UTAKATIFU NDIO TIKETI YA KUMUONA MUNGU.

Biblia kwa kina No Comments

UTAKATIFU NDIO TIKETI YA KUMUONA MUNGU.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu.

Neno la Mungu linasema..

Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, AMBAO HAPANA MTU ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO;” (Waebrania 12:14).

Andiko hilo ni muunganiko wa maneno mawili, Neno la kwanza ni “TUTAFUTE KWA BIDII KUWA NA AMANI NA WATU WOTE”, na neno la pili, ni “TUTAFUTE KWA BIDII KUWA WATAKATIFU”.

Ni sawa na mtu aseme “katafute nyanya na vitunguu sokoni”…tukiichambua sentensi hiyo tunapata maneno mawili, 1) Tukatafute nyanya na pia 2) Tukatafute vitunguu.

Vivyo hivyo hapo biblia iliposema “Tutafute kwa bidii kuwa na amani na watu wote” na “huo utakatifu”..imemaanisha “tutafute amani kwa bidii” na pia “tuutafute utakatifu kwa bidii”.

Ikimaanisha kuwa amani na utakatifu, ni wa kutafutwa, Tena kwa bidii sanaa!!..

Na ni kwanini tumeambiwa tuutafute kwa bidii???…Ni kwasababu hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao. Maana yake utakatifu ni tiketi ya kumuona Bwana, pasipo huo hakuna atakayemwona. Haijalishi amefanya kazi ya Mungu kiasi gani au amedumu kanisani kwa muda gani.

Kumbuka mambo hayo “amani na watu wote, na utakatifu” tunatafuta kwa bidii. Maana yake tunatia nia ya kweli ya kuhitaji, bila hivyo hayaji tu kiwepesi wepesi.

Hayahitaji ulele mama wala uvivu!

Maana yake ukiwa mvivu wa kuomba na kufunga, kusoma biblia, kukesha, utakatifu sahau, wala hautoweza kuishi na watu wote kwa amani. Uvumilivu utakushinda tu.

Kwahiyo ili uweze kuishi maisha ya utakatifu na kuwa na amani na watu wote, huna budi kutafuta kwa bidii.

Na hatua ya kwanza ya kutafuta utakatifu na amani kwa watu wote ni kuzaliwa mara ya pili (KUOKOKA).

Kumbuka maana ya kuokoa sio kuombewa sala ya toba na kwenda kanisani. Hapana hiyo ni hatua ya pili baada ya mtu kuamua kuokoka.

Kuokoka ni kutambua kazi ya msalaba na kuamua kujutia dhambi na hivyo kudhamiria kubadilika na kumfuata Yesu pasipo kuwa mguu ndani na nje. Maana yake unamfuata huku ukiwa tayari kutii Neno lake lote, unakubali kuacha mambo yote mabaya kama ulevi,uzinzi, uvaaji mbaya mfano suruali kwa mwanamke, vimini, na nguo zote za kikahaba, mapambo, picha chafu, kamari, magemu, miziki, movies, na mambo yote ya kidunia.

Baada ya hapo unaenda kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, na Roho wa Mungu anaingia ndani yako. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kutafuta utakatifu.

Hatua ya pili ni kuwa muombaji kila mara.

Unapoakuwa muombaji mara kwa mara unaanza kuruhusu Roho Mtakatifu azidi kujenga makao ndani yako na kiwango chako cha utakatifu kinazidi kuimarika. Hivyo maombi ni muhimu sana, tena yale ya masafa marefu walau lisaa limoja kila siku ni bora sana. (Kumbuka ni maombi ya kujijenga kiroho ndio yanafaa sana zaidi ya yale ya mahitaji ya mwilini).

Hivyo baada ya kuzaliwa mara ya pili, jiwekee desturi ya kuomba kila siku, Muombe Mungu akujaze Roho Mtakatifu na kadri unavyoomba kwa bidii ndivyo unavyozidi kujazwa, na hatimaye Roho Mtakatifu afafurika ndani yako, na ukishafikia hapo..hautaona tena ugumu wa kuishi utakatifu, itakuwa ni jambo linalotoka ndani yako… kumbuka ni kila siku tunamwomba Baba atujaze Roho Mtakatifu kwa kuwa ni ahadi kuwa tukiomba atatujaza.

Luka 11:9 Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

[10]Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

[11]Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

[12]Au akimwomba yai, atampa nge?

[13]Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?

Hatua ya pili ni kufunga.

Bwana alisema mambo mengine hayatoki isipokuwa kwa kuomba na kufunga. (Mathayo 17:21)

Hivyo ili uweze kuishi utakatifu huna budi kuwa na ratiba ya kufunga mara kwa mara. Kumbuka ni kufunga na kuomba..ukifunga bila kuomba utakuwa unajitesa tu.

Tunapokuwa waombaji, katika ulimwengu wa roho shetani na mapepo yake yananakaa mbali nasi..Hivyo na viwango vyetu vya utakatifu vinapanda.

Hatua ya tatu ni kusoma na kujifunza Biblia.

Baada ya kuzaliwa mara ya pili ni lazima uanze kula chakula cha rohoni ambayo ni Neno la Mungu ili ukulie wokovu. Hivyo hakikisha unasoma na kujifunza biblia kila siku.

Tunapokuwa watu wa kujifunza Neno la Mungu, tunakuwa tunatakasika kwasababu Neno la Mungu lina maonyo ndani yake, na linatufunza na kutukumbusha kudumu katika Imani na utakatifu. Dalili ya kwanza ya mtu anayerudi nyuma kiimani, ni kupungukiwa na nguvu ya kujifunza Neno. Hivyo ili na sisi viwango vyetu vya utakatifu vipande hatuna budi tuwe wasomaji wa Neno la Mungu (yaani biblia).

Hatua ya nne na ya mwisho ni KWA KUKAA MBALI NA VICHOCHEO VYOTE VYA DHAMBI.

Dhambi inayo vichocheo, kama vile hasira ilivyo na vichocheo, kwa mfano vichocheo vya dhambi ya uasherati ni utazamaji wa pornography, mazungumzo mabaya na ya mizaha, makundi mabaya ya watu, uvaaji mbaya, filamu za kidunia ambazo asilimia kubwa maudhui zake ni kuchochea tamaa ya zinaa, vile vile magroup na kurasa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kama vile  facebook, Tikitok, whatsapp, instagram na mengineyo.

Mtu anayekesha muda wote kwenye facebook au kwenye mitandao mingine ya kijamii, mtu huyo kamwe asitegemee atakuwa salama..

Biblia inasema “Tutafute kwa bidii!!”…Sio kwa ulegevu..Maana yake “ukamilifu” hatuwezi kuupata tukiwa walegevu. Hivyo huna budi kukaa mbali na vyanzo vyote vya dhambi ili Roho Mtakatifu ajae ndani yako wakati wote.

Bwana atusaidie.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *