Jina kuu la Bwana wetu Yesu KRISTO Mwokozi wa ulimwengu litukuzwe, karibu tujifunze Neno la Mungu.
Mji wa Serepta ni mji mdogo uliopatikana katika Taifa la Lebanoni, nje kidogo mwa nchi ya Israeli,
Nyakati za biblia kipindi ambacho mvua ilizuiliwa miaka mitatu na nusu Kwa kwa Neno la Bwana kupitia mtumishi wake Eliya, Bwana alimwongoza Eliya afike hadi mji huu wa Serepta na huko alikutana na mama mmoja ambaye Bwana alimtayarisha ili amtunze kwa chakula.
Bwana hakushindwa kumletea mtumishi wake Eliya chakula toka mbinguni, ila hakumletea, isipokuwa alitumia watu na ndege kumlisha kipindi ambacho dunia yote inateseka na njaa kwa ajili ya ukame, tunaona mara ya kwanza Bwana alitumia kunguru(1Wafalme 17:4), na baadaye akatumia mwanadamu(huyu mama wa Serepta).
Huyu mama wa Serepta ni mwanamke wa kipekee sana kwani alikuwa na tabia ya tofauti sana..kwa kweli tabia yake ina funzo kubwa kwetu sisi tunaohitaji mafanikio ya mwilini na rohoni.
Pengine mambo yako hayajanyooka, labda unapitia nyakati ngumu sana ya ukame wa mbingu kufungwa kwenye utafutaji wako wa mafanikio, labda umejaribu kila namna ila bado hali ni ngumu,
Iwapo unapitia hali kama hiyo, basi usiangaike huku na huku kutafuta maombezi! unachotakiwa kufanya ni kama alivyofanya huyu mama wa Serepta.
Kama utatenda kama alivyotenda huyu mama wa Serepta, hakika utakuwa kwenye furaha tele, wakati wengine wanateseka na ukame, majanga na matatizo kadha wa kadha..
Sasa ni nini alichokitenda huyu mama hadi kuweza kufikia hatua ya kufurahia maisha wakati ambao wengine wanalia na njaa na vifo?
Hebu tuone kwa ufupi habari zake alafu tujifunze tabia ambaye alikuwa nayo.
1Wafalme 17:7 “Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.
8 Neno la Bwana likamjia, kusema,
9 Ondoka, uende Serepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe
10 Basi, akaondoka, akaenda Serepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.
11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.
12 Naye akasema, kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.
13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.
14 kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.
15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.
16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya”.
Tabia ya huyu mama… alikuwa tayari kutoa mkate wake mdogo aliobakia nao…pasipo kuangalia kesho yake nini kingemtokea..aliacha kujiuliuliza juu ya maisha yake, akafanya kila linalowezekana ilimradi tu mtumishi wa Mungu aendelee kusambaza Neno la Mungu, alitambua mtumishi wa Mungu, au kazi ya Bwana ni bora zaidi kuliko kazi zake mwenyewe au uhai wake na mwanae.
Kwahiyo akakubali kujihatarisha maisha yake…akifahamu kuwa hata kama wangekufa pamoja na mwanae…kule mbinguni wangeenda kupokea thawabu kubwa sana, na huku kazi ya Mungu inaendelea…na hiki alichokifanya ndicho kilimfanya Mungu amsaidie matatizo yake, na kumfungulia milango ya mafanikio huku wengine wakiangaika bila majibu.
Na Mungu bado hajabadilika, na wala hatowahi kubadilika, yeye ni yule jana, leo na hata daima (Waebrania 13:8)..Iwapo unahitaji Mungu ayatazame maombi yako, huna budi kuweka pembeni mambo yako, shida zako, matatizo yako, na uanze kufanya kazi ya Mungu..
Na hii ndilo tatizo linalowakumba watu wengi, mara nyingi wanakimbilia kupeleka matatizo yao mbele za Mungu na hao wenyewe hawataki kumtafuta Mungu katika maisha yao… wanakimbilia kuombewa mambo yao yakae vizuri, ila kutengeneza uhusiano wao na Mungu na kufanya Kazi ya Mungu hawataki..
Watampelekea Mungu malalamiko, Mungu angalia watoto wangu hawana chakula, mwanangu amefukuzwa shuleni ada, watoto wangu wameharibika, mimi sina chakula, sina cha kufanya, sina hiki na kile,..(ni watu ambao wanaangalia tu mambo yao) wala mambo ya Mungu hapana! kazi ya Mungu hawana habari,..wakifikiri eti kwasababu Mungu anaweza kila kitu, basi hana haja na kitu chochote, hastahili kutendewa lolote.
Kwa kweli Mungu anaweza yote, na hana haja ya kutendewa ama kupewa chochote, ila mara nyingine Mungu anapima upendo wetu kwake,..asingeshindwa kumshushia Eliya mana kama alivyofanya kwa Wana wa Israeli kule jangwani ila hakumshushia Eliya hicho chakula cha mbinguni, bali alimwendea huyu mama wa Serepta ili ampime upendo wake kwake,
Watu wengi hawana ufahamu kuwa Mungu hafurahishwi sana na matoleo yetu wakati ambapo tumeshiba, tuna vingi,.. kuliko kipindi ambacho tuna njaa… wakati ambapo hatuna vingi,..labda utauliza ni wapi katika biblia inavyoonesha hili,? Kumbuka habari ya yule mwanamke mjane ambaye alitoa riziki yake yote akatia ndani ya sanduku la sadaka,… baada ya kutoa Bwana Yesu alimpongeza, na zaidi alisema huyo mwanamke alitoa zaidi ya wote, kwamaana hao wengine walitoa katika sehemu zilizobaki katika mali zao,..
Marko 12:41 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.
42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.
43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;
44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia”
Tunaweza kusema huyu mjane, hakubakiwa na chochote, inawezekana alifikiri baada ya kutoa atashinda na njaa siku nyingi…ila wakati yupo kwenye hiyo hali, Bwana Yesu alimsifia ,…labda baada ya ile ibada, huenda alishangaa vile milango ya mafanikio ilivyomfungukia.
Vivyo hivyo na wewe kama unahitaji kuona milango ya mafanikio ikikufungukia mbele yako..usiwe na visababu vingi katika kumtolea Mungu, usifikiri juu ya shida zako, usianze kupiga mahesabu ya mahitaji yako, labda utaanza kujiuliza sina chakula, sina kodi, nadaiwa ada, nataka nifanye hiki na kile, au sina hiki na kile,.. usisubiri kupata kiasi kikubwa, usisubiri matatizo yaishe,..ni kweli unaweza ukasema ngoja nikusanye nikipata nitatoa, na kweli ukipata utatoa na Mungu atakubariki!!!! shida hujui tarehe wala siku ambayo utapata vile unataka kupata, na pia kumbuka matatizo hayaishi.
Katika kipindi cha Eliya Nabii… walikuwepo wanawake wengi sana wenye matatizo ya chakula kama tu huyu wa Serepta…na wenyewe wanaweza kuwa walikuwa wanaomboleza na kulia Mungu awajalie chakula kwasababu ya huo ukame…ila tunaona Eliya hakuagiziwa kwao shida ni hiyo hiyo, pengine angefika kwao na kuwaambia wamtengenezee kwanza mkate, wangemrushia mawe na kumtupia matusi.
Wangejitetea kwamba hatuwezi kuangalia watoto wetu wakifa na njaa halafu wewe mtu mzima tukupe chakula cha watoto,… pengine wangethibitisha kabisa kwa kutumia biblia kwamba wanachokisema ni sawa..kila mmoja angejitetea kwa namna yake kwamba kwanini hawezi kutoa mkate wake kumpa mtu wa Mungu….hiki ndicho Bwana Yesu alichokiongelea katika kitabu cha Luka 4:25
Luka 4:25 “lakini, kwa hakika nawaambia Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima;
26 wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Serepta katika nchi ya Sidoni”.
Vilevile na sisi ili tuweze kufunguliwa milango ya baraka kabla hata ya wakati wake kama mbingu zilivyomfungia huyu mama kabla ya wakati, ni lazima kuangalia kazi ya Mungu zaidi ya kazi zetu, ni lazima tuangalie mambo ya Mungu zaidi ya tunavyoangalia mambo yetu, moja ya kanuni ya mafanikio ni hii.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.