ENDELEA MBELE USITAZAME NYUMA

Uncategorized No Comments

ENDELEA MBELE USITAZAME NYUMA

Nakusalimu katika jina tukufu la Bwana Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya Mungu.

Na siku ya leo tutajifunza umuhimu wa kuendelea mbele katika safari ya imani.

Bila shaka safari ya imani ni safari ndefu yenye milima na mabonde kama ilivyo kwa safari zingine za haya maisha.

Lakini pamoja na hayo, ipo kanuni moja ambayo tukiitumia katika safari yoyote iwe ya imani au hata ya maisha tu ya hapa duniani bila shaka tutafanikiwa kufika tunakokwenda salama.

Na kanuni hiyo ni KUENDELEA MBELE, kwa hakika tukiitumia hii kanuni tutafika tu..hata kama tutakutana na vikwazo vya aina gani.

Tukirudi katika biblia, tunasoma kuhusu habari ya ile safari ya wana wa Israeli wakiwa njiani walikutana na kikwanzo kikubwa ambacho kilitaka kuwarudisha walikotoka, ila Bwana akawaambia kanuni ni kuendelea mbele.

Kutoka 14:10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.

[11]Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?

[12]Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.

[13]Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.

[14]BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.

[15]BWANA AKAMWAMBIA MUSA, MBONA UNANILILIA MIMI? WAAMBIE WANA WA ISRAELI WAENDELEE MBELE.

Hiyo ndiyo kanuni katika safari ya imani na maisha haya yenye milima na mabonde ni kuendelea mbele pasipo kutazama ukubwa wa tatizo.

Ukikutana na kikwanzo chochote aidha katika huduma yako, wokovu wako, usitazame nyuma, wala usiangailie mazingira..we endelea mbele maana ipo nguvu ya ziada katika kuendelea mbele, upo muujiza ambao utaona..kwani siku zote yale yasiyowezekana kwa nguvu zetu na akili zetu ni ya Mungu.

Ukikutana na changamoto za Afya, uchumi, familia usirudi nyuma, simama imara na ukumbuke hii kanuni ya kuendelea mbele.

Kadhalika unapotengwa na ndugu, marafiki, au kufukuzwa kazi na boss wako kwa sababu ya imani, usitazame nyuma maana hizo ni hila za adui shetani kukurudisha nyuma, we endelea mbele, haijalishi umepoteza kila kitu, haijalishi unasemwa kwa maneno gani, haijalishi unatukanwa na kuitwa majina ya kila aina, we endelea mbele,

Endelea mbele katika utumishi, endelea mbele katika wokovu, usimpe Ibilisi nafasi akurudishe nyuma kamwe.

Vile vile ukitaka kuwa muombaji wa masafa marefu.. kanuni ni kuendelea mbele hata pale unapoona uzito fulani.. endelea mbele hakika Bwana atakuongezea nguvu na utajikuta unakesha hata katika kuomba.

Lakini kama ulikuwa umeshaanza kurudi nyuma, bado hujachelewa hebu kataa hiyo njia na leo mwombe Bwana rehema na kuziacha hizo njia utaona maajabu ya Bwana, kwani atakutia nguvu na utaendelea mbele kwa mbio kubwa, Bwana atakurehemu na utamfurahia.

2 Wafalme 4:24 Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia.

Je umempokea Yesu? Unahabari kuwa tunaishi ukingoni mwa siku za nwisho?

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *