USIRUHUSU CHAWA WAINGIE NDANI YAKO
Jina kuu la Bwana Yesu Kristo libarikiwe milele daima. Karibu tujifunze biblia.
Kabla hatujaangalia chawa wanawakilisha nini katika roho, hebu kwanza tutazame chawa wa kawaida na tabia zao kwa ufupi.
Kama wengi tunavyojua chawa ni mdudu ambaye hukaa au kuishi kwenye mwili, nywele au nguo za kiumbe mchafu.
Chawa hutokana na uchafu. Mtu mwenye chawa mara zote hujikuna na kukosa utulivu.
Kwahiyo moja ya tabia ya chawa ni kupenda kukaa kwenye sehemu iliyo na uchafu. Kwa mfano mtu akivaa nguo mpya iliyoshoonywa..halafu akakanayo mwezi ndani ya mwili wake bila kubadilisha na tena asioge..ni wazi kuwa utakutana na chawa wengi tu kwenye mwili wake.
Sasa tukirudi kwenye mambo ya rohoni, wapo pia chawa wa rohoni ambao ndio wabaya zaidi ya hawa wa mwilini ambao wanaishia tu kuharibu mwili, wapo chawa wa rohoni ambao si tu wanaharibu mwili bali wanaharibu zaidi roho. Na Bwana alisema ”Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu;..”(Yohana 6:63).. Ndio maana sehemu nyingine biblia inasema “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”. (Mithali 4:23). Moyo unayozungumziwa hapo sio huu wa nyama bali ni roho.
Hivyo ili tuweze kulinda roho zetu kwa ukamilifu hatuna budi kuthibiti wale chawa ambao wanaweza wakaleta uharibifu kwenye roho zetu.
Sasa ili kuelewa hawa chawa ni wapi? Hebu tuangalie uchafu wa rohoni ni upi, kwakuwa chawa huvutwa na uchafu kama tunavyojua.
Uchafu wa rohoni ni pamoja na dhambi zote zinafanyika nje ya mtu na ndani ya mtu. Kwa mfano tukisoma biblia tunaona Mungu anatuonya kwamba tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwilini na rohoni ambao ndio hizo dhambi za nje na ndani…na ndizo zinazovuta wale chawa wa rohoni kuingia ndani ya mtu.
2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na UCHAFU WOTE WA MWILI NA ROHO, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”.
Hapo anaposema tujitakase na Uchafu wote wa mwilini. Anamaanisha kuwa tujiweke mbali na dhambi zote zinazozalika katika miili yetu. Mfano wa dhambi hizi ni kama vile, uzinzi, ulevi, wizi, uvutaji sigara, utukanaji, uvaaji mbovu, kama vile vimini na suruali kwa wanawake, kujichubua, kujipaka make-up, kutoa mimba, kuvaa milegezo, kujichoraji tattoo, na ushoga, utumiaji wa madawa ya kulevya na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, ambayo asili yake ni mwilini..huu ni uchafu wa mavazi ya nje ambayo mtu akiwa na moja ya uchafu huo..moja kwa moja anaingiwa na chawa.
Na pale aliposema tuweke kando Uchafu wa rohoni, Anamaanisha dhambi zote zinazotoka ndani ya mtu, ambazo hazihusiani na mwili moja kwa moja, mfano wa dhambi hizi ni kama vile, wivu, hasira, tamaa, mawazo mabaya, unafki, uchoyo, husuda, fitna, majigambo, kiburi, ibada za sanamu, uongo. Hizi ni dhambi ambazo zinazalika ndani, na Mungu anazichukia sana, kama vile tu anavyozichukia zile zinazozalika katika mwili…na huu ndio uchafu ambao unampelekea mtu avamiwe na roho chafu/mapepo ambao ndio wanafananishwa na chawa.
Kumbuka mtu msafi si rahisi kuwa na chawa.. halikadhalika mtu msafi rohoni ni vigumu kuingiwa na mapepo. Tabia mojawapo ya mapepo ni kupenda kuingia na kuweka makao ndani ya mtu mchafu.
Na mtu mchafu sio mlevi tu, au muasherati, au mtukanaji, bali ni mtu yoyote ambaye hajaokoka… yaani hajamwamini Yesu Kristo na kumpokea kikamilifu.
Biblia inasema..
Luka 11:24 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,
25 Nitairudia nyumba yangu niliyotoka.
26 Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza”.
Ukitafakari vifungu hivyo, utagundua tabia kadha wa kadha za mapepo;
Jambo la kwanza huwa linatabia ya kwenda kuishi mahali pasipokuwa na maji;
Ni adui wa maji; Sasa ni lazima ujue sehemu isiyokuwa na maji ni ipi kiroho? Ni moyo mkavu, usiokuwa na chemchemi ibubujikayo maji ya uzima ndani yake, yaani Roho Mtakatifu..
Yohana 4:14 “walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”.
Mtu yeyote asiyekuwa na Kristo ndani yake, tayari kwa namna moja au nyingine ndani yake kuna mapepo, kwasababu ni kukame. Ni sawa na mtu ambaye amekaa muda mrefu bila kugusa maji na kubadilisha nguo, ni lazima tu atakuwa na chawa. Ndivyo alivyo mtu ambaye yupo nje ya Kristo…hata kama haanguki anguki na kupiga kelele.. hakosi kabisa kuwa na aina fulani ya pepo mchafu… kwasababu naye ni mchafu rohoni.
Na hata kama umeokoka kweli kweli..unapaswa kuwa makini sana na wokovu wako maana mapepo/chawa wanatafuta makao. Hivyo jihadhari na uchafu uwao wote wa mwilini na roho.
Ukiwa mtu wa vinyongo, na kutokusamehe, tayari umefungua mlango wa mapepo kukuvamia na kukuharibu..Ukigeuka na kuwa mwabudu sanamu na mchawi wewe tayari ni ngome ya adui.
Ukiwa mtu wa kuvaa kizinzi, na moyoni unajua kabisa mavazi kama hayo hata ukiitwa kwenye interview ya kazi huwezi kwenda nayo, lakini unaendelea kuyavaa na kukatisha nayo mtaani na hata kuingia nayo kanisani, fahamu kuwa wewe ni kituo cha mapepo.
Lakini leo umesikia neno hili, fungua moyo wako tubu, mwambie Bwana sitaki kuwa kituo cha mapepo, bali unataka kuwa kituo cha Roho Mtakatifu ndani yako. Na kama umedhamiria kutubu kabisa, unachopaswa kufanya baada ya toba hiyo ni kugeuka kikweli kweli, kama kulikuwa na watu hujawasamehe moyoni mwako kutokana na sababu Fulani Fulani, kuanzia dakika hii unawasamehe wote, haijalishi wamefanya kosa gani, kwasababu hata sisi Kristo alitusamehe.
Pia kama ulikuwa ni mzinzi na mwasherati, kuanzia dakika hii unakiri kuuacha kwa vitendo, maana yake Yule uliyekuwa unafanya naye uzinzi, unakata mawasiliano naye, na pia kama ulikuwa unavaa nguo za kizinzi unachoma, wala usiende kuzigawa, unazichoma zote usiache hata moja, na kama ulikuwa unatazama picha za pornograph na unasikiliza miziki ya kidunia katika simu yako unafuta yote kuanzia saa hii, wala usingoje kesho, kwasababu hujui yatakayozalika ndani ya siku moja, biblia inasema hivyo.
Na baada ya kufanya hayo na mengine yote yanayofanana na hayo, hapo toba yako itakuwa ni ya matendo, hivyo Roho Mtakatifu atashuka ndani yako kuhakikisha uyarudii matapishi na kuithibitisha imani yako, na hata kama kulikuwa ndani yako kuna mapepo, yataondoka yenyewe kwasababu Toba inayoambatana na matendo ina nguvu ya kufungua minyororo kuliko kitu kingine chochote, wala huhitaji kukemewa mapepo tena, (Toba ya namna hiyo hakuna pepo litakalosalia), ulichobakisha ni wewe kwenda kutafuta ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa Jina la Yesu Kristo kuukamilisha wokovu wako, kama bado hujabatizwa hivyo. Na baada ya hapo unaendelea kujitakasa na kujiweka katika hali ya usafi ili mapepo wasipate nafasi hata kidogo ndani yako.
Unajitakasa kwa kuwa mwombaji kila siku (muombaji wa masafa marefu), kusoma biblia kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu, kufanya kazi ya Mungu, kukusanyika na watakatifu wenzako.
Ukiwa hivyo basi fahamu kuwa hakuna hoja yeyote ya shetani itakayoshinda juu yako, na mapepo yatawekwa mbali na wewe, na utaishi maisha yasiyo na usumbufu wowote kutoka kwa adui… lakini ukipuuzia na ukaishi maisha machafu, basi fahamu kuwa utakuwa tu kao la kila roho chafu, na mwisho utakufa na kwenda kuungana na hayo mapepo kule shimoni kusubiria hukumu ya ziwa la moto.
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.