Mungu ndiye abadilishaye mashauri.

Biblia kwa kina No Comments

Mungu ndiye abadilishaye mashauri.

Ni kawaida kusikia ushauri wa mtu Fulani ni zuri au kusikia yule usimsikilize ushauri wake utakupoteza. Lakini watu wengi hatujui kuwa ushauri wa Bwana ni mzuri zaidi ya ushauri wa wanadamu, kwani mara nyingi adui shetani amekuwa akiwatumia watu kuharibu maisha ya watu wengi kupitia ushauri ambao tunaweza kuupokea na kuona kuwa ni njema..kumbe ni mtego wa ibilisi, kama sio Mungu anabatilisha yale mashauri tungepotea siku nyingi..kwani kila siku utawala wa giza wanatunga mashauri juu yetu.

Sasa leo tutatazama habari moja kwenye biblia ili tupate kuelewa vyema ni kwa namna gani BWANA anatupigania kinyume na adui shetani kwa kuyabatilisha mashauri yake yanayoletwa kwetu na mawakala wake. Na hapa tutasoma habari ya Mfalme Daudi jinsi Bwana alivyompigania na kumuokoa na njama za adui.

Kama we ni mwanafunzi wa biblia utakuwa unafahamu kuwa Daudi aliwahi kunusurika kupoteza ufalme na hata maisha yake kutoka kwa mwanae aliyeitwa Absalomu. Absalomu alipanga kumuondoa baba yake kwenye kiti cha ufalme na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, hali manusura Daudi aangamie kama sio Mungu alisimama upande wake. Sasa kuna mtu mmoja jina lake Ahithofeli, alimpelekea Absalomu ushauri wa njia za kumuondoa Mfalme kwa urahisi, lakini tunasoma biblia, alitokea mtu mwingine aliyeitwa Hushai naye akatoa ushauri ambao ushauri wake ulibatilisha lile shauri la Ahithofeli, Na biblia inarekodi huo ushauri ulikusudiwa na Mungu ili kuvunja shauri la Ahithofeli kwasababu Bwana alikuwa alikusudia kumletea Absalomu mabaya. Tunasoma..

2 Samweli 16:20 Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje.

[21]Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe.

[22]Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote.

[23]Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.

Tuendelee ..

2 Samweli 17:1 Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu;

[2]nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake;

[3]na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani.

[4]Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.

Lakini tusome ushauri kutoka kwa Mungu.

2 Samweli 17:5-14 Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.

[6]Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.

[7]Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.

[8]Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.

[9]Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.

[10]Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.

[11]Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.

[12]Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.

[13]Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.

[14]Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. KWA MAANA BWANA ALIKUWA AMEKUSUDIA KULIVUNJA SHAURI JEMA LA AHITHOFELI, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.

Umeona hapo, ndivyo Bwana anavyowapigania watu wake, yapo mashauri mengi yanapangwa juu yako.. Lakini ukiwa umesimama vizuri na Mungu..basi fahamu kuwa hayo mashauri hayatakuwa, kwani Bwana yupo karibu na wanaokupangia mabaya kuyabatilisha mashauri yao, na kuwapa ushauri ambao utawaangamiza wao wenyewe kama ilivyokuwa kwa Absalomu.. yeye alidhani ushauri wa Hushai ni jema kuliko ule wa Athofeli lakini kumbe hakujui kuwa Bwana alikusudia kumletea mabaya.

Lakini ukiwa mbaya machoni pa Mungu… fahamu kuwa adui atakupangia mabaya bila wewe kujua na hakuna atakayebatilisha hayo mabaya..yatakupata tu.

Huwenda ni kazini..watu wanaotumiwa na adui watatoa mashauri kwa huyo bosi wako ufukuzwe kazi, kama hauna mahusiano mazuri na Mungu wa kweli nani atakupigania hapo?

Au ni shuleni wametoa mashauri mabaya ili ufeli..nani atayabatilisha hayo mashauri kama hauna Yesu wa kweli? Unaona! Usifurahie tu kuishi maisha ya raha na huku hauna Yesu moyoni mwako.. fahamu kuwa yapo mashauri mengi yanakusudiwa kwa ajili yako ili usifikie malengo yako, kwa ufupi shetani halali kwa ajili yako. Lakini ukiwa na Yesu wa kweli.. yeye ndiye abatilishaye mashauri yao na kuwaletea adui zako mabaya.

Hivyo kama hujampokea Yesu sawa sawa, ni heri sasa umgeukie kwa kuamua kutubu dhambi zote na kuacha kabisa ili useme kama Daudi…”sitaogopa maana mtetesi wangu Yu hai”.

Bwana akubariki.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *