
WOKOVU WA KWELI NI UPI?
Habari ya uzima wako mtu wa Mungu, Ni siku nyingine tena leo nakukaribisha tushiriki pamoja kujifunza Neno la Mungu, maji yaliyosafi yasafishayo roho zetu kila siku.
Je unaposema umeokoka, ni nini kinakupa uhakika huo?
Wengi wetu tunafundishwa au tunafahamu kuwa ukitaka kuokoka jambo la kwanza ni kuamini Yesu alifufuliwa katika wafu,halafu unazungumza kwa kinywa chako(Kukiri) kuwa yeye ni Bwana, basi hiyo inatosha kukufanya wewe kuwa mtoto wa Mungu na kuurithi ufalme wa mbinguni.
Na ndio maana imekuwa ni rahisi hata leo hii kusikia mlevi anakuambia nimeokoka, hata mtukanaji anakuambia nimeokoka, mwabudu sanamu anakwambia nimeokoka, mzinzi anakuambia nimeokoka, ni kwasababu gani?, ni kwasababu alishamkiri Yesu na kumwamini zamani.
Ni kweli katika Warumi 10:9 biblia inasema;
“Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka”.
Lakini je! hivyo ndivyo biblia inavyofundisha juu ya wokovu?.. Tukitazama hayo hayo mandiko yanatuambia hata mashetani nayo yanaamini na kutetemeka mbele za Yesu, na yaanamini kwamba alikufa akafufuka,(Yakobo 2:19) na vilevile yanakiri, kuwa yeye ni mwana wa Mungu..(Luka 4:41).
Sasa kukiri kunakozungumziwa katika biblia, sio sawa na inavyotafsiriwa sasa. Zamani, kukiri kulimaanisha kutangaza vita na ulimwengu, Pamoja na kuhatarisha Maisha yako pia . Kwani ukristo ulijulikana kama ni dini asi, dhidi ya Imani za kipagani.
Soma,
Yohana 9:22 “.. kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi”.
Unaona zamani zile ilikuwa kabla hujafikiria kumkiri Yesu kwa namna yoyote ile, ilikuwa unapiga kwanza gharama ya mambo yatakayofuata baada ya hapo, Maana ilikuwa ukifikiria kuonyesha dalili za kumkiri tu moja kwa moja ulikuwa unatengwa na Sinagogi, kumbuka wayahudi walikuwa ni watu wa kidini, hivyo mtu ukitengwa na sinagogi ilimaanisha umetengwa na jamii nzima ikiwemo ndugu zako, na hivyo unajulikana kama kafiri, kama watu wa mataifa wasio na Mungu, hata siku ukifa hauzikwi pamoja na ndugu zako, hakuna sikukuu yoyote utakayoruhusiwa kushiriki, vilevile misaada ya kijamii haitakuhusu, unakuwa ni mtu wa kukataliwa siku zote hata katika mashauri yoyote hushirikishwi, unakuwa ni mtu wa kuudhiwa na kuvunjwa moyo kila siku.
Na ndio maana utaona wengi sana wakati Bwana Yesu yupo duniani walimwamini ikiwemo mafarisayo kama vile Nekodemo na wakuu wengine, lakini ki chini chini wakiogopa kumkiri hadharani kwasababu ya adhabu hiyo mbaya sana.
Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.”
Vile vile na baada ya Bwana Yesu kufa na kufufa,na kuondoka hali hiyo ndio ikazidi kuwa mbaya zaidi, ilikuwa sio tu kutengwa, lakini sasa mtu yoyote alikuwa akionekana anamkiri hadharani, ilikuwa ni mambo matatu yapo mbele yako, la kwanza lilikuwa ni kifo, na kama ukinusurika sana, basi ni kutupwa gerezani au kupigwa.. Hivyo mtu yoyote aliyeonekana anachukua uamuzi wa kumfuata Kristo au kumkiri alionekana ni mtu aliyechukua maamuzi ya kishujaa sana. Na ndio maana tunaona jinsi kanisa la kwanza lilivyokuwa linapitia dhiki nyingi sana, walikuwa kama wakimbizi, na wapitaji tu hiyo yote ni kwasababu ya Imani yao kwa Kristo.
Na ndio maana sasa hapa mtume Paulo aliliambia kanisa:
Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”.
Lakini leo hii hili neno kumkiri Bwana Yesu linapewa tafsiri tofauti, Tunasema tumemkiri Yesu lakini hatupo tayari kujitwika misalaba yetu na kumfuata. Kiuhalisia hapo hatujamkiri Kristo maishani mwetu, yaani kwa lugha rahisi kumkiri Yesu kwa sasa sio kuzungumza tu mdomoni, kwasababu sasahivi hakuna dhiki yoyote utakayopitia kwa kusema YESU ni Bwana.
Hivyo neno kukiri tu kwa kinywa, sio kipimo tosha kwamba wewe umemfuata Yesu, kwasababu mtu yeyote anaweza kufanya hivyo hata mpagani, kwasababu hakuna hatari yoyote inaweza kumtokea kama akifanya hivyo. Kwasababu anakuwa ni kama tu kaongea.
Na ndio maana leo hii kuna idadi kubwa sana ya watu wanajiita wakristo wanasema wameokoka. Ukiwauliza wameokokaje watakuambia, kwasababu walimkiri Yesu kwa vinywa vyao, hilo tu.Na huku ukiangalia Maisha yao, hayana tofauti na watu wa kidunia.
Ndugu usidanganyike, wokovu wetu ili ufanane na ule wa watu wa zamani, hatuna budi tumkiri Yesu KWA MATENDO YETU. Tunaukataa ulimwengu na mambo yake yote, kivitendo.
Maana yake kumkiri Yesu hasaa katika nyakati hizi ni pale unapochukua uamuzi kama vile Kanisa la kwanza lilivyofanya kweli kwa vitendo, utamkiri kwa kuacha kuvaa vimini, na suruali, kwa kuacha kutembea na kampani zako mbaya za zamani, kuacha kwenda disco, na club, kukaa mbali na uasherati, kumtumikia Mungu, kuonyesha kuwa unamfauta KRISTO, huko ndiko kukiri kunakomaanishwa.
Lakini ikiwa mtu atasema nimemkiri, na bado unaipenda dunia kuliko Kristo, hapo haijalishi uliongozwa sala ya toba mara ngapi, bado utakuwa mbali tu na wokovu.
Hivyo ndugu ikiwa hapo nyuma haukumaanisha, ulikiri tu, basi kama desturi na mazoeza basi leo hii maanisha kweli kweli mbele zake.
Kumbuka wokovu sio wa kuchaguliwa na mtu, au kuletewa na mtu, ni jukumu la wewe binafsi kuchagua.. Mungu hawezi kulazimisha wokovu uingie ndani yako kama wewe hutaki. Hivyo ni jukumu lako aidha kuchagua kuishi katika dhambi siku zote ambapo mshahara wake ni mauti ya mwilini na rohoni, au umkriri Yesu Kristo kwa kumaanisha kabisa kumgeukia.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.