NAMNA YA KUKATA KIU YA DHAMBI MAISHANI MWAKO.
Shalom: Nakusalimu kwa jina lipitalo majina yote jina la Bwana Yesu Kristo mkuu wa Uzima. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.
Na leo tutaenda kufahamu jinsi ya kukata kiu ya dhambi na kiu ya kila kitu maishani mwetu.
Yamkini unatamani kuacha dhambi na unashindwa, unatamani kuacha uzinzi, ulevi, punyeto/kijichua, uongo, usengenyaji, kamari, na dhambi zote unazozijua.
Huwenda umejaribu kila namna lakini imeshindikana, pengine umejaribu kuhudhuria kanisani, umeombewa vya kutosha, umefunga na kuomba, umejiwekea sheria kadha wa kadha lakini bado kiu ipo pale pale.
Leo nitakupa njia rahisi ya kukata kiu ya kila dhambi ndani yako.
Na njia yenyewe ni kwa KUNYWA MAJI!!
Siku zote dawa ya kiu ni kunywa maji, na wala sio kunywa chai, au uji au soda hapana, hivyo ni vimiminika lakini sio MAJI, haviwezi kukata kiu isipokuwa inaongeza tu.
Halikadhalika na hili tatizo la kiu ya dhambi, haikatiki isipokuwa ni kwa kunywa tu maji na wala sio kitu kingine.
Kumbuka maji tunayozungumzia hapa sio yale ya kisima!, sio maji ya chemchemi, wala ya bombani, wala kisimani, wala sio maji ya upako, yanayouzwa leo huku na huko.
Hapa tunazungumzia MAJI YA UZIMA ndiyo yanayoweza kukata kiu za kila namna iwe ni dhambi au kiu chochote kile.
Katika kitabu cha Yohana, Bwana Yesu alijaribu kugusia kidogo haya maji, kuwa maji ya uzima yaliyo hai…sio maji ya kisimani..
Yohana 4:5“ Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.
6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.
7 Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.
8 Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.
9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)
10 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, UNGALIMWOMBA YEYE, NAYE ANGALIKUPA MAJI YALIYO HAI.
11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo MAJI YALIYO HAI?
12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?
13 Yesu akajibu, akamwambia, KILA ANYWAYE MAJI HAYA ATAONA KIU TENA;
14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi HATAONA KIU MILELE; BALI YALE MAJI NITAKAYOMPA YATAKUWA NDANI YAKE CHEMCHEMI YA MAJI, YAKIBUBUJIKIA UZIMA WA MILELE.
15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka”.
Umeona hapo? jinsi Bwana alivyomfafanulia huyo mwanamke kuwa Yale maji anayoyadhania ya kisimani, sio maji ya uzima..Bali maji ya uzima ni kitu kingine kabisa lakini chenye tabia zinazofanana na hayo maji ya asili. Na ukipata hayo maji basi umekata kiu ya dhambi maishani mwako.
Sasa swali hayo maji ni nini?
Bwana Yesu, yeye mwenyewe alitupa majibu ya swali hili katika kile kitabu cha Yohana.
Yohana 7:37 “ Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, MTU AKIONA KIU, NA AJE KWANGU ANYWE.
38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, MITO YA MAJI YALIYO HAI ITATOKA NDANI YAKE.
39 Na NENO HILO ALILISEMA KATIKA HABARI YA ROHO, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; KWA MAANA ROHO ALIKUWA HAJAJA, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa”.
Umeona hapo?..Maji ya uzima ni ROHO MTAKATIFU.
Maana yake mtu anayepokea Roho Mtakatifu, anakuwa amekata kiu yote ya dhambi.
Kiu ya kunywa pombe na kuvuta sigara inakufa..kiu ya kufanya zinaa na uasherati inakufa, kiu ya kufanya mabaya inakufa, na mambo mengine yote mabaya yanakufa kabisa.
Kwasababu Roho Mtakatifu anatoa raha ambayo inazidi raha zote zinazopatikana katika mambo hayo ya ulimwengu yasiyompendeza Mungu.
Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kumpokea Roho Mtakatifu na kujazwa.
Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushinda dhambi kwa jitihada zake au kwa kujiwekea sheria.
Dhambi hatushindi kwa kuombewa, au kushinda kanisani au kwa kushauriwa, au kwa njia nyingine yoyote ile, Bali tunashinda kwa kunywa maji ya uzima (kujazwa Roho Mtakatifu)
Maana yake kama unaenda kanisani, au kwenye maombi na hujapokea Roho Mtakatifu na kujazwa, basi fahamu huko kote unajisumbua.
Sasa tunampokeaje Roho Mtakatifu?
Tunampokea Roho Mtakatifu kwa kumaanisha kabisa kutubu dhambi na kwenda kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo.
Matendo ya Mitume 2:37-39 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.
[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”
Watu wengi hawapokei Roho Mtakatifu kwasababu hawajadhamiria kutubu dhambi zao, kutubu dhambi sio kuomba tu msamaha, bali ni kuacha kabisa kwa vitendo hata kama itakugharimu hasara au maumivu kiasi gani.
Lakini pia hatuishii tu kupokea Roho Mtakatifu, bali tunapaswa tujazwe kila siku ndio kiu ya dhambi itakatika kabisa, kwani ukinywa maji kidogo haiwezi kukata kiu.
Tutajazwaje Roho Mtakatifu?
Ni kwa kudumu kwenye maombi kila siku na kujifunza biblia pamoja na kukusanyika na wenzako mara kwa mara.
Kumbuka hapa sizungumzii yale maombi ya kuomba mahitaji au kuombea kitu kingine, nazungumzia maombi ya kuomba ujazo wa Roho Mtakatifu na ni maombi ya masafa marefu sio yale ya dakika 5. (Kiwango cha chini ni saa limoja kila siku).
Marko 14:37Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? HUKUWEZA KUKESHA SAA MOJA?
Kukesha hapo ni kukesha katika kuomba, hivyo tunapaswa kuomba kwa bidii ili tujazwe Roho, na halikadhalika tunakaa mbali na mazingira yote ya dhambi na namna zote za ulimwengu. (Kwa ufupi baada ya kuokoka tunaishi maisha ya usafi) kadri tunavyozidi kuishi maisha ya utakatifu na kumtafuta Mungu kwa bidii ndivyo tunavyozidi kumpa Roho Mtakatifu nafasi ndani yetu na kiu ya dhambi tunasahau kabisa.
Je! Umeokoka? Umetubu dhambi na kubatizwa ubatizo sahihi, Je umejazwa Roho Mtakatifu?
Ishara ya kuwa haujapokea Roho Mtakatifu au umepokea lakini hajajaa katika kipimo chake ni kushindwa kushinda dhambi na kuishi maisha ya utakatifu.
Kumbuka kuishi maisha ya utakatifu sio sheria au maswala ya dini au kuwa ndani ya kanisa, hapana huko kote ni kupoteza muda! Utakatifu unawezakana kwa kujazwa Roho Mtakatifu basi. Na pasipo huo (utakatifu) hakuna atayemwona Mungu Soma Waebrania 12:14.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.