JE UMEPOKEA UWEZO WA KUFANYIKA MTOTO WA MUNGU?

Biblia kwa kina No Comments

JE UMEPOKEA UWEZO WA KUFANYIKA MTOTO WA MUNGU?

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Biblia inasema katika..

Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

[13]waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”.

Anasema wote waliompokea aliwapa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu?

Tafsiri nyingine ni wote waliomwamini walipewa huo uwezo.

Ni nani huyo anatoa huo uwezo mkuu? Si mwingine zaidi ya mkuu wa uzima YESU KRISTO.

Wote waliompokea na wanaompokea hata sasa wanapewa huo uwezo bure. Na faida ya kufanyika mtoto wa Mungu ni kuurithi ufalme wa Mungu kwasababu kwa kawaida hakuna baba anayemridhisha mtoto asiye wake uridhi wake, haijalishi anampenda kiasi gani!

Hivyo ili tuweze kuurithi uzima wa milele na ufalme wa Mungu hatuna budi kufanyika kuwa watoto wake, kumbuka hapo kabla, tulikuwa tu kama viumbe vingine kama kuku.

Lakini kwa upendo wa Mungu alimtuma mwanaye mpendwa aje azaliwe kama sisi, aishi kama sisi na mwisho asulubiwe msalabani ili kupitia yeye tupokee huo uwezo wa kuwa wana wa Mungu.

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Sasa tunampokeaje huyu mwana wa Mungu ili tupewe huo uwezo wa kuwa watoto wa Mungu?

Jibu ni kwa kuzaliwa mara ya pili baada ya kuwa tumemwamini.

Yohana 1:12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, NDIO WALE WALIAMINIO JINA LAKE;

[13]waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.

JE KUZALIWA MARA YA PILI KUKOJE?

Kuzaliwa mara ya pili kunakuja kwanza baada ya mtu kutubu dhambi zake, [kumbuka maana ya kutubu ni KUGEUKA], sio kuongozwa sala ya toba, unageuka kwa kudhamiria na kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, kuyaacha ya kale na kuanza maisha mapya kwa Kristo, na baada ya kutubu, bila kukawia hatua inayofuata ni kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele, na kwa JINA LA YESU KRISTO, (kulingana na Matendo 2:38), upate ondoleo la dhambi zako, na hatua ya tatu na ya mwisho ni Roho wa Kristo kuingia ndani yako, sasa hapo ndipo ule uwezo unaingia ndani yako. Mtu yeyote akiruka hatua yoyote kati ya hizo, bado hajazaliwa mara ya pili..Kumbuka ndugu hii sio dini wala dhehebu ni maagizo ya Bwana Yesu mwenyewe ambayo yapo kwenye biblia.

Biblia inasema wazi kabisa, katika Yohana 3: 5 “Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.”

Sasa kumbuka kuzaliwa kwa maji kunakozungumziwa hapo ndio UBATIZO WA MAJI, na kuzaliwa kwa Roho ndio UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU. Hapo ndipo unakuwa umeshazaliwa mara ya pili. Lakini Wapo wengine wanataka kubatizwa lakini hawajadhamiria kuacha maisha yao ya kale ya dhambi, hao hata wakienda kubatizwa wanafanya kazi bure, hakuna chochote kitakachotokea katika maisha yao.. Kadhalika wapo wengine, wametubu lakini hawataki kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wanasema ubatizo wa maji hauna maana sana hawa nao pia hawataona mabadiliko yoyote katika maisha yao.. Maagizo yote aliyoyatoa Bwana Yesu hakuna hata moja lisilokuwa na maana, alisema aaminiye na kubatizwa atakoka, na sio aaminiye tu peke yake. Hapana bali vyote viwili vinakwenda pamoja.

Hivyo mtu akizingatia hizo hatua zote za yeye kuzaliwa mara ya pili utapokea UWEZO, wa kufanyika Mwana wa Mungu na mridhi wa ahadi za Mungu.

Je! Umefanyika mtoto wa Mungu? Umezaliwa mara ya pili?

Kama bado unasubiri nini mpaka sasa? Hujui kuwa hii neema haitadumu milele! Muda wowote unaweza kuondolewa? Usiendelee kukawia kawia maana hujui siku mlango wa neema utafungwa mwako! Hivyo amua leo kumgeukia YESU na uzaliwe mara ya pili..

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *