Je! Neno la Mungu limefunuliwa kwako?
1 Samweli 3:7 “Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.”
Kuna mambo huwezi kuyafahamu kama Neno la Mungu halijafunuliwa kwako, utaishia tu kubaki vile vile huku ukidhani umekamilika kumbe bado.
Kwa mara ya kwanza Mungu alipoiumba hii dunia, kuna mambo ambayo hayakuweza kutokea hapo hapo ili dunia hii ikamilike, ilibidi Roho wa Mungu atulie juu ya vilindi vya maji na ndipo Mungu akatamka Neno lake ambalo kupitia hilo dunia ilikamilika. Tukisoma kitabu cha Mwanzo1 ule mstari wa 1 kabisa, Neno la Mungu linasema..
Mwanzo 1:1 Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.
Lakini tukiendelea na mstari wa pili, tunaona kuwa hiyo nchi ilikuwa bado haikukamilika, ilikuwa ukiwa na utupu.
[2]Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.
Sasa, baada ya Roho wa Mungu kutulia juu ya uso wa maji Ndio hapo sasa tunaona katika mstari unaofuata Mungu akitamka Neno lake na hapo ndipo nchi ilipokamilika.
[3]Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.”
Ukiendelea na vifungu vinavyofuata, utaona dunia iliendelea kukamilishwa kwa NENO la Mungu.
Hivyo ukweli ni kwamba hatuwezi kuwa wakamilivu kama Neno la Bwana halijafunuliwa kwetu, haijalishi tutasema tunamjua Mungu kwa namna gani. Kama Neno la Mungu halijafunuliwa kwetu bado hatujakamilika.
Neno la Mungu likifunuliwa kwetu ndipo tutaweza kumuelewa Mungu ipasavyo, Ndipo tutaweza kusikia na kuelewa sauti yake anaposema nasi, Ndipo tutaweza kujua mapenzi yake ni yapi.
Lakini kama Neno lake halijafunuliwa kwetu ipasavyo, kamwe hatuwezi kumuelewa Mungu, wala hutuwezi kuyajua mapenzi yake, tutabakia tu kuwa watupu. Haijalishi tutakesha kanisani kila siku, Samweli alikuwa anakaa hekaluni kila siku lakini hakuwahi kumjua Mungu wala kufahamu sauti yake, alikuwa tu anamsikiaga kwa juu juu mpaka siku Neno la Mungu lilipofunuliwa kwake ndipo alipomjua Mungu na kuelewa sauti yake.
Leo hii unasukumwa sukumwa ufanye kazi ya Mungu, umtafute Mungu kwa bidii,..wewe mwenyewe hauna ratiba yako binafsi na Mungu, huna ratiba ya kuomba, huna ratiba ya kufunga, huna ratiba ya kusoma biblia, unasubiria mpaka ukumbushwe, ni kwanini? Ni kwasababu bado Neno la Mungu halijafunuliwa kwako, hivyo huwezi kujua wala kufahamu umuhimu wa maombi, huwezi kufahamu umuhimu wa kufunga na kuomba, huwezi kufahamu umuhimu wa kuwa na uhusiano wako binafsi na Mungu.
Ndio maana leo hii bado unatembea na vimini na masuruali barabarani na unasema umeokoka, na huoni kabisa kuwa upo uchi, ni kwasababu bado Neno la Mungu halijafunuliwa kwako.. hivyo bado upo kwenye dunia ile ya utupu, na hata ukiambiwa au we mwenyewe ukisoma kuwa hayo mambo uyafanyayo ni machukizo kwa Mungu..hauwelewi kwasababu bado Neno la Mungu halijafunuliwa kwako. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa Neno la Mungu kufunuliwa kwako. Vinginevyo utaendelea kuishi maisha ya dhambi na huku unasema umeokoka, utaendelea kuvaa mavazi ya aibu na mapambo ya kidunia bila kuona shida, na mwisho utaishia kwenda Jehanum.
Na Neno la Mungu ni YESU KRISTO mwenyewe. Yeye ndio ile sauti ya Mungu tangu pale mwanzo, iliyosema na iwe NURU. Ambayo baadaye ikaja kufanyika mwili, likakaa na sisi;
Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, NAO ULE UZIMA ULIKUWA NURU YA WATU. 5 NAYO NURU YANG’AA GIZANI, WALA GIZA HALIKUIWEZA”
Maana yake ni kuwa kama huna KRISTO YESU maishani mwako, Wewe ni bure. Ni sawa na ule mdoli wa nguo inayofanana na mwanadamu lakini sio mwanadamu.
Hivyo mpokee Yesu wa kweli ili uweze kumjua Mungu na kuelewa sauti yake. Leo dhamiria kuacha uchafu wote unaoufanya ili Yesu aingie ndani yako akupe ufahamu wa kumjua Mungu.
Ondoa hayo mawigi kichwani mwako, ondoa hiyo rangi bandia mdomoni, kwenye kucha n.k, ondoa hizo ringi kwenye masikio yako, tupa hizo takatataka zote, hizo vipodozi na hayo mavazi yote ya kikahaba yachome moto kabisa, ondoa kila kitu bandia kwenye mwili wako na ubaki kama ulivyoumbwa.
Futa kila aina ya uchafu kwenye simu yako, hizo picha chafu na hayo magemu ya kishetani yafute zote, miziki zote za kidunia na filamu zote zenye maudhui ya uasherati futa kabisa usibakize hata moja, sema mimi na udunia mwisho.
Baada ya hapo tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, hapo Roho wa Mungu atakaa juu yako na lile Neno la Mungu litafunuliwa kwako na ndipo utakapoanza kumjua Mungu katika upendo wake na katika wema wake na utaona matendo yake ya ajabu. Lakini leo kama usipotii mahubiri haya, ukayapuuzia tu kama wengine wanavyopuuzia.. hakika utakuja kujuta pale utakapojikuta upo kuzimu..na wakati huo utakuwa umeshachelewa. Hivyo saa ya wokovu ni sasa na sio kesho au baadaye.
Yesu anarudi!!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Na ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.