TUSILEWE KWA MVINYO BALI TUJAZWE ROHO

Biblia kwa kina No Comments

TUSILEWE KWA MVINYO BALI TUJAZWE ROHO

Neno la Mungu linasema katika..

Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;

Katika biblia, mtu ambaye amejazwa Roho Mtakatifu anaonekana kama mlevi, kwasababu ya tabia zake kufanana na tabia za walevi.

Hebu tusome maandiko yafuatayo ili tulithibitishe hili.

Matendo ya Mitume 2:1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

[2]Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.

[3]Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

[4]Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.

[5]Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.

[6]Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

[7]Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?

[8]Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?

[9]Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia,

[10]Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,

[11]Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

[12]Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?

[13] WENGINE WALIDHIHAKI, WAKISEMA, WAMELEWA KWA MVINYO MPYA.

Watu hao walionekana kama walevi kwasababu walijazwa Roho, Roho Mtakatifu anafananishwa na mvinyo/kilevi ambacho kikijaa ndani yako ni lazima tu ikulevye na utaonekana ni mlevi kama walevi wanaokunywa pombe, isipokuwa we sio mlevi wa pombe, lakini katika roho unakuwa na tabia za mlevi wa pombe/mvinyo.

Hebu tuangalie mtu mwingine ambaye alijazwa Roho Mtakatifu akaonekana kama mlevi.

1 Samweli 1:10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana.

[11]Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.

[12]Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake.

[13]Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli ALIMDHANIA KUWA AMELEWA.

[14]Ndipo Eli AKAMWAMBIA, JE! UTAKUWA MLEVI HATA LINI? Achilia mbali divai yako.

[15]Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila NIMEIMIMINA ROHO YANGU MBELE ZA BWANA.

Umeona hapo, Hana alipozama kwenye maombi..akajazwa Roho Mtakatifu na Eli alipomwangalia alimdhania kuwa amelewa.

Hata na sisi tunapojazwa Roho Mtakatifu tunadhaniwa kuwa ni walevi.. kwasababu gani? Kwasababu ya tabia ambazo tunakuwa tunaonesha.

Hebu tuangalie baadhi ya tabia za walevi.

1) Hana kumbukumbu

Siku zote mlevi akishalewa kwa kupindukia kabisa..huwa anapoteza ufahamu kwa wakati huo, hivyo hakumbuki tena chochote alichokifanya au alichofanyiwa wakati alipokukuwepo kwenye ulevi.

Hali kadhalika pale tunapojazwa Roho.. tunakuwa na hiyo tabia ya mlevi ya kutokukumbuka mambo mabaya tuliyofanyiwa, ndio maana mkristo wa kweli aliyejazwa Roho Mtakatifu sio rahisi kuwa na kinyongo au uchungu kwasababu hana tabia ya kukumbuka na kuhifadhi mambo yale mabaya aliyofanyiwa.

Mkristo akisamehe anakuwa amesehe kweli na anasahau kabisa.. Kwasababu amejazwa Roho, na moja ya tunda la Roho ni UPENDO ..na moja ya tabia ama sifa ya upendo wa Roho Mtakatifu ni kutohesabu mabaya (soma 1Wakorintho13:5)

Hivyo mtu mwenye upendo wa kweli wa ki-Mungu katika roho ni kama mlevi ambaye amelewa kwa mvinyo mpaka akawa hana kumbukumbu tena, hajui hata ni nani jana alimpiga..au alimwibia! Vivyo hivyo kwa mkristo aliyejazwa Roho.

2) Tabia nyingine ya mlevi ni kwamba hasikii maumivu akiwa kwenye hiyo hali ya kulewa.

Mlevi akilewa huwa hasikiagi tena maumivu..anaweza akaangukia kwenye miiba akachomwa na asisikie chochote hadi kesho yake au kesho kutwa baada ya pombe kuisha.

Ni vivyo hivyo kwa mkristo aliyejazwa Roho Mtakatifu..si rahisi kuhisi maumivu pale anapokutana na mazingira au hali zinazoleta maumivu, mfano kufiwa, kudhulumiwa, kuibiwa, kuishiwa, na hali zote ambazo zinawafanya wanadamu wapate maumivu katika mioyo yao.

Mkristo wa kweli aliyejazwa Roho.. atakutana na changamoto kama hizo lakini hizitamuondolea furaha yake kabisa, ndio ataumia kama mwanadamu lakini hatapoteza kabisa furaha na amani kiasi cha kuchanganyikiwa, kwasababu Roho Mtakatifu anampa amani, furaha, uvumilivu katika kipindi hicho au apitiapo katika hali hiyo. tofauti na watu wengine wasio na Roho ambao..wakitikiswa tu kidogo wanaumia na kuhuzunika mpaka wanakata tamaa kabisa ya kuishi, wengine wanaishia kujiua, kulia, kukonda, kuzimia, n.k

Hivyo mkristo aliyejazwa Roho Mtakatifu kweli..akikutana na hizo changamoto, anaumia tu kidogo..kisha anaendelea mbele kama kawaida na anakuwa na furaha kabisa, jambo linalomfanya aonekane kama mlevi.

3) Tabia ya tatu ya mlevi ni kuongea lugha asiyoifahamu.

Bila shaka umewahi kumuona mlevi jinsi anavyoongea..huwa anatamka maneno ambayo unaweza usielewe kabisa, wakati mwingine anaongea hata lugha nyingine ambayo akiwa katika hali ya kawaida hawezi kuongea, mfano labda utasikia anatamka maneno ya lugha ya kiingereza ingawa hata hajui hiyo lugha, au anaongea maneno yasiyoeleweka..tena huwa mlevi anaongea sana na pia wakati mwingine anaimba hata nyimbo asiyoijua.

Na halikadhalika mtu aliyeookoka akajazwa Roho Mtakatifu..anajikuta anazungumza lugha nyingine ambayo hajawahi kuzungumza hapo kabla, anajikuta ananena lugha ambaye hata wakati mwingine haelewi maana yake, hiyo ni lugha ya rohoni ambayo Roho Mtakatifu anamjalia huyo mtu kunena kwa lengo la kumjenga nafsi yake au kujenga kanisa..na mara nyingi hizi lugha hudhihirika wakati mtu yupo kwenye maombi, kwa kuwa sisi hatujui kuomba ipasavyo.. Roho Mtakatifu huwa anatusaidia kuomba vizuri katika Roho, na anaomba na sisi kwa kuugua sana na katika kuomba ndivyo tunajikuta tunanena lugha mpya, ambayo mtu aliye nje anaweza akadhani kuwa tumelewa.. kama ilivyokuwa katika ile siku ya pentecoste ndivyo walivyodhaniwa..na ndicho pia kilichomkuta Hana..Eli alimdhania kuwa amelewa kwasababu Roho Mtakatifu alikuwa anaugua ndani yake kiasi kwamba huku nje ni mdomo tu ilionekana inaongea pasipo kusikika sauti yake mwenyewe…hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kujazwa Roho.

4) Tabia ya nne ya mlevi ni kuyumba yumba akiwa anatembea.

Hii ni tabia ya walevi wengi (kumbuka tunawazungumzia walevi na sio wanywaji), hivyo hii ni moja ya tabia ya walevi wengi..mara nyingi akitembea njiani anaenda upande upande, hawezi kusimama tu sehemu moja au kutembea kawaida. Na hii ni moja ya tabia ya mtu aliyezaliwa mara ya pili. Biblia inasema mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa kama upepo, mara huku mara kule..anakuwa kama mlevi ambaye anatembea kwa kuyumba yumba..anafuata muelekeo wa kile kilevi kinavyomwendesha, Vivyo hivyo na mtu aliyezaliwa mara ya pili na akajazwa Roho Mtakatifu.. Roho Mtakatifu anakuwa anamuongoza huku na huku asikojua yeye..Yohana 3:7-8. Bwana anamwambia Nikodemu..

“Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

[8]Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.”

Ndio hapa utakuta mtu maisha yake yanabadilika balika kila siku, Watu wa nje wanaweza kushangaa mbona huyu mtu tabia yake imebadilika kwa ghafla hivi,wasijue ni nani aliyembadilisha, wakijaribu kachunguza labda ni dini hawaoni, labda ni dhehebu hawaoni, labda ni mwanadamu hawaoni, na ndio hapo utaona maisha ya yule mtu yanabadilika, pengine mambo aliyokuwa anapenda kuyafanya hapo mwanzo yanageuzwa ghafla, maisha aliyokuwa anaishi nyuma yanageuka ghafla, mara nyingine atajikuta anachukia hata kufanya baadhi ya vitu alivyokuwa anavifanya nyuma, anajikuta kiini cha maisha yake ni kumwangalia Bwana YESU tu mahali popote alipo…Baadhi ya mambo yasiyokuwa na maana yataanza kumkera, anaanza kutokujiona kuwa huru akiwa katika vikao vya usengenyaji, tofauti na alivyokuwa hapo mwanzo..

Hii yote inatokea ni kwasababu yule Roho aliye ndani yake humsukuma kufanya vitu ambavyo hata pengine yeye mwenyewe hajui ni kwanini anavifanya, saa nyingine anaweza akadhani ni kwa akili zake anafanya hivyo.Au ni kwasababu ametokea tu kupenda mwenyewe Lakini ukweli ni kwamba sio yeye anafanya hivyo bali ni Roho wa Mungu ndani yake atembeaye kama upepo usioonekana anamwelekeza asikojua yeye.. kama tu vile mlevi anapoongozwa na ule mvinyo mahali asikojua yeye.

5) Tabia ya tano ya mlevi ni kutokuwa na aibu.

Mara nyingi tumewashudia watu ambao wanatumia vilevi ili waweze kusimama mbele za watu au kufanya jambo fulani, kwasababu wakiwa kwenye hali ya kawaida wanakuwa na aibu ya kufanya jambo lile. Hivyo mtu akishalewa anakuwa haoni tena ile aibu, kama alikuwa anaona aibu kuzungumza mbele za watu au kusema na mtu Fulani..akishalewa anazungumza bila aibu kabisa.

Na hali kadhalika mtu aliyelewa kwa mvinyo wa Roho Mtakatifu, kama alikuwa na aibu aibu…,ile hali inaondoka kabisa. anajikuta anatangaza habari njema ya Yesu Kristo bila kufikiri fikiri, kama alikuwa anaona aibu kumshudia mwingine habari za wokovu.. baada ya kujazwa Roho, ile aibu inapotea, anajikuta anafanya kazi ya Mungu bila kuona aibu aibu, anamwimbia Bwana na kumsifu katikati ya kusanyiko kubwa na wala haoni aibu..ni kwasababu gani? Ni kwasababu amelewa na mvinyo mpya wa Roho Mtakatifu..hata na sisi tukitaka kufanya kazi ya Mungu au hata kazi zetu pasipo kuona haya, suluhisho pekee ni kujazwa Roho Mtakatifu na sio kutafuta njia zingine.

6) Tabia nyingine ya mlevi ni kutokuogopa chochote.

Mlevi haogopi chochote kilicho mbele yake, haogopi mtu yoyote, haogopi mkubwa wala mdogo, haogopi hatari yoyote, wala hana hofu na maisha..yeye hajui kesho..huyo ndiye mlevi.

Vivyo hivyo na sisi wana wa Mungu tunapojazwa Roho wa Mungu..ile hofu ya maisha inaondoka ndani yetu, hofu ya kufikiria kesho nitaishije, itakuwaje!, Unakuwa kama mlevi, huogopi chochote.. iwe ni kifo, au iwe ni hatari yoyote ile, ukiona bado unahofu ndani yako ya kitu chochote ni ishara kuwa huwenda bado hujajazwa Roho, yawezekana kweli ulimpokea siku ile ulipomwamini Yesu na kutubu dhambi zako lakini huwenda bado hujajazwa kikamilifu…ndio maana hofu inakutawala, ndio maana unaogopa wachawi, ndio maana unaogopa majini, ni kwasababu hiyo hujajazwa Roho Mtakatifu, ndio maana hata unaogopa kushuhudia habari za Kristo, unaogopa sheria za nchi, unaogopa ogopa watu fulani ambao wanasema injili isihubiriwe.

Mitume walipojazwa Roho Mtakatifu baada ya pentecoste maisha na mienendo ya mitume ilibadilika  ghafla tangu ule wakati, walipokea ujasiri usio wa kawaida kuhubiri injili, walijawa na Imani kwa Mungu, hawakuwaogopa maadui zao tena, na kwenda kujificha kama ilivyokuwa pale mwanzo.. Mara nyingi roho alikuwa akiwatwaa na kuwapeleka wasikojua, na huko wanapofika wanalihubiri Neno la Mungu kwa ushujaa mwingi..Tunamwona mtu kama Filipo alitwaliwa na Roho na kupelekwa kule Roho alipopenda kumpeleka.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI.

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Unaona umuhimu wa kujazwa Roho Mtakatifu, huwezi kufanya kazi ya Mungu kikamilifu kama bado hujajawa Roho, Hivyo kuna umuhimu sana wa kujawa Roho Mtakatifu kama mwamini.

7) Tabia ya upendo.

Kama umeshawahi kuwasogelea walevi.. utakuwa unaelewa hii tabia, mara nyingi walevi huwa wanapendana wao kwa wao… wakikutana wote kwa pamoja..wanafurahi sana, mmoja akiwa hana ela ya kununulia pombe.. wengine wanamnulilia.. hivyo ni watu wa kushikamana sana.

Na halikadhalika na sisi watoto wa Mungu pindi tunapolewa kwa Roho Mtakatifu..tunakuwa na hiyo tabia ya upendo ambao huo unaenda mpaka kuwapenda hata maadui zako.

Kwa ufupi hizo ndio tabia chache za walevi ambao na sisi kama watoto wa Mungu hatuna budi kuwa na tabia hizo..kama tulivyojifunza, na tabia hizo zinakuja ndani yetu pale tunapojazwa Roho Mtakatifu ambayo ndiyo kama kilevi chetu.

Pengine utauliza nifanye nini ili nijazwe Roho Mtakatifu?

Roho Mtakatifu anaweza kuendelea kujaa ndani yetu, kwa walau mambo makuu manne.

Kwa kuomba;

Biblia inasema, Luka 13:13 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

Ukiwa mtu wa kuomba, na kukataa uvivu kwa kutokusali walau saa moja kwa siku, ndivyo utavyojiongezea mafuta yako ya rohoni na hivyo Roho Mtakatifu atapata wigo mpana wa kuyatawala maisha yako siku baada ya siku.

2.  Kwa kujifunza kwa bidii Neno la Mungu..;

Neno ndio chakula cha uzima wa mtu. Usipojibidiisha kujifunza Neno la Mungu, kutafuta habari za uzima, usidhani kuwa Roho Mtakatifu atapata nafasi ya kukufundisha kitu chochote ndani yako. Kwasababu Mungu yupo katika Neno lake(Sauti ya Mungu ni Neno lake). Ukiwa umeokoka, halafu unaona uvivu kujifunza Biblia basi ujue Roho wa Mungu ameshazimika ndani yako kitambo..Na hivyo hata wakati wa unyakuo utakapofika utafananishwa na wale wanawali wapumbavu.

3.  Kaa mbali na uovu;

Siku zote dhambi inavutia, lakini mwisho wake ni mbaya..Tunapoivumilia dhambi katika maisha yetu ndivyo Mungu anavyouficha uso wake. Na matokeo yake Roho Mtakatifu anazimika, au anaondoka kabisa ndani yetu.(Isaya 59:2)

4.  Tangaza habari njema: 

Ukiwafundisha wengine, na wewe hapo hapo Roho wa Mungu anakufundisha, ukiwafungulia wengine hazina ya maneno ya uzima, Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kukufunulia wewe Zaidi na kukutumia, ili kuwaokoa watu wake..Na hivyo ni sharti atakaujaza tu Roho wake, kwasababu siku zote unafanya kazi yake..Na hapo utakuwa na nafasi nyingine ya kuwa karibu na yeye.

Hivyo tusiridhike tu, na hali za kiroho tulizopo, tukajificha nyuma ya kivuli cha Neno nimeokoka..Tunapaswa tujiulize Je! kweli katika roho tunatibia za walevi? Je tuna upendo wa kiMungu, je hatuna vinyongo? Hatuna hofu, n.k, kumbuka ni watakatifu tu waliojazwa Roho Mtakatifu ndio watakaonyakuliwa kumlaki Bwana mawinguni.. kwakuwa hao ndio wale wanawali warevu. Hivyo kama bado Roho Mtakatifu hajatulewesha… basi huu ndio wakati wa kufanya bidii kutafuta ujazo wake, kwa kuhakikisha kuwa kila siku Roho Mtakatifu anapata nafasi maishani mwetu..Ili ile siku ambayo hatujui ni lini itakapotujilia kwa ghafla basi tuwe na uhakika kuwa UNYAKUO hautatupita. (Kumbuka unyakuo umekaribia sana kuliko tunavyodhani)

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *