
FANYA KAZI YA BWANA BILA KUCHOKA.
Kama we ni msomaji wa biblia..utakuwa unafahamu habari ya Ruthu, alikuwa ni mwanamke wa kimataifa aliyekubali kufuatana na Mungu wa Israeli..kama vile sisi tuliokuwa watu wa mataifa tukakubali kumfuata Mungu wa Israeli na tukafanyika wana wa Israeli kupitia neema ya Yesu Kristo, hivyo tukisoma.. huyu mwanamke alikuwa ni mwanamke wa kuigwa sana, sio tu katika mambo ya rohoni bali hata katika maisha ya kawaida, kwani alikuwa ni mchapakazi, hakuwa na uvivu katika kufanya kazi, alikuwa anaweza akashinda tangu asubuhi hadi jioni huko mashambani. Hebu tumsome kidogo.
Ruthu 2:1 Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi.
[2]Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda.
[3]Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki.
[4]Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki.
[5]Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani?
[6]Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu;
[7]naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; BASI AKAJA, NAYE AMESHINDA TANGU ASUBUHI HATA SASA, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo.
[8]Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu.
[9]Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana.
Na sisi tumewekwa katika shamba la BWANA, hivyo yatupasa kuiga bidii ya Ruthu, tufanye kazi ya Bwana bila kuchoka.
Neno la Mungu linasema katika..
Wagalatia 6:9 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”
Tena sehemu nyingine anasema..
1 Wakorintho 15:58 Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.
Moja ya wema ambayo hatupaswi kuchoka kuwatendea watu ni kuwahubiria habari njema za wokovu, huu ni wema ambayo sio wema tu, bali ni jukumu letu sote kama waamini. Kuhubiri injili ni moja ya agizo tuliopewa, Kwahiyo kila mwamini ni lazima ashughulike ipasavyo katika kuwatendea watu wema huu kwa kuwahubiria/kuwapelekea habari za wokovu unapotikana kupitia Yesu Kristo.
Hivyo ikiwa umeokoka kweli kweli, fahamu kuwa Bwana anatarajia ufanye kazi yake bila kuchoka..kwa maana yeye mwenyewe hakuchoka kutuhubiria habari za ufalme wake.
Utakumbuka ile safari ya Bwana alipokuwa anatoka Uyahudi kwenda Galilaya kuhubiri, maandiko yanatuonyesha kuwa kwasababu safari yake ilikuwa ndefu, ya saa nyingi, ilibidi waweke kituo kwanza kwenye mji mmoja wa wasamaria, wapumzike. Yeye na wanafunzi wake kwenye kile kisima cha Yakobo.
Yohana 4: 5 Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. 6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu AMECHOKA KWA SAFARI YAKE, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

Jua la mchana likiwa kali, anasikia mwili ni mchovu hautaki, kufanya kazi yoyote, njaa zinauma, mpaka mitume wakaondoka kwenda kutafuta chakula mjini. Lakini katika mazingira hayo hayo Analetewa na Mungu mtu mwenye dhambi amshuhudie habari za neema ya wokovu. Ndio Yule mwanamke msamaria.
Lakini Yesu hakuwa na udhuru kwa kusema, huu ni muda wangu wa kupumzika, ni muda wangu wa kulala, ni muda wangu wa lunch nile na wanafunzi wangu. Alitii vilevile katika uchovu wake, akaanza kuongea na Yule mwanamke habari za ukombozi, kwa kipindi kirefu kidogo.
Lakini mwisho wa mazungumzo yao haukuwa bure, Yule mwanamke aliondoka, lakini baada ya muda mfupi alirudi na jopo la watu, ili kuja kumsikiliza Bwana Yesu, maneno aliyoshuhudiwa na yeye (Yohana 4:1-42). Na baada ya hapo tena, Samaria yote ikamwamini, sehemu nyingine mpaka wakawa wanataka hata kumfanya mfalme.
Na vivyo hivyo Bwana anataka tuwe na hiyo nia aliyokuwanayo.
Wafilipi 2:5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;
Hatupaswi kabisa kuchoka kufanya kazi ya Bwana, hatupaswi kuchoka kuhubiri Injili ya Bwana kwa karama tulizopewa. Kila mtu awepo katika huduma yake kila siku. Kama vile tufanyavyo kazi zetu kwa bidii bila kuchoka.
Warumi 12:6 Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;
[7]ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;
[8]mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.
[9]Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.
[10]Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;
[11] KWA BIDII, SI WALEGEVU; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;
Ni mara ngapi tumeshindwa kutimiza makusudi ya Mungu mengi tu, kwa kisingizio cha kuchoka? Kwa kisingizio cha kusema nimetoka kazini, nimefanya kazi wiki nzima, hivyo nimechoka siwezi kwenda kuomba, siwezi kwenda kushuhudia, n.k
Hebu leo ondoa uvivu, amka na anza kumtumikia Mungu kwa bidii, anza kufanyia kazi hiyo karama uliyopewa ili umzalie Mungu matunda, usiwe kama yule mtumwa mvivu ambaye alipewa talanta moja…badala akafanye kazi azalishe faida ili aje kulipwa … yeye alienda kufukia. (Mathayo 25: 24-29).
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.