KWASABABU MSIPONISADIKI YA KUWA MIMI NDIYE MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU.
Yohana 8:21-24 “Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.
[22]Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?
[23]Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
[24]Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU.
Usife na dhambi zako!!
Jina la Mfalme Mkuu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maneno yake ambayo ni mwanga wa njia zetu, na taa iongozayo miguu yetu (Zab. 119:105)
Leo tutajifunza kwa ufupi, umuhimu wa kutubu dhambi kabla ya kumaliza haya maisha, kuna hatari kubwa sana pale mtu anapokufa na dhambi zake, kitu ambacho labda wengi hawajui ni kwamba mtu akifa mifupa itakwenda kuchimbiwa kaburini, nguo zitachimbiwa ardhini, nyama ya mwili wake itachimbiwa na kuoza lakini dhambi zake alizonazo atavuka nazo upande wa pili…biblia inatuonyesha kuwa kitu pekee kinachomfuata mtu anapokufa sio vitu alivyonavyo ikiwa na maana ya mali, fedha, uzuri wake, n.k. kitu pekee kinachomfuata mtu anapokufa ni matendo yake, Tunasoma katika Ufunuo 14:13 biblia inasema..
“Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, HERI WAFU WAFAO KATIKA BWANA tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; KWA KUWA MATENDO YAO YAFUATANA NAO.”
Umeona hapo, ana heri mtu yule anayekufa katika Bwana yaani katika Kristo Yesu, maana dhambi haipo ndani yake bali ni matendo mema ndiyo yatakayomfuata na huko aendako atakwenda kupumzishwa mahali pema, lakini kinyume chake ni ole kwa mtu yule afaye nje ya Yesu Kristo kwa maana dhambi inakaa ndani yake na hivyo anapokufa matendo yake yote mabaya yatamfuata na hivyo hatapata pumziko la amani bali mateso ya milele. Ndio maana Bwana alisisitiza kwamba watu wote wamsadiki yeye ili wasife na dhambi zao. (Kumbuka dhambi kubwa ni kutomwamini yeye)
Hivyo ndugu usijidanganye wala usikubali kudanganyika kuwa kuna nafasi ya pili ya kutubu dhambi baada ya kufa.
Yapo mafundisho mengi yanayohubiri kuwepo kwa nafasi ya pili ya kusamehewa moto wa milele baada ya kufa…Miongoni mwa mafundisho hayo ni mafundisho ya kupitia Toharani. Lengo kuu la mafundisho haya ni kuwapa watu wanaoishi katika dhambi matumaini kwamba hata wakifa katika dhambi zao bado watakuwa na nafasi ya kutolewa kwenye mateso hayo ya milele na kuingia paradiso, na maombi ya watakatifu waliopo duniani yanaweza kupunguza mateso ya kule.
Haya ni moja ya mafundisho ya shetani yaliyobuniwa kuzimu kwa ujuzi wa hali ya juu yanayowapa watu matumaini na faraja za uongo…shetani anajua watu wanapenda faraja….Alijua Hawa anapenda faraja ndio maana uongo wa kwanza alioutumia ni uongo wa faraja…alimwambia Hawa kwamba “hakika hamtakufa” wakati Bwana alishawaambia wakila tu “watakufa”
Hivyo shetani ni Yule Yule aliyoyatumia Edeni kuwaangusha watu wa kwanza kuumbwa (Adamu na Hawa) ndio hayo hayo anayoyatumia kuwaangusha watu siku za mwisho (yaani mimi na wewe) hivyo tusipokuwa makini kidogo tu! Ni rahisi kwenda na maji!
Mahubiri ya Toharani yatawafanya watu wengi sana wajute siku ile, watakapokwenda huko na kugundua kuwa hakuna kitu kama hicho cha kupata nafasi ya pili. Walidanganywa! Kuna hatari sana ukifa na dhambi.
Ingekuwa hakuna tatizo katika kufa ukiwa na dhambi na kwamba kuna nafasi nyingine ya kuokoka ukiwa kule…Bwana Yesu asingesema hivyo…jiulize sana kwanini ahusishe “kifo” na “dhambi” maana yake ukishakufa na dhambi ndio basi tena…ndio maana alikuwa anakazana kuwaambia watubu kabla ya kufa! Kwasababu hakuna tena toba, wala injili baada ya kifo..kinachofuata baada ya hapo ni hukumu..
Waebrania 9: 27 “ Kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;
Hivyo ndugu, ni vema utazame hatima ya maisha yako ya milele sasa, maana kifo kipo mbele yako na haujui siku wala saa, Ni heri leo ukamwamini Yesu na ukadhaniria kutubu dhambi zako kwa kumaniasha kuziacha kabisa na kwenda kubatizwa kwa jina lake ili upate ondoleo la dhambi zako na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu atakayekusaidia kuishi maisha matakatifu ili parapanda ikilia leo uende na Bwana au ukifa uende kupumzishwa mahali pema peponi.
Usifurahie tu kuwa na vitu vya dunia hii na huku hujapata ondoleo la dhambi maana siku ukifa hizo vitu havitakufuata, bali ni matendo yako ndiyo yatakufuata, biblia inasema..
“Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
[17]Maana ATAKAPOKUFA HATACHUKUA CHO CHOTE; UTUKUFU WAKE HAUTASHUKA UKIMFUATA.
Umeona hapo, usiridhike tu kuwa na magari mazuri, nyumba nzuri, elimu kubwa, ni kweli kuwa na vitu hivyo sio vibaya.. lakini unapaswa kufahamu kuwa vitu hivyo havitakufuata utakapokufa..bali ni matendo yako ndiyo yatakufuata sawa sawa na Ufunuo 14:13.
Bwana anatuonya hapo juu! Kwamba tusipomwamini tutakufa katika dhambi zetu! Je! Na wewe unataka kufa katika dhambi zako? Kama sio basi ni vema ukakata shauri leo la kumgeukia Bwana Yesu, akusafishe dhambi zako na akuoshe kabisa…unachotakiwa kufanya ni kutii msukumo uliopo ndani yako unaokusukuma kuacha dhambi na kumgeukia mwokozi, ujumbe huu unaweza ukawa ni wa kwako kukubadilisha.
Chakufanya ni kutii huo wito kwa kuamua kwa dhati kwamba kuanzia leo mimi na dhambi basiii, disko ndio mwisho leo, kuchat chat ovyo katika mitandao kwenye vitu visivyo na maana ndio mwisho, kutukana ndio mwisho, kusikiliza miziki ya kidunia ndio mwisho, na unaifuta yote sasahivi bila kuacha wimbo hata mmoja, na unakata kila mnyororo, unasema mimi na uasherati basi, na wale wanawake au wanaume unaotembea nao sasa inatosha, unawapigia simu na kuwaeleza maamuzi yako, na unawaacha kabisa…na unachukua msalaba wako unamfuata Yesu wewe kama wewe.
Baada ya hapo ile nguvu ya Roho itakuvaa itakayokuwezesha kutokutamani hayo mambo tena…utakuwa hujilazimishi kujizua kutukana, au kuiba, au kuzini, n.k itakuwa ni kitu kinachotoka ndani chenyewe (kama vile usivyotumia nguvu yoyote kusukuma damu kwenye moyo wako)…na utaona amani Fulani ya ajabu imekuingia Ukiona hali kama hiyo imekuja ndani yako fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu huyo..Lakini ukikaidi sauti yake na kuendelea na ulimwengu huu wa kitambo utakufa katika dhambi zako na hakutakuwa na nafasi ya pili tena huko uendako.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.