MIMI NAMI NITACHEKA SIKU YA MSIBA WENU.

Siku za Mwisho No Comments

MIMI NAMI NITACHEKA SIKU YA MSIBA WENU.

Jina la Bwana Yesu libarikiwe daima, karibu tuendelee kuyatafakari maneno ya Mungu.

Mambo mengi yanayoendelea hapa duniani yamebeba ufunuo wa mambo yalivyo rohoni.

Kwa mfano hukuku wanazotoa wanadamu kwa wanadamu wenzao katika mahakama yao, ni ufunuo wa hukumu ambayo Mungu ameandaa kuwahukumu wanadamu, ambao kila mtu atahukumiwa kulingana na matendo yake (ufunuo 20:11-15)

Lakini pia msiba ambao unawapata wanadamu sasa hivi ni ufunuo wa msiba mkubwa ambao utakuja kuipata dunia nzima.

BWANA wa Majeshi, Mtakatifu wa Israeli anasema..

Mithali 1:24 “Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;

[25]Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu;

[26]Mimi nami nitacheka SIKU YA MSIBA WENUNitadhihaki hofu yenu ifikapo;

[27]Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.

[28]Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.

[29]Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha BWANA.

[30]Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.

[31]Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

Unaona hapo, kuna msiba ambao utawapata wanadamu, lakini Mungu anasema atacheka siku hiyo.

Umewahi kupatwa na msiba halafu mtu badala akufariji kinyume chake anakucheka. Maana yake anakuongezea maumivu, ndivyo itakavyokuwa siku ile ya msiba wa huu ulimwengu.

Kwanini Mungu atacheka siku hiyo, ni kwasababu wakati alikuwa analia na kuhuzunika kwa ajili ya maovu yetu, wakati anatulilia tumgeukie na kuacha njia zetu mbaya, badala tutubu na kugeuka, kinyume chake tunadhihaki na kuwacheka watumishi wake.

2Mambo ya Nyakati 36:15 Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

[16]lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.

Kwahiyo, siku hiyo Bwana atacheka na kudhihaki, watu watakapokuwa katika kilio kikuuu, ni wakati wa kupatilizwa maovu.

Wanadamu watalia, na kuomboleza wakimlilia Mungu asiwasikie.

Ufunuo 16:2,7-9,17 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.

[7]Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.

[8]Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.

[9]Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu.

[17]Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.

[18]Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.

[20]Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.

[21]Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.

Ufunuo 9:6 Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.

Luka 21:22 “Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.”.

Siku hizo Bwana anasema hakutakuwa na huruma, watu watalia na kujutia na kutubu lakini hakuna atakayesikia, mpaka ghadhabu ya Mungu ya mwisho itakapomalizwa kumwagwa duniani. Na Bwana anasema ni HIVI KARIBUNI huo msiba mkuu utatokea.

Ezekieli 7: 5 “Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, JAMBO BAYA LA NAMNA YA PEKE YAKE; ANGALIA, LINAKUJA.

6 Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja.

7 Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.

8 BASI HIVI KARIBU NITAMWAGA GHADHABU YANGU JUU YAKO, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; NAMI NITAKUPATILIZA MACHUKIZO YAKO YOTE.

9 Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga”.

Ndugu Hii SIKU YA BWANA usitamani uwepo. Kumbuka haitakuwa jehanamu ya moto, bali itakuwa ni adhabu ya hapa hapa duniani.

maandiko yanasema:

Amosi 5:18 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani SIKU YA BWANA; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru. 

19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. 

20 Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.“

Pia tukisoma…

Isaya 13:6″ Pigeni kelele za hofu; maana SIKU YA BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.

7 Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. 

8 Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.

9 Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.

10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. 

11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;

12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.”

Maandiko yanaposema SIKU YA BWANA hayamanishi ni siku kama siku moja, bali inamaanisha ni kipindi fulani cha WAKATI ambacho Bwana amekitenga kwa kusudi fulani. Kama maandiko yanavyotueleza ni kipindi ambacho kimetengwa cha GHADHABU NA HASIRA ya Mungu kulipiza kisasi kwa wanadamu wote wasiomcha Mungu.

Kipindi Hichi cha SIKU YA BWANA kitadumu kwa muda wa siku 75, Hizi zimepatikana kutoka katika kitabu cha Nabii Danieli 12:12, ambapo tunaona kipindi cha ile dhiki kuu kitadumu kwa muda wa siku 1260, na hapo zimeongezeka siku nyingine kutoka siku 1260 mpaka kufikia siku 1335, kwahiyo ukichukua hizo siku 1335-1260=75.

Kwahiyo hizi siku 75 zilizoongezwa ni mahususi kwa ajili ya BWANA kujilipizia kisasi kwa wanadamu wote waliosalia juu ya uso wa nchi. (Hiyo ndio siku ya MSIBA wenyewe).

Rafiki haya mambo ni kweli yatatokea, ndivyo yatakavyokuja kuupata ulimwengu na dalili zote zinaonyesha kuwa yatatokea katika kizazi chetu tunachoishi mimi na wewe, Bwana amekwisha kutuonya mbele, Nia yake ni sisi tuiepuke hiyo ghadhabu na ndio maana kuna mahali alisema alipokuwa katikati ya kitasa cha sita (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake). Kwahiyo ametuonya tukeshe na kuyatunza mavazi yetu, maana hii siku ya ghadhabu itakuja ghafla.

Ndugu kimbia injili ambazo zinakufanya usifikiri hatma ya maisha yako ya milele badala yake inakupeleka kutazama mambo ya ulimwengu huu. Hii ni roho ya shetani inawapumbaza wengi wafikiri mambo hayo yatakuja kutokea baada ya miaka 2000 mbele, usidanganyike ni uongo wa shetani, ndugu dalili zote zinaonyesha, unabii wote umetimia kwamba tunaishi katika kizazi cha hatari sana.

Chunguza maisha yako angali neema ipo, mambo hayatakuwa hivi siku zote, pale mlango wa neema utakapofungwa kutakuwa hakuna kurudi nyuma itakuwa ni vilio na maombolezo, kimbilia kalvari sasa tubu dhambi zako, uoshwe kwa damu ya Yesu, na Upokee Roho Mtakatifu kabla ya huo wakati kufika. Kumbuka adhabu ya hii SIKU YA BWANA, sio jehanamu ya moto, baada ya mapigo hayo ndipo ziwa la moto ziwa la moto litafuata.

Ikiwa unataka kumpa Bwana Yesu maisha yako na kugeuka leo tubu mwenyewe moyoni mwako au fuatiliza sala hii kwa imani:

Sema:

Bwana Yesu, Leo hii nasogea mbele zako nikiwa mwenye dhambi, natubu makosa yangu yote niliyokukosea, naomba unisamehe, nimeamua kugeuka leo, nisaidie Bwana Yesu, neema yako iwe juu yangu, nikuishie wewe, siku zote za maisha yangu, asante Bwana Yesu kwa kunisikia na kunisamehe. AMEN! “.

Baada ya kutubu unahitaji kubatizwa, Hivyo basi tafuta kanisa linalobatiza ubatizo sahihi nao ni kwa kuzamishwa kwenye maji mengi na ni kwa jina la YESU KRISTO, Kwa kufanya hivyo Bwana atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu na utakuwa umekamilisha wokovu wako.

MUNGU AKUBARIKI.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *