Fahamu Injili inayopatikana katika mimea chungu.

Biblia kwa kina No Comments

Fahamu Injili inayopatikana katika mimea chungu.

Je unafahamu kuwa kila kitu unachokiona kinahubiri injili ya Yesu Kristo?

Shalom, jina kuu tukufu la Bwana Yesu libarikiwe milele na milele. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Bwana wetu Yesu alitoa mifano mingi tofauti tofauti ya vitu vya hapa duniani kuelezea/kuhubiri Injili ya ufalme wa Mungu, ukisoma biblia utaona sehemu nyingine anafananisha ufalme wa Mungu na lulu ya thamani, hazina iliyostirika, mkulima, mfanyabiashara, mvuvi, mwizi, punje ya haradali, chachu, n.k n.k

Na sehemu nyingine anatuambia tufakari ndege wa angani, tuangalie maua ya kondeni,..hii Ikiwa na maana karibia vitu vyote tunavyoviona hapa duniani vinabeba injili ya ufalme wa Mungu, ndio maana biblia inasema katika..

Zaburi 119:19 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, MAANA VITU VYOTE NI WATUMISHI WAKO.

Yohana Mbatizaji aliwaambia wayahudi..

Mathayo 3:8-9 “Basi zaeni matunda yapasayo toba;

[9]wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto”.

Ikiwa na maana sisi watu wa mataifa hapo kwanza tulikuwa tunafanana na mawe yasiyokuwa na uhai.. lakini kupitia YESU KRISTO yeye ambaye ni jiwe lililo hai, nasi kwa neema yake tunafanyika watoto wa Ibrahimu (mawe yaliyo hai)

1 Petro 2:1-5 Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.

[2]Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;

[3]ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.

[4]Mmwendee yeye, JIWE LILILO HAI, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima.

[5]Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.

Umeona hapo, kumbe mawe yanabeba siri kuu za ufalme wa Mungu, vivyo hivyo na miiba, magugu, mizizi, upepo, miti, maua, mimea, mbegu, na vitu vingine vyote vilivyo hai na visivyo hai vinabeba injili ya Yesu Kristo, ni hekima tu ya Roho Mtakatifu inahitajika ili kufahamu siri hizo.. hivyo tunapaswa tuwe watu wa kutafakari sana na kutafuta ufalme wa Mungu kwa bidii sana maana ndiyo agizo tulilopewa. Usiichie tu kusoma biblia yote ukasema tayari umeshamaliza.

Hivyo siku ya leo, tutaona injili mojawapo ambayo inapatikana kwa mimea.

Kama tunavyojua, zipo mimea yenye ladha tofauti tofauti, zingine zina ladha ya uchachu, zingine ladha chungu na zingine tamu. Sasa hebu tuangalie mimea yenye ladha ya uchungu.

Tunafahamu kuwa siku zote mwanadamu hapendi kitu chenye ladha ya uchungu, lakini katika tafiti nyingi, vitu vingi vyenye ladha ya uchungu ndiyo zinatumika kutatua matatizo mengi ikiwamo maradhi mbali mbali, hata wewe mwenyewe bila shaka umewahi kutumia dawa ya miti shamba au ya hospitalini kwa namna moja au nyingine.

Sehemu kubwa ya haya madawa tunazotumia mahospitalini zimetokana na mimea na ni mimea yenye ladha chungu, ndio maana dawa yenyewe ni chungu..na ili upone huna budi kunywa.

Kwahiyo tunaona pamoja na kuwa mimea hii haipendwi kutumiwa na watu wengi kwasababu ya ladha yake chungu…ndio mimea ambayo inafaida nyingi ndani ya mwili wa mwanadamu na hata wanyama, ndio maana wale wanyamapori mara nyingi hawaumwi umwi kirahisi kwasababu wanatumia mimea yenye dawa.

Ni kweli unapoweka mdomoni..utahisi uchungu lakini..ikiingia tumboni inakuwa dawa.

Sasa tukirudi katika mambo ya rohoni, mimea michungu inafanana na kile kitabu kidogo ambacho Yohana aliambiwa akile nacho kilikuwa kitamu kinywani mwake lakini tumboni kiligeuka kuwa kichungu.

Ufunuo wa Yohana 10:8-11 “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.

[9]Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

[10]Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

[11]Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.”

Hapa Yohana anaambiwa akitwae kitabu akile, kwa namna ya kawaida huwezi kula kitabu, kwahiyo hilo ni ono, na kitabu hicho hakuambiwa akisome, hapana bali akile…kusoma ni tofauti na kula, mtu asomaye anaingiza taarifa katika Akili yake…lakini mtu alaye anaingiza taarifa au uzima ndani ya mwili wake…Kwasababu kile alichokila kinaingia katika tumbo lake kisha kinameng’enywa na kuingia katika damu na mfumo wa mwili mzima…baadaye kile alichokila kinageuka sehemu ya yeye kinageuka na kuwa nyama yake, misuli yake, Ngozi yake n.k…

Na sisi Neno la Mungu hatujapewa kulisoma tu au kulikariri hapana! bali tumepewa tulile katika roho, ndio Maana Bwana anasema yeye ni “chakula cha uzima” ili kitakapoingia katika miili yetu ya roho kiwe ni sehemu yetu!..

Neno la Mungu au kwa jina lingine linaitwa Gombo, ni dawa inayoponya maisha ya mtu kwa ujumla.Tofauti na Dawa nyingine, ambazo zinaweza kuishia kuponya mwili tu, na baada ya hapo hakuna kitu kingine zinaweza kufanya, na licha tu ya kutibu kifo bali hata nafsi iliyopondeka hakuna dawa yoyote inayoweza kuiponya isipokuwa Neno la Mungu peke yake, (Mithali 4:20-22), Na hiyo ndio inayolifanya Neno la Mungu liwe ni dawa bora kuliko dawa yoyote ambayo ilishawahi kuwepo duniani.

Lakini pia kabla ya kuzifurahia dawa tunapaswa tujifunze asili ya dawa jinsi zilivyo, kama mtu hajui dawa huwa zinaasili gani basi ni rahisi kukata tamaa na asikae arudie tena kuzijaribu ..Kwasababu sikuzote dawa huwa hazina ladha nzuri mdomoni, dawa nyingi ni chungu, tena chungu kweli kweli kiasi kwamba zinakufanya uzimeze nzima nzima, vinginevyo unaweza kutapika endapo ukizitafuna..labda ni kutokana na mimea inayotoa nayo kuwa chungu, Lakini tunajua pamoja na uchungu wake wote huo zikishafikia tumboni basi uchungu wote unakuwa umeisha hatuusikii tena, baada ya hapo tunasubiria tu matokeo mazuri ya kuponywa miili yetu, na mwisho wa siku tunazifurahi zile dawa, tunazisifia japokuwa hapo mwanzoni tulikuwa tunakunja nyuso zetu kama vile tunamezeshwa sumu.

Vivyo hivyo tunapaswa pia tujue asili ya dawa KUU (Neno la Mungu) pale tunapokusudia kulila, kwa lengo la kupata uzima, linatabia gani rohoni mwetu..Tofauti na dawa za asili kwamba tunapozila zinakuwa chungu mdomoni mwetu lakini zikifika tumboni zinakuwa ni raha..Neno la Mungu (Gombo) ni kinyume chake.. biblia inasema Mdomoni ni tamu kama asali lakini likifika tumboni libadilika na kuwa chungu sana…

Yohana alipopewa kitabu kile (yaani Ufunuo ule) aule alipewa angalizo hilo mapema kabisa tusome tena..

Ufunuo 10:8 “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.

9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi”.

Ezekieli naye aliambiwa hivyo hivyo…

Ezekieli 2:9 ‘Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.

10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!

3:1 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.

3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali”

Unaona asili ya dawa KUU (Neno la Mungu), ni tamu kama asali, wengi tunaposikia habari za kwenda mbinguni kwa kumwamini tu YESU tunafurahia, tunaposikia Yesu anakupenda mwenye dhambi tunafurahia, tunaposikia mafunuo mapya kila siku Kristo anayotufundisha kila kona juu ya habari za ufalme wa mbinguni tunafurahia sana, ni asali nzuri, tunaposikiwa tunahesabiwa haki kwa neema, tunafurahia Zaidi, tunaposikia alifanyika maskini ili sisi tuwe matajari ni maneno mazuri yenye faraja..Hiyo inatufanya wengi tuvutiwe na wokovu, si ndio?..Lakini ili Neno la Mungu lifanye kazi yote ya kumwokoa mtu ni lazima lishuke tumboni limengenywe Uponyaji wa Roho yake uanze kufanya kazi na ndio hapo uchungu unapoanzia..

Wengi wanaishia kulitapika na kurudi nyuma kama vile mtu atapikapo dawa chungu asijue ndiyo njia ya yeye kuponywa, wanafananishwa na zile mbegu zilizoangukia kwenye miamba, ambao ni watu waliopitia dhiki kidogo tu kwa ajili ya lile Neno wakajikwaa wakarudi nyuma.., Pale Bwana Yesu anaposema jitwike msalaba wako unifuate, wengi hawataki kusikia hivyo, wanataka waendelee kukaa katika dhambi zao na huku wanasema wameokoka, wanataka waendelee kwenda disko na huku wanasema tumeokoka na tumebatizwa, wanataka waendelee kuvaa vimini na suruali na kuweka make-up na huku waseme tumeokoka tunampenda Yesu.

Wanadhani kuwa wameokolewa kweli,?.. Sio tu kufurahia unahubiriwa kila siku Neno la Mungu unasema sasa ninajua mafunuo mengi, ukadhani ndio tayari Umekamilishwa Maisha yako, Hapo ndugu bado hujaanza ikiwa hutataka kuyatiii maneno Bwana Yesu aliyoyasema, basi ujue kuwa wokovu wako ni batili.

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

Injili imekuvuta kwa maneno mazuri na ya faraja kwa muda mrefu, umeshauona uzuri uliopo ndani ya Kristo kwa muda mrefu, umeshajua faida zote mtu anazozipata akimfuata Kristo, unaendelea kulifurahia tu Neno la Mungu mdomoni mwako lakini hutaki kulimeza, kisa tu unaogopa Baba atanitenga, mama atanichukia, marafiki watanionaje..kazini watanifikiriaje, wakisikia mimi nimeokoka,..Ndugu kama unapenda Kristo ayaokoe Maisha yako kikweli kweli unapaswa ufanye maamuzi hayo pia..

Injili ya kweli inafananishwa na zile dawa chungu au mmea mchungu ambayo mtu akipokea na kuweka ndani ya mwili wake anapona, ni kweli unapoisikia injili ya kweli itakutia uchungu.. kwasababu ukiamua kutii hiyo injili na kumfuata Yesu kwa ukamilivu, ni kweli hautapendwa na watu wote..yamkini hata ndugu wa karibu wakakutenga, au ukapoteza kazi, n.k lakini hiyo ndiyo njia ya kupata wokovu, Kwahiyo ni lazima ukubali kuinywea hiki kikombe hata kama ni kichungu.

Mathayo 10:34 “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;

36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.

Huu ni wakati wa kuyapokea maneno ya Mungu kwa moyo wote na kuyafanyia kazi, hizi ni siku za mwisho za kanisa la watu walio vuguvugu lijulikanalo kama Laodikia (Ufunuo 3:14)ambao watu wake ni watu walio vuguvugu wa hali ya juu sana..Na hao Kristo amesema atawatapika. Je na wewe unasubiri utapikwe baada ya kukaa katika uvuguvugu huo kwa muda mrefu?. Fanya uamuzi wa kulimeza Neno lote zima zima bila kujali ni nini kitakutokea mbele kwasababu kwa kufanya hivyo ndivyo utakavyoinusuru roho yako katika nyakati hizi za uvuguvugu ambao kila mtu hata mlevi, mzinzi, fisadi, hata msanii wa nyimbo za kidunia anasema ameokoka..

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *