UMEFANYA HIVYO KWA KUTOKUJUA

Biblia kwa kina No Comments

UMEFANYA HIVYO KWA KUTOKUJUA

Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe daima. Karibu katika mafundisho ya biblia, Neno la Mungu wetu lililo Taa na Mwanga wa Njia zetu (Zab.119:105).

Katika biblia tunasoma habari ya mtu mmoja aliyeitwa Abimeleki, huyu alikuwa ni mfalme wa nchi iliyojulikana kwa jina la Gerari ambayo ilikuwa inapatikana kule mashariki ya kati enzi za biblia.

Sasa huyu mfalme Abimeleki, tunasoma bila kujua alimchukua Sara ambaye alikuwa ni mke wa Ibrahimu, alifanya hivyo akijua kuwa Sara ni ndugu na Ibrahimu na sio mkewe, lakini kwasababu Abimeleki alikuwa anamcha Mungu wa mbingu na nchi, na alifanya hivyo kwa kutokujua (alichukua mke wa mtu), Mungu alimtokea katika ndoto na kumwambia maneno haya, tusome…

Mwanzo 20:1 “Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari.

[2]Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara.

[3]Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.

[4]Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki?

[5]Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi.

[6] MUNGU AKAMWAMBIA KATIKA NDOTO, NAMI NIMEJUA YA KWAMBA KWA UKAMILIFU WA MOYO WAKO UMEFANYA HIVI, NDIPO NAMI NIKAKUZUIA USINITENDEE DHAMBI, kwa hiyo sikukuacha umguse.

[7] BASI SASA UMRUDISHE MWANAMKE KWA MTU HUYO, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. BALI USIPOMRUDISHA, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao”.

Kumbe! unaweza ukafanya kosa kwa Mungu, na Mungu akakuacha uishi kwasababu tayari anajua moyo wako, kwamba umefanya hayo kwa ukamilifu wa moyo wako yaani kwa kutokujua.

Lakini, anapokujulisha makosa yako, halafu ukaendelea na makosa hayo, Mungu mwenyewe anakuadhibu, Ndivyo biblia inavyosema katika..

Waebrania 10:26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;

[27]bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao”.

Abimeleki alipojulishwa kosa lake alilolifanya kwa kutokujua, baada ya hapo aliambiwa arudishe huyo mwanamke kwa mumewe, na asiporudisha atakufa yeye na familia yake yote na hata taifa lake.

Na wewe leo pia, Mungu anakuambia huyo mume/mke uliye naye ambaye ulimchukua baada ya kuachana na yule aliyekuwa naye, mrudishe maana ni mke/mume wa mtu!. Na usimporudisha utapata matatizo wewe na nyumba yako.

Halikadhalika mke/mume uliye naye na hamjafunga ndoa halali kanisani ni heri mvunje leo hiyo ndoa hata kama mlizaa watoto kumi, kwasababu mnachokifanya ni uasherati, leo leo muachane au mkafunge ndoa kanisani kabla hamjapata madhara makubwa, maana Mungu aliwaacha tu kwa kuwa mlifanya hivyo kwa kutokujua. Lakini sasa anakujulisha haya kwa upendo wake ili usiangamie hukumuni.

Dada/mama unayejipamba kwa mapambo ya kila namna, hereni, vipini, lipustiks, wanja, wigi, mekaups, kucha bandia, na kuvalia mavazi ya nusu uchi/vimini, suruali, makaptula, nguo za kubana, kifua wazi, mabega wazi, mgongo wazi, tumbo wazi, n.k hiyo yote ni mionekano ya watu wa kidunia au makahaba. Lakini huwenda ulikuwa unafanya hivyo kwa ukamilifu wa moyo wako/Kwa kutokujua lakini sasa Mungu anakujulisha ili utubu na kuacha hizo mitindo ya kigeni ili usije ukatupwa jehanumu.

Matendo 3:17 “Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda.

[19]Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;

Kijana ulikuwa unabeti, unacheza magemu, unasikiliza miziki za kidunia, unaangalia filamu za kidunia, mipira ya kidunia, unanyoa kidunia, unavaa kidunia, unaishi na girlfriend, unatazama pornography, unafanya masturbation/unajichua, na bado unaenda kanisani tena ni mtumishi, huwenda ulikuwa unafanya hayo kwa kutokujua na Mungu alikustiri mpaka sasa, lakini leo anakujulisha haya ili utubu na kuacha hayo mambo kabla hujaenda huko Ahera.

Matendo 17:30 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu”.

Dada/mama ulikuwa hujui kuwa mwanamke anapaswa kufunika kichwa akiwa ibadani (1Wakorintho11), lakini leo umejua hivyo nenda kabadilike maana Mungu alikuwa anakuangalia tu kwakuwa hukujua.

Ulibatizwa kwa maji madogo, lakini leo fahamu kuwa ubatizo sahihi ni wa maji mengi na Kwa jina la Yesu Kristo (Yohana 3:23 & Matendo2:38), hivyo nenda katafute huo ili ukamilishe wokovu wako vinginevyo hutozaliwa mara ya pili na hivyo huwezi kuingia katika ufalme wa Mungu (Yohana 3:3).

Maran atha!.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *