yako, basi unakuwa kiumbe kipya.. unahesabiwa kuwa asiye na dhambi kama Yesu Kristo alivyozaliwa pasipo kuwa na dhambi. Hiyo ni neema ya ajabu sana.

Hivyo ndugu ni muhimu sana kumwamini Yesu ipasavyo katika nyakati hizi..kama bado hujamwamini, na sio kumwamini tu basi, bali na kubatizwa pia kwa maji na kwa Roho..hapo utaweza kumuona Mungu.

Kumbuka sio kila ubatizo tu ilimradi maji, hapana! Ubatizo sahihi ni ule wa MAJI MENGI na KWA JINA LA YESU KRISTO. (Yohana 3:23 & Matendo 10:48)

Na kumwamini Yesu kunaambatana na TOBA.. ishara mojawapo itakayodhibitisha kuwa umemwamini Yesu ni kuwa tayari kuacha dhambi zote na udunia.

Ukiona bado unaupenda ulimwengu..hiyo ni ishara kuwa bado hujazaliwa mara ya pili na huwezi kumuona Mungu, ukiona dhambi na tamaa za kidunia bado zinakusumbua, kuna uwezekano kuwa bado hujazaliwa mara ya pili kwasababu wote waliozaliwa mara ya pili.. dhambi haina nguvu juu yao.

Hivyo ndugu fanya juu chini uzaliwe mara ya pili kabla mlango wa neema haujafungwa. Kwa maana hakika muda uliobakia ni mfupi sana na wewe mwenyewe haujui mwisho wako ni lini?

Maran atha.

Washirikishena wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *