Kuokoka na kuzaliwa mara ya pili
Jina kuu la Mfalme na Mwokozi YESU KRISTO libarikiwe. Karibu tuongeze maarifa ya kufahamu biblia.
Leo tutafahamu ukweli kati ya kuokoka na kuzaliwa mara ya pili, je ni kuokoka ndio kuzaliwa mara ya pili au kuzaliwa mara ya pili ndio kuokoka? sahihi ni ipi?
Ni vizuri kuelewa na kufahamu maana ya maneno hayo, ili usije ukajihesabiwa kuwa umeokoka na ilihali hujazaliwa mara ya pili!
Kwa ufupi, kuzaliwa mara ya pili ndio kuokoka.
Mtu hawezi akawa ameokoka na hajazaliwa mara ya pili, na halikadhalika mtu hawezi akawa amezaliwa mara ya pili na hajaokoka. Na hapa ndipo wengi tunapokosea pale tunapodai tumeokoka na ilihali hutujazaliwa mara ya pili.
Ni rahisi mtu kutamka kiwepesi bila shaka kabisa kuwa ameokoka hata kama hajazaliwa mara ya pili, na sababu kuu ni kwamba wengi wanatumia hilo neno”nimeokoka” kukataa wokovu wa kweli, na wengine ni kwasababu hawana maarifa sahihi kuhusu wokovu wa kweli. Huwenda wamedanganywa na dini/madhehebu yao au viongozi wao wa kidini kuwa kuokoka ni kuhudhuria kanisani kila week, au kutoa sadaka kwa uaminifu, au kushiriki kufanya kazi ya kanisa na huduma ya kiMungu..ndio kuokoka.
Lakini je! ni kweli?
Inawezekana ikawa ni kweli ila sio ukweli wote bali ni ukweli nusu.
Ukweli mkamilifu ni kwamba “Kuokoka ni badiliko la ndani na nje ambayo mtu anapata baada ya kuzaliwa mara ya pili” Ndio maana tunasema kuokoka ni kuzaliwa mara ya pili”.
Sasa ili tuwelewe maana ya kuzaliwa mara ya pili.. tusome maneno ya Bwana, tufahamu ukweli wote.
Yohana 3:3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
[4]Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
[5]Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
[6]Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
[7]Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.
Kumbe kuzaliwa mara ya pili ni kuzaliwa kwa maji na kwa Roho!. Sasa kuzaliwa kwa maji na kwa Roho ndio kukoje?
Kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa maji mengi na kuzaliwa kwa Roho ni kubatizwa kwa Roho (yaani kupokea Roho Mtakatifu).
Mtu akifuata hizo hatua kikamilifu baada ya yeye kusikia na kutii wito wa Mungu.. atakuwa amezaliwa mara ya pili/ameokoka.
Lakini kama mtu hajatii wito wa Mungu (hajatubu dhambi), na hajafuata hizo hatua… Yaani hajabatizwa kwa maji mengi na hajapokea Roho Mtakatifu, mtu huyo hajaokoka, hata kama atakiri mara mia kuwa ameokoka, hata kama anahudhuria kanisani na kufanya kazi ya Mungu.
Kwahiyo kuokoka ni kusikia injili na kutubu dhambi na kubatizwa kwa maji na kupokea Roho Mtakatifu..hapo utakuwa umefanyika kiumbe kipya/umezaliwa mara ya pili.
Matendo ya Mitume 2:38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Na ukishazaliwa mara ya pili ni lazima tu ujulikane kwa nje, kwa tabia ambazo utakuwa unaonyesha. Kama vile mtoto mdogo aliyezaliwa katika tumbo zipo tabia atakazokuwa anaonyesha katika ukuaji wake. Na halikadhalika mtu aliyezaliwa mara ya pili kuna tabia atakazokuwa anazionyesha katika ukuaji wake na tabia hizo ndizo zinaashiria kuwa mtu huyo amekuwa kiumbe kipya.
Je! Umezaliwa mara ya pili? au unasema tu umeokoka!
Kumbuka mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuona ufalme wa Mungu. Hivyo kama bado hujazaliwa mara ya pili, leo fanya maamuzi sahihi ya kufuata vigezo hizo tulizojifunza.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.