NAYE AKAJINYOSHA AKALALA CHINI YA MRETEMU.
Mretemu ni nini?
Mretemu ni aina ya mti ujulikanao sasa kama “MTARAKWA”. Zipo jamii nyingi za mitarakwa kulingana na mahali na mahali. Mtarakwa unaomea katika bara la Afrika ni tofauti kimwonekano na ule unaomea katika bara la Ulaya, (kutokana na hali ya hewa). Lakini yote inamatawi yanayofanana na tabia zinazofanana, kinachoitofautisha ni unene na urefu.
Mti wa Mtarakwa (au Mretemu) ni mti unaovumilia ukame sana, na kamwe matawi yake hayapotezi rangi yake ya ukijani, hata kama yatapitia ukame mkali.
Ndio maana utaona kipindi Eliya anamkimbia Yezebeli, tayari dunia nzima ilikuwa ni jangwa kwasababu mvua haikunyesha kwa miaka mitatu na nusu, na Eliya anauona mretemu na kukaa chini ya uvuli wake, sasa kikawaida mti uliokauka na ukame hauwezi kuwa na uvuli.
1Wafalme 19:4 “Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya Mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.
5 NAYE AKAJINYOSHA AKALALA CHINI YA MRETEMU; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule”
Sasa Mretemu ni nini katika Roho?
Eliya aliona mti wa Mretemu kuwa sehemu iliyo tulia, yenye mazingira mazuri ya kupumzika, hivyo akaenda akajinyosha chini yake akalala, tena akajiombea afe…akidhani kwamba ndio kafika. Lakini tunaona malaika wa Bwana alikuja kumwamsha na kumwambia ainuke ale kwani safari inaendelea tena bado ni ndefu.
1Wafalme 19:7 “Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.
[8]Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.”
Huwenda mretemu wako ni mtu fulani ambaye anakupa raha, anakupa uvuli, na wewe umeona ndiyo umefika, hivyo umeamua kulala moja kwa moja, nataka nikuambie leo inuka ule.. maana bado safari ni ndefu.
Chochote kile ambacho kinakupa pumziko mbali na Yesu, kinakupa usalama, kinakupa raha, kinakupa kivuli mbali na Mkuu wa Uzima Yesu Kristo iwe ni cheo, mali, mke/mume, rafiki, kiongozi wa dini awe ni mchungaji, Nabii, Mtume, au huduma fulani n.k, hicho kitu au huyo mtu ni mretemu ambayo umejinyosha na kulala chini yake, hivyo unapaswa kuamka na kula mkate wa uzima/ kumpokea Yesu ambaye ndio pumziko la kweli.
Watu wengi walipojikuta wamezaliwa katika dini zao au madhehebu yao…tena wazazi wao ni wachungaji, Maaskofu, Manabii, n.k wamejiona kuwa ndio wamefika… hivyo wameamua kulala kwa uvuli wa dini, na madhehebu yao…na kibaya zaidi wapo tayari hata kufia dini zao, na madhehebu yao
Ndugu, yamkini imani yako imejengwa juu ya mtu, huwenda ni Nabii au Mtume fulani ambaye wewe unamuona atakufikisha mbinguni na hivyo umeona kulala kwakwe ni salama, umeona ufe katika kivuli hicho. Yawezekana ulikimbia wachawi waliokuwa wanatafuta roho yako, ukajikuta kwa mtu mfulani au dhehebu fulani, na sasa umeona unafuu kidogo…ukadhani ndio umefika.
Lakini leo Bwana anakuambia… inuka hapo ulipolala, amka ule chakula maana safari bado inaendelea.
Inuka, toka kwenye hiyo kivuli cha waganga, toka kwenye kivuli cha dini na madhehebu ya uongo, dhehebu pekee la kweli ni Yesu Kristo, hayo mengine ni mapango ya ibilisi. Fahamu kuwa dini haikupeleki mbinguni, wala dhehebu lako haijalishi lina wafuasi wengi kiasi gani, unapokuwa mtu wa kidini na madhehebu hauwezi kuukulia wokovu wala kujua ukweli wote, utabaki tu kujua ukweli nusu. Na kibaya zaidi utakuwa unajiona upo sawa, utajiona umeokoka unaenda mbinguni kumbe hata jina lako halijulikani kule, ukiulizwa huo uhakika umeutolewa wapi? utasema ni kwasababu unaimba kwaya, unanena kwa lugha, unatoa sadaka, unaona miujiza na maono ndivyo utakuwa umedanganywa na huo mretemu ukadanganyika.
Hivyo leo amka toka usingizini maana muda uliobakia nao ni mfupi, huu sio wakati wa kulala..inuka ule chakula cha uzima (maneno ya Mungu ya kweli), bado safari inaendelea.. wokovu ni safari na unahitaji kula chakula chenye nguvu ili uweze kuendelea na safari ya wokovu.
Je! Umempokea Yesu ipasavyo au umempokea kwa namna ile ya kidini? Kama umempokea kwa namna hiyo ya kidhehebu fahamu kuwa bado upo chini ya mretemu umelala, hivyo amka umgeukie Yesu wa kweli. Yesu wa kweli ni yule aliyesema..
“...Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
[35]Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.’ (Marko 8:34-35).
Kujikana nafsi ni kukataa mapenzi yako na kufuata mapenzi ya Mungu, nafsi yako inakuambia tumia mkorogo kidogo unakataa, inakuambia vaa kimini, vaa suruali, vaa wigi, paka rangi kucha, tia wanja kidogo ili uonekane unaenda na wakati, unajikana.. unajiambia mimi si wa ulimwengu hivyo siwezi kufuatisha namna ya ulimwengu, unajiambia mwili wangu ni hekalu la Mungu hivyo siwezi kutia mapambo ya kidunia na kutembeza uchi, huko ndiko kujikana nafsi, na kuchukua msalaba maana yake unakubali kutengwa na marafiki, ndugu, unakubali kupoteza kazi, mume, unakubali kuonekana mshamba, na mateso yote unakubali..huko ndiko kubeba msalaba. Kama hujapitia moja ya vikwazo hivyo.. huwenda bado hujajikana nafsi kweli kweli. Hivyo leo amua kujikana nafsi na kuchukua msalaba wako na kumfuata Yesu.
Usiendele kulala chini ya huo mretemu/mtarakwa.
Tunaishi ukingoni mwa nyakati na moja hizi siku parapanda ya mwisho italia.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.