ONJENI, MWONE KUWA BWANA YU MWEMA

Uncategorized No Comments

ONJENI, MWONE KUWA BWANA YU MWEMA

Zaburi 34:8 Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.

Ulishatembelea soko la vyakula, na kukutana na wafanya-biashara wengi, halafu kila mmoja anakuvutia upande wake ununue bidhaa yake. Kwakawaida si rahisi kuchukua maamuzi, kwa hofu ya kuuziwa kitu kusicho bora.

Wafanyabiashara wengi hulijua hilo, hivyo wanachokifanya ni kukuonjesha kwanza…uone kama kweli bidhaa yao ni bora au la, na ndio hapo kama ni muuza karanga au ubuyu atakupimia kidogo mkononi. Ili uonje kwanza, ndipo uridhishwe uwe na ujasiri wa kile utakachokinunua.

Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu..kutokana na hofu ya kupotezwa katika imani zisizo sahihi zilizopo ulimwenguni leo hii, Yesu anakuja kukwambia Njoo kwangu, nitakupa uzima wa milele, na kukusaidia shida zako.

Lakini kama una mashaka na hilo, basi anakuambia onja kwanza uone kama kweli yeye yu hai anaokoa watu au la?

Kumbuka Yesu sio dini, Yesu sio nabii fulani ambaye alishakufa zamani, hajui ni kitu gani kinaendelea duniani. Yesu yupo hai, na kila siku anayagusa maisha ya watu, anazitazama shida zao, anawarehemu, kuonyesha kuwa yeye sio hadithi za vitabuni tu.

Hivyo ikiwa kweli unahitaji kupata wokovu wa kweli, kupata imani ya kweli embu onja, kumfuata Yesu…uone kama kweli utaupata au la?

Sasa utauliza mtu unaonjaje?

Ni kwa kumaanisha kwanza ndani ya moyo wako, kwamba kweli unatamani kuijua njia ya kweli ya kumfikia Mungu, sio kwa kufikiri juu juu tu, au kujaribu jaribu na huku moyoni mwako hakuna shauku yoyote ya kutaka msaada kutoka kwa Mungu wa kweli. Hapo huwezi kupokea chochote.

Sasa ukishakuwa tayari kufanya hivyo, hatua inayofuata mwombe Yesu akufanyie hitaji lako, au mwombe lolote..na kwa kupitia hilo, ili uwe na ujasiri wa kumwamini na kumtumikia. Hivyo akishakupatia basi, kuanzia huo wakati yasalimishe maisha yako moja kwa moja kwake, kwasababu hakuna msaada unaoweza kuupata kwa mwingine zaidi ya kwa huyo.

Yeye mwenyewe anasema..

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

[29]Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

[30]kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Mimi nilionja na nikaona, na watu wengi vivyo hivyo. Na wewe pia ingia kwake uone, haijalishi dini yako au dhehebu lako.

Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.

Je! Una uchungu moyoni, umekulemea? Una dhambi unashindwa kuiacha? Unasumbuliwa na nguvu za giza? Una ugonjwa usiotibika? Maisha yako ni ya masumbuko?

Jibu lipo kwa Yesu, alikuja duniani kwa ajili ya kutuokoa sisi roho zetu, na pia mateso yetu.

Anasema..

Luka 4:18 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,

[19]Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.

Ni nini unangoja? Anza sasa kuzungumza naye, kwasababu yupo karibu na wewe hapo ulipo kukusaidia.

Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *