Elewa maana ya neno, ameshiba siku, mwanzo 35:29

Maswali ya Biblia No Comments

Shalom,

Biblia inasema na tumfahamu sana Yesu Kristo hata tufikie kimo cha ukamilifu (Waefeso 4:13),

Imekuwa ikiaminika kwa asilimia kubwa kuwa mtu aliyeshiba siku ni yule aliyeishi miaka mingi, au mwenye miaka mingi akiwa hai, jambo ambalo halina ukweli kulingana na biblia..

Kama ni msomaji wa maandiko utagundua hilo siyo jambo jipya, kwasababu kuanzia agano la kale watu walikuwa wanaweza kuishi mpaka miaka mia tano na kuendelea,kwa  misemo yetu tunasema ameishi miaka mingi au (amekula chumvi nyingi) hivyo linamtambulisha kama ameshiba siku,

Tunaliona hilo likiendelea mpaka pale Mungu alipopunguza kipindi cha kuishi kwa wanadamu na kufikia miaka 70-80, (zaburi 90:10)

Pamoja pia na miaka kupunguzwa bado watu waliendelea kuona hata kwa miaka michache hiyo ukiishi unaonekana umeishi miaka mingi,..

Lakini nataka ujue hiyo siyo tafsiri yake kulingana na maandiko,mtu aliyeshiba siku ni yule aliyetembea na Mungu Katika kipindi chote alichokuwa duniani mpaka anaondoka,mtu huyu Mbele za Mungu anaonekana ameshiba siku, amejitenga na dhambi,na uovu na mambo mabaya ya ulimwengu hu  na kujitakasa na kuishi maisha Matakatifu yenye kumpendeza Mungu,

Mhubiri anasema…

Mhubiri 6:3
[3]Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo;

Umeona hapo, haijalishi utaishi miaka mingi kiasi gani kama hutendi yanayompendeza Mungu, huna uhusiano wowote na muumba wako, anasema ni heri mimba iliyoharibika kuliko huyo mtu..

Henoko alitembea na Mungu miaka mia tatu, mwisho wake ukawa ni kunyakuliwa tu hata kifo hakukionja

Mwanzo 5:22-24

[22]Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake.

[23]Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano.

[24]Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa.

Utaliona hilo kwa kwa baba zetu wa imani, Ibrahimu,Isaka na Daudi, biblia inawataja kama ni watu walioshiba ijapokuwa sio kwamba waliishi miaka mingi bali ni kile kipindi walichomtumikia Mungu Mpaka kifo kilipowakuta..

Mwanzo 25:7-8

[7]Hizi ndizo siku za miaka ya maisha ya Ibrahimu alizoishi, miaka mia, na sabini na mitano.

[8]Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake.

Mwanzo 35:28-29

[28]Siku za Isaka zilikuwa miaka mia na themanini.

[29]Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika

1 Mambo ya Nyakati 29:28

[28]Akafa mwenye umri mwema, ameshiba siku, na mali, na heshima; naye Sulemani mwanawe akamiliki badala yake..

Jambo hili pia lipo kwa wale waliompokea Yesu Kristo Katika maisha yao na kudumu Katika Wokovu na kujiweka mbali na mambo maovu ya ulimwengu, WaKristo hawa wakiendelea kusimama imara  na kutembea na Mungu katika imani watakutwa na tukio linalojulikana kama unyakuo, sawa tu na  henoko, kwa kuwa rohoni wanaonekana wameshiba siku, hivyo hawana namna zaidi ya kupumzika kwa amani kwa kunyakuliwa wasionje mauti kwa maisha waliyoishi ya kumpendeza Mungu..

1 Wathesalonike 4:17-18

[17]Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

[18]Basi, farijianeni kwa maneno hayo.

Hivyo ukitaka uonekane na Mungu umeshiba siku  kwa kipindi kifupi cha maisha yako,wewe mtumikie Mungu,ishi kulingana na Neno lake,jiepushe na dhambi na mambo yote mabaya ya ulimwengu..

Ubarikiwe..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *