Je umeushinda ulimwengu?
Yohana 16:31 “Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa?
[32]Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami.
[33]Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; MIMI NIMEUSHINDA ULIMWENGU.”
Shalom mwana wa Mungu..jina la Bwana Yesu Kristo mkuu wa uzima libarikiwe sana, Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Moja ya ishara kuwa tumemwamini Yesu Kristo kweli kweli na tumefanyika wana wa Mungu sawa sawa na Yohana 1:12 ni kuushinda ulimwengu..kwa kuwa wote waliofanyika wana wa Mungu/waliozaliwa na Mungu kupitia kumwamini Yesu Kristo wamepewa huo uwezo wa kuushinda ulimwengu.
1 Yohana 5:4 Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.
[5]Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?
Ukiona bado ulimwengu unakutaabisha, huwenda bado hujafanyika Mwana wa Mungu!! Na wana wa Mungu ndio watakaourithi ufalme wa Mungu TU! aliowekewa na Baba yao.
Tunaushindaje ulimwengu?
Tunaushinda ulimwengu kwa kuacha kazi zake mbovu na mitindo yake yote. Utauliza kazi za ulimwengu huu ni zipi? Ni pamoja na matendo yote yanayouburudisha mwili ikiwemo uzinzi, uasherati, ulevi, utumiaji wa madawa ya kulevya, anasa, tamaa za macho, fashion, n.k mtu aliyezaliwa na Mungu ni lazima ashinde hayo yote. Lakini pia kuushinda ulimwengu ni pamoja na kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa.
Tito 2:11 Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
[12]nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;
Kuushinda ulimwengu ni pamoja na kukataa mabaya yote ya kidunia, ni pamoja na kustahimili dhiki na majaribu mbali mbali ya hapa na pale… kwasababu ni wazi ukiwa mwana wa Mungu huwezi kukwepa dhiki za ulimwengu huu. Na moja ya dhiki ambayo utakutananayo ni kuchukiwa na ulimwengu, na unapaswa kuushinda kwa kukubali kuchukiwa na hata kutengwa na walimwengu kwasababu ya kuwa we ni mwana wa Mungu na hapa sio kwetu, Kristo alisema…
Yohana 15:18 Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.
[19]Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.
Ukizaliwa mara ya pili jiaendae kuchukiwa na ulimwengu, jiaendae kutengwa hata na ndugu zako wa karibu.. wakati mwingine unaweza hata ukafukuzwa kazi na boss wako, ukapitia dhiki kadha wa kadha kutoka kwa walimwengu.. kwasababu tu ya wokovu, kwasababu tu umekataa matendo ya giza na namna ya ulimwengu huu, umekataa mitindo ya uvaaji wa kiulimwengu, umekataa mapambo ya kiulimwengu, umekataa urafiki na ulimwengu, lakini yakupasa ujipe moyo.. kwasababu Kristo alisema yeye ameushinda ulimwengu.. akaishi pasipo kutenda hata dhambi moja, yeye alikubali kuchukiwa kabisa na ulimwengu..akaanikwa uchi wa mnyama msalabani..na hapa anatuambia na sisi hatuna budi kuchukiwa na ulimwengu na hivyo tujipe moyo ikiwa na maana kama yeye ameushinda huu ulimwengu na sisi pia tuliomwamini tutashinda tu, Hiyo ni lazima.
Je! Umeushinda ulimwengu? Kama bado unaupenda ulimwengu ni wazi kuwa we ni wa ulimwengu na hivyo mwisho wako ni kuharibiwa, kwasababu huu ulimwengu umeshahukumiwa na hukumu yake imekaribia.
Kwahiyo ni heri leo ukamgeukia Yesu akuoshe dhambi zako na akupe uwezo wa kuwa mwana wa Mungu ili uweze kuushinda ulimwengu na mwisho kuketi pamoja na Baba katika ulimwengu ujao.. kama yeye alivyoshinda na akapewa hiyo nafasi. Kumbuka tunaishi ukingoni kabisa mwa nyakati.. Kristo yupo mlangoni.. fungua moyo wako aingie kabla hujachelewa.
Ufunuo wa Yohana 3:20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
[21]Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
[22]Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.