MFAHAMU MFALME YOSIA.

Biblia kwa kina No Comments

MFAHAMU MFALME YOSIA.

Shalom: karibu tujifunze biblia kwa kina.

Mfalme Yosia ni nani?

2 Wafalme 22:1 “Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.”

Mfalme Yosia ni Moja ya Wafalme 19 waliotawala Yuda, enzi zile za wafalme. Tukiachilia wale wafalme watatu ambao waliitawala Israeli kabla ya kugawanyika yaani (Sauli, Daudi, na Sulemani)..Ni mfalme mmoja tu ambaye kuzaliwa kwakwe kulitabiriwa kwa namna ya ajabu sana, na mfalme huyu sio mwingine zaidi ya mfalme Yosia.

Mfalme huyu kuzaliwa kwake kulitabiriwa miaka kama 300 nyuma, wakati taifa la Yuda peke ndio liliobakia baada ya Israeli kuchukuliwa utumwani na taifa la Ashuru, mfalme mmoja aliyejulikana kama mfalme Amoni, alimzaa mtoto akamwita jina lake Yosia, mtoto huyu katika umri wa miaka 15 alianza kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii sana, na alipofika umri wa miaka 19, alianza kusafisha, madhabahu zote za mabaali na maashera na mahali pa juu, ambazo baba zake walishindwa kufanya,.kwa muda wa miaka yote hiyo, alizifanya kuwa vumbi, yaani hakuacha sanamu yoyote katika Yuda, isitoshe hakuishia hapo alipanda mpaka kule Israeli ambapo sio hiyama yake, akasafisha kila madhabahu ya mabaali aliyokutana nayo njiani aliipondoponda na kuiichoma, na alikuwa haondoki mpaka ahakikishe imekuwa jivu, akawaua wapunga pepo wote, na makuhani wao, vile vile akafukua makaburi ya makuhani wao waliokuwa wanaifukizia uvumba zamani, moja baada ya lingine, na kutoa mifupa yao, na kuisagasaga.

Mpaka alipofikia kwenye kaburi moja lililokuwa kando-kando ya madhabahu zile, akaliona limekewa kumbukumbu juu yake, akaisoma, akasema hii ni kumbukumbu ya nani?..ndipo akaambiwa, hebu tusome ili tuelewe vizuri..

2 Wafalme 23:17 “Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.

18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.”

Ndipo hapo Israeli yote ikajua kumbe huyu ndiye aliyetabiriwa vile vile zamani kama tunavyosoma unabii wake katika..

1 Wafalme 13:1 “Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.

2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, JINA LAKE YOSIA; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.

3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.

4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.

5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana”.

Yosia alipoona hilo, akagundua kumbe Mungu alishauona wema wake tangu zamani, na kumwekea kumbukumbuku lake. Haleluya. Maandiko yanatuambia hakukuwa na mfalme aliyemwelekea Mungu kwa moyo wake wote kama ilivyokuwa kwa Yosia, Alimfanyia Mungu sherehe kubwa ambayo haikuwahi kufanywa Israeli tangu enzi za wafalme, isitoshe alikwenda kulikarabati hekalu la Mungu ambalo lilikuwa limechakazwa na wafalme waliotangulia.

2Wafalme 23:25 “Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.”

Sasa kwa undani wa habari za mfalme Yosia, unaweza soma kwa muda wako binafsi kitabu cha 2 Wafalme 22 au kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 34).

Lakini leo kuna tabia moja Bwana anataka tujifunze kwa huyu mfalme, Na tabia hiyo ni ile ya kurarua mavazi kama ishara ya toba na kuomboleza.

Kipindi ukarabati wa nyumba ya Bwana ulipokuwa ukiendelea kwa agizo la mfalme, Hilkia Kuhani mkuu ambaye alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa ukarabati alikiona kitabu cha torati katika nyumba ya Bwana, (ambacho ndani yake kiliandikwa maagizo ya Mungu na ghadhabu na laana pindi watakapoenda tofauti na yote yaliyoandikwa humo)

2 Wafalme 22: 8 Naye HILKIA, KUHANI MKUU, AKAWAAMBIA SHAFANI, MWANDISHI, NIMEKIONA KITABU CHA TORATI KATIKA NYUMBA YA BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. 

Na baada ya Shafani kukisoma kile kitabu, akaenda pia kukisoma mbele ya mfalme Yosia. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maagizo yote ya torati na ghadhabu na laana zilizoandikwa mle, MFALME ALIYARARUA MAVAZI YAKE, kwa sababu ghadhabu na laana zote zilizoandikwa mule ndizo walizozistahili kwa sababu baba zao hawakuyaangalia maneno ya kitabu kile na kufuata kama walivyoagizwa.

2 Mambo ya Nyakati 34:18 Shafani mwandishi akamweleza mfalme, akisema, HILKIA KUHANI AMENIPA KITABU. SHAFANI AKASOMA NDANI YAKE MBELE YA MFALME. 

19 IKAWA, MFALME ALIPOYASIKIA MANENO YA TORATI, ALIYARARUA MAVAZI YAKE. 

20 Mfalme akawaamuru Hilkia, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Abdoni, mwana wa Mika, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, kusema, 

21 Nendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa hao waliosalia wa Israeli na wa Yuda, katika habari za maneno ya kitabu kilichoonekana; maana ghadhabu ya Bwana ni nyingi iliyomwagika juu yetu, KWA SABABU BABA ZETU HAWAKULISHIKA NENO LA BWANA, KUTENDA SAWASAWA NA YOTE YALIYOANDIKWA KITABUNI HUMO.”

Hivyo ndivyo Yosia alivyofanya baada ya kusikia maneno ya torati na kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kurarua Mavazi yake baada ya kutambua makosa waliyomkosa Mungu na ghadhabu zitakazo wapata zilizo andikwa humo.

Nini tunajifunza tusomapo habari hizi? Je tunasoma tu kama stori fulani ya kusisimua?

Biblia inasema mambo hayo yote yaliyokwisha kuandikwa, yaliandikwa kwa jinsi ya mifano ili kutufundisha na kutuonya sisi watu wa sasa tuliofikiwa na miisho.

Warumi 15:4 Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. 

Hivyo basi, lipo funzo nyuma ya habari hiyo ambayo ni kuwa, hata sasa Torati ya Mungu, ambayo ni Injili ya Yesu Kristo iliyohubiriwa na mitume wake watakatifu bado ina maagizo yale yale, laana zile zile, na ghadhabu zile zile endapo wewe unayejiita mkristo ukienda tofauti na yale yaliyoagizwa katika Injili kwamba, utakumbana nazo tu kwani torati ndio Injili ya Kristo iliyohubiriwa na mitume wake, kwani mitume hawakuhubiri yaliyotofauti na hayo kama Paulo alivyosema katika..

Matendo ya Mitume 26:22 Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, WALA SISEMI NENO ILA YALE AMBAYO MANABII NA MUSA WALIYASEMA, kwamba yatakuwa;

Maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa, yale yote yaliyosemwa na Torati na manabii ndiyo hayo hayo yaliyohubiriwa na mitume (Injili ya Yesu Kristo), kwa ufunuo wa Roho wa Yesu Kristo Yule Yule aliyewaongoza manabii.

1 Petro 1:10 Katika habari ya wokovu huo MANABII walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, AMBAO WALITABIRI HABARI ZA NEEMA ITAKAYOWAFIKIA NINYI.

11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa NA ROHO WA KRISTO ALIYEKUWA NDANI YAO, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.

12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, AMBAYO SASA YAMEHUBIRIWA KWENU NA WALE WALIOWAHUBIRI NINYI INJILI KWA ROHO MTAKATIFU aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.

Hivyo, pindi usikiapo maneno ya Injili (Torati), kwamba Ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa mwili wako katika maji na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38), na kwamba, hakuna Mkristo yo yote yule kwenye maandiko aliyebatizwa vinginevyo, basi, unatakiwa kurarua moyo wako mbele za Mungu (na si Mavazi yako tena), maana baba zako hawakuzingatia yaliyoagizwa na injili kwa kukubatiza vingine kwani ghadhabu ya Mungu juu ya wote wasioamini na kubatizwa kama Yeye alivyoagiza ni kuu mno (Marko 16:16).

Unaposikia maneno ya kweli ya Injili, yaliyokinyume na dini yako au dhehebu lako, au yote uliyoyaamini na kufundishwa na baba zako, basi unapaswa kurarua moyo wako na kuanguka mbele za Mungu kwa kuomba rehema na msamaha kwa sababu dhehebu lako au baba zako hawakuzingatia na kuitii injili maana ghadhabu ya Mungu juu ya wote wasioitii Injili ya Yesu Kristo ni kuu mno (ni maangamizi ya milele na kutengwa na Utukufu wa nguvu zake).

2 Wathesalonike 1:8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, NA WAO WASIOITII INJILI YA BWANA WETU YESU; 

9 watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; 

Unaposikia au unaposomewa biblia kuwa wanawake wanaovaa vimini, makuptula, na masuruali na kujipamba kama Yezebeli sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti, kwamaana wanafanya machukizo mbele za Mungu (ufunuo 21:8), unapaswa kurarua mavazi na kutubia hayo machukizo yote kwa maana hasira ya Mungu ni kali juu ya watu wanaokwenda kinyume na Neno lake.

Na mambo yote ni vivyo hivyo. 

Je unaliishi Neno la Mungu ipasavyo? Ni mara ngapi umekuwa ukisikia maneno ya Mungu ya kweli kuwa waabuduo sanamu, wazinzi, wachukizao na waovu wote hawataurithi ufalme wa Mungu lakini unazipuuzia. Hebu leo ikiwa hujaokoka kikamilivu, rarua moyo wako na kisha omba rehema kwa Mungu na ujutie dhambi zako na umaanishe kumgeukia Mungu wa kweli YESU KRISTO, tafuta ubatizo sahihi usiendelee kupuuzia maneno ya Mungu.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *