
ACHA KUZIBA MASIKIO YAKO
Shalom karibu tujifunze maneno ya uzima.
Tunasoma kitabu cha Matendo ya Mitume 7:54-58, Neno la Mungu linasema..
“Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.
[55]Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.
[56]Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, WAKAZIBA MASIKIO YAO, wakamrukia kwa nia moja,
[58]wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.

Hawa watu waliposikia mahubiri ya kweli, wakashuhudiwa dhambi zao, na wakachomwa mioyo yao badala watubu..lakini wakaziba masikio yao, hawakutaka kutubu na kuacha njia zao za uovu.
Na hata sasa katika siku hizi za mwisho ndicho kinachoendelea, watu wanasikia injili ya kweli lakini WANAZIBA masikio yao, hawataki kugeuka kwasababu wamechagua kupenda giza kuliko Nuru.
Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.”
Kwahiyo hiyo hii ndio hukumu ya kuwa injili ya toba inahubiriwa ulimwengu kote, lakini watu kwasababu ya kupenda dhambi, wamechagua wenyewe kuziba masikio yao wasisikie habari hizi, kumbuka hawajazibwa na shetani, hapana ni wao wenyewe wamejiziba.
Mathayo 13:14 Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.
[15]Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, NA MACHO YAO WAMEYAFUMBA; WASIJE WAKAONA KWA MACHO YAO, WAKASIKIA KWA MASIKIO YAO, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.
Soma tena..
Matendo ya Mitume 28:27 “Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, NA KUSIKIA KWA MASIKIO YAO, Na kufahamu kwa mioyo yao, NA KUBADILI NIA ZAO, nikawaponya.
Jiulize we dada ni mara ngapi umesikia kuwa suruali kwa mwanamke ni machukizo kwa Mungu (kumb.22:5), ni mara ngapi umehubiriwa kuwa kuvaa vimini, nguo za kubana ni mavazi ya kikahaba na kwamba mwanamke wa kikiristo hapaswi kuvaa kikahaba (1Timotheo2:9), lakini hutaki kugeuka.
Umesikia na umeshuhudiwa kuwa hayo mapambo uliyoweka kwenye mwili wako (hereni, vipini, lipustiks, wanja, wigi, mekaups, kucha bandia, rangi bandia, nywele bandia) ni mapambo ya kipepo na kwamba yatakupeleka jehanumu (1Petro3:3) lakini umejitia ganzi kwenye masikio yako hutaki kusikia.
We kijana umehubiriwa vya kutosha na umesikia na kuchomwa na Neno la Mungu ili uache huo uasherati unaofanya, hizo miziki za kidunia unazosisikiliza, hizo picha chafu unazozitazama, hiyo kamari na magemu unazocheza, huo ulevi wa pombe na starehe za kidunia lakini UNAZIBA MASIKIO YAKO hutaki kusikia, unaendelea na uchafu wako.
Nataka nikuambie, leo usipokubali kufungua hayo masikio yako, muda na saa usiyoijua utajikuta kuzimu na utajuta majuto ya milele. (Nakuambia ukweli sio hukumu).
Hivyo kubali leo kutii wito wa Mungu unaokuita.
Tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Yesu ili upokee muhuri wa Roho Mtakatifu atakayekusaidia kuishi maisha ya utakatifu.
TUNAISHI KATIKA NYAKATI ZA MWISHO KABISA.
BWANA YESU ANARUDI.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.