SWALI,
Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema “Utoapo sadaka mkono wako wa kulia usijue ufanyalo mkono wako wa kushoto”
JIBU,
Hebu tusome kwanza hiyo habari katika kitabu cha Mathayo 6:1-4
Mathayo 6:1“ Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2 Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu
3 Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume;
4 sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.
Kwa hali ya kawaida ni vigumu mtu kutumia mkono mmoja na mwingine usiwe na ushirika..kwani viungo vya mwili zimeshikamanishwa kwa pamoja kiasi kwamba kila kiungo kinawasiliana na mwenzake, Kwahiyo ni ngumu kufanya jambo kwa mkono mmoja na mwingine usihusike,
Hivyo Bwana Yesu aliposema neno hilo, hakumaanisha tutoe sadaka kwa mkono mmoja huku tumeuficha mkono mwingine, bali alitumia ishara ya mikono kama mfano au picha tu.. kutufundisha namna ipasavyo kumtolea Mungu.
Bwana Yesu alichokuwa analenga ni sisi kumtolea Mungu pasipo kujiinua inua na kutafuta kuonekana na watu, matoleo yetu yanatakiwa yawe ni kwa siri sana, kiasi kwamba hata mioyo yetu isiinuke mbele za Mungu, tusiweke weke kumbu kumbu mbele za Mungu..tukishatoa tunasahau kabisa kwamba tulitoa.
Hebu tuangalie hawa watu wawili…
Luka 18:10 “ Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
11, Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; HUTOA ZAKA KATIKA MAPATO YANGU YOTE.
13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”.
Kwenye hiyo habari hapo juu, huyo mtoza ushuru haimaanishi kuwa hatoagi fungu la kumi au sadaka… hapana, alikuwa anatoa na yamkini hata zaidi ya yule Farisayo, lakini tabia aliyokunayo ambayo inapaswa na sisi tuwenayo ni kwamba.. alikuwa ni kama mtu ambaye hatoagi kabisa,
Kila akitoa hazikumbuki tena kama alitoa, na wakati anatoa hajiinui inui wala kujitangaza tangaza ili aonekane kama anatoa, au Mungu amwone, hahesabu wala haangalii kiasi alichotoa, tena akisimama mbele za Mungu anakua kama hajawahi kumtolea Mungu, anajihisi bado anapaswa kumtolea Mungu kana kwamba bado ana deni kubwa la kumtolea Mungu, tabia hiyo ikamfanya apate kibali mbele za Mungu, zaidi hata ya yule Farisayo ambaye alijtukuza moyo wake kwa sadaka zake,
Leo hii hali ni tofauti, mtu akitoa sadaka fulani labda kiasi fulani cha fedha utamkuta anajinadi na kusema sema, kujiweka weka ili tu watu wamwone kuwa ametoa, na wakati mwingine akiona kuna jambo halijakaa sawa pale kanisani au mahali anapotolea sadaka zake utasikia akilalamika lalamika, na kuwa na maneno maneno mingi kuhusu habari ya sadaka zake, utasikia akisema juzi nilitoa sadaka kiasi fulani au nilitoa hichi ila sioni hichi kikifanyika, sadaka zetu zinatumika vibaya,..
Na pia hata kama hatatoa hayo malalamiko, utakuta maombi yake ni ya kujiinua inua mbele za Mungu, moyo wake unakua umeinuka kwasababu ya utoaji wake, kiasi kwamba akiomba utasikia akimwambia Mungu nitasame mimi..ona ninakutolea sadaka nzuri Kila week,
Mungu angalia juzi tena nilitoa kiasi hiki, na mwezi uliopita nilikutolea hiki, anakua kama anamhesabia Mungu sadaka zake anazozitoa, kila akitoa anaweka kumbukumbu, kana kwamba anamfaidisha Mungu na si kama sehemu ya wajibu wake au Ibada yake,
Lakini kwa upande wa pili yupo mtu mwingine ambaye kila wakati anamtolea Mungu sadaka iliyo ya thamani kubwa..na wakati yupo kwenye maombi hathubutu hata kujinyajua kidogo na kuona kuwa anastahili,
Anakua kama hajawahi kumtolea Mungu, kiasi alichokitoa nyuma anakua kama kasahau, wala hahesabu kabisa matoleo yake, anakua kama hatoagi, (mtu kama huyu ndiye Bwana Yesu alimfananisha na mtu anayetoa sadaka huku mkono wake mmoja hajui afanyalo mkono wake mwingine)… yaani sadaka yake inakua kwa siri sana.
Kwahiyo Bwana Yesu alisema Neno hilo ili tuweze kujifunza jinsi ipasavyo kumtolea Mungu kwa adabu na unyenyekevu wa hali ya juu kama yule mtoza ushuru ambaye tumeona tabia yake, tujue tunapomtolea Mungu, au kuwapa watu misaada, tusitafute kuonekana au kutambuliwa na watu au na Mungu kwamba tumetoa,
tusikumbuke kumbuke kama tumetoa, zaidi tuendelee kumtolea Mungu zaidi na zaidi bila kukoma, ukishatoa sadaka zako, kuwa kama mtu ambaye hajatoa, usitafute njia yoyote ili ujulikane kuwa umetoa au kumfanya Mungu akuone, Ndivyo utaweza kupokea thawabu yako kwa Mungu, ila ukifanya kinyume chake usitegemee kupokea kitu wala thawabu yoyote Kwa Mungu, sadaka yako iwe Kwa siri na yeye mwenyewe atakujazi.
Bwana Yesu Kristo atusaidie sana tumtolee Kwa upendo na uzuri.
Fahamu kama bado injili inakufikia na huna habari nayo..hutaki kusikia, kila siku unahubiriwa uokoke, uache dhambi ili usiende jehanum, usikutwe na ghadhabu ya Mungu, hutaki kuacha uasherati wako, unafanya makusudi kuendeleanayo, umehubiriwa sana utoke kwenye ulevi wako, ulevi wa pombe, madawa ya kulevya kama sigara, ulevi wa filamu za kidunia kama movies, na ulevi wa mipira, miziki ya kidunia, na mambo yote ya ulimwengu huu, hutaki kuacha uvaaji wako mbaya we mwanamke..
kuvaa vimini, masuruali, na kutumia vipodozi, lipstick, mawigi, mahereni hutaki kuacha, mapambo yote na fashion za kidunia hutaki kuacha, we kijana hutaki kuacha kamari/kubeti, kutazama pornography na kujichua, na mambo yote machafu hutaki kuacha na unakimbilia kumtolea Mungu sadaka, Neno la Mungu linasema “kutii ni bora kuliko dhabihu (1Samweli 15:22)”..na tena biblia inazidi kusema…
Mhubiri 5:1 “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya”.
Na vilevile maandiko yanasema “Sadaka ya wasio haki ni chukizo;…(Mithali 15:8)”
Na pia..
Kumbukumbu 23:8 Neno la Mungu linasema ” Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.”
Mshahara wako unaoupata kwenye kazi yako ya ukahaba, kazi yako ya kuuza bar, kuuza biashara haramu, ukampelekea Mungu ukidhani ya kuwa Mungu atakufurahia na kustiri uovu wako Kwa sadaka yako… unazidi kumchukiza Mungu,.. Mungu hana haja na fedha zako ulizopata kwenye umwagaji wako wa damu, kwenye wizi wako, au kwenye kazi yoyote ambayo ni machukizo kwa Mungu,
Mungu anachotafuta kwako ni roho yako iokoke na ziwa la moto, ni vizuri kuelewa kuwa sadaka ni sehemu ya shukrani kwa Mungu..sasa ni shukrani gani unataka kumpa Mungu ingali hutaki kutii neno lake kama si unamnafikia tu Mungu, na kumfanya akuhuzunikie.
Hivyo basi, ndugu yangu kama hujampokea Bwana Yesu, bado neema ipo, ila haitakuwepo siku zote, kabla hujawaza kumtolea Mungu, hebu wazia kwanza kuacha na roho zinazokutumikisha kwenye uasherati wako, kwenye ulevi wako na nyingine zote ndipo ufikirie jambo la kumtolea Mungu bila kujiinua kwake..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.