
WAMENOA NDIMI ZAO KAMA NYOKA.
Jina la Bwana YESU mkuu wa uzima libarikiwe milele. Karibu tujifunze Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa njia zetu (Zab.119:105)
Moja ya silaha anayoitumia adui kumshambulia Mtu ni “ULIMI WA UOVU”.. Ukiona Maneno ya uongo kuhusu wewe, au ya vitisho au ya uchonganishi yanatembea huku na huko basi fahamu kuwa hiyo ni silaha ya adui anataka akuangushe kwenye imani.
Zaburi 143:1 “Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.
2 Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.
3 WAMENOA NDIMI ZAO KAMA NYOKA, Sumu ya fira i chini ya midomo yao”
Nyoka ni kiumbe anayeuma (au anayeng’ata kwa kutumia mdomo)..Silaha yake kubwa ni mdomo na mate yake, hana silaha nyingine kiasi kwamba ukikibana kile kichwa hakuna atakachoweza kufanya ili kukudhuru. Nyoka ni mfano wa Watu wanaotumika na shetani, kwa kujua au kwa kutokujua kukudhuru wewe kupitia maneno wanayoyazungumza…Yaani kwaufupi silaha yao ni maneno..
Yeremia 18:18 “Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na TUMPIGE KWA NDIMI ZETU, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.
Sasa kwanini Adui, aiweke hii silaha ya ulimi kama chaguo lake la kumshambulia mwamini?… Ni kwasababu anajua ulimi wa mtu unaweza kuwasha moto mkubwa, na kama mtu hatakuwa na Imani ya kutosha basi anaweza kuanguka kabisa.
Yakobo 3:6 “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum”
Hivyo shetani anaweza kukuwashia tu moto kupitia ulimi wa mtu au ndimi za watu, na moto huo ukawa mkubwa sana, kiasi kwamba kama huna imani na ujasiri wa kutosha, unaweza kurudi nyuma kabisa.
Shedraka, Meshaki na Abednego walijikuta wapo katika tanuru la Moto, kwasababu tu ya baadhi ya watu waliotumia ndimi zao kupeleka mashitaka kwa mfalme kuwa hawataki kuisujudia ile sanamu.(Danieli 3:8-12).
Danieli naye alijikuta katika tundu la simba kwasababu tu ya vinywa vya watu, na Yeremia naye alijikuta katika lile shimo refu lenye giza lililojaa matope kwasababu ya maneno ya watu(Yeremia 38:6).
Lakini wote hao walishinda, kwani moto ule uliokusudiwa juu yao uliwala maadui zao, na mashimo yale na matundu yale yaliyokusudiwa juu yao yaliwaharibu maadui zao, lakini kama wangetetemeka na kuogopa na kurudi nyuma bila shaka wangepotea kwa kuharibiwa na ibilisi!.
Na sisi hatuna budi kusimama Imara bila hofu, kwa ujasiri mwingi pale ambapo adui anatumia NDIMI za watu kama silaha yake…
Sasa tutasimamaje imara ili tuwashinde watu wa namna hii? Jibu tunalisoma katika..
Luka 10:19 “Tazama, NIMEWAPA AMRI YA KUKANYAGA NYOKA NA NGE, NA NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”

Unaona hapo, tunawashinda kwa amri hiyo, yaani kwa ”kuwakanyaga”… Unaelewa maana ya kukanyaga???…Kukanyaga maana yake ni KULIPOTEZEA JAMBO!!..Kulishusha hadhi, kulipunguza nguvu, kuliabisha, kulidhalilisha, kulidharau. Hiyo ndio maana ya kukanyaga, wala kukanyaga sio kuingia kwenye maombi ya mifungo ya masafa, au kwa kusema ninakukanyaga shetani, hapana hiyo sio maana yake.. Maana yake ni kuliweka chini yako jambo. Kama tu vile watu wanavyolikanyaga chini neno la Mungu, wanafanya hivyo kwa kulidharau…Kitendo cha kukidharau kitu tayari umekikanyaga chini.
Waebrania 10.28 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.
29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”
Umeona hapo?. Watu wote wanaoihesabia damu ya agano la Yesu kuwa ni kitu ovyo, na kumdharau (au kwa lugha ya sasa, ni kuipotezea), watu hao ndio wanahesabika kama wamemkanyaga Mwana wa Adamu.
Ni hivyo hivyo, mtu anayehesabia kazi za shetani kuwa ni kitu ovyo, hapo anakuwa amemkanyaga chini, ya miguu yake. Hiyi ndio silaha ya kuwashinda watu wanaotumiwa na shetani kukudhuru kwa njia hii ya ulimi.
Sasa hatuwakanyagi na sisi kwa kuwarudishia maneno.. Hapana, tukifanya hivyo na sisi tutakuwa ni nyoka kama hao. Lakini tunakanyaga vichwa kwa kuyapuuza maneno yale, na kuyazuia yasiingie moyoni mwetu.
Kwasababu ukiyaruhusu yaingie moyoni mwako, yatakuwa sumu kwako na yatakudhuru.. Hivyo unayapuuzia yale maneno na kuyapiga mateke, hiyo ni silaha kubwa sana..Ambayo kwa hiyo utaweza kuwakanyaga nyoka wote.. (Kumbuka nyoka hapo ni lugha ya rohoni, usimwite kamwe ndugu yako nyoka hata kama ni mbaya kiasi gani kwako).
Bwana akubariki.
Kama hujaokoka kumbuka hizi ni siku za mwisho na Yesu anakaribia kurudi, biblia inasema itatufaidia nini tukiupata ulimwengu mzima na kupata hasara za nafsi zetu?..Tafakari neno hilo kwa makini, hivyo kama utaamua leo kumpa Kristo Maisha yako, utakuwa umefanya jambo la busara sana, ambalo hutakaa ujutia katika maisha yako, hivyo kwa msaada Zaidi na maombezi wasiliana nasi kwa namba zilizopo chini ya makala hii.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.