Fahamu Maana halisi ya Kuabudu.
Shalom, Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Kuabudu ni Neno ambalo limezoeleka kwa Wakristo wengi sana. Karibu Wakristo wote wanalisema neno hili. Wachungaji, waimbaji wa nyimbo za injili, nk lakini wengi haswa hawafahamu/hatufahamu maana halisi ya Neno hili “ Kuabudu ” ni neno ambalo lina maana pana sana ndani yake na sio Neno tu bali ndio maisha/njia bora na pekee ambayo mtu aliezaliwa mara ya pili anatakiwa kuishi.
Sasa Wakristo wengi wanaposikia kuabudu na ndio inavyojulikana kwa wengi kwamba “ kuabudu ni kuimba nyimbo za utulivu yaani za polepole zenye biti linalolia taratibu sana huku umenyoosha mikono na kumtafakari Mungu, yaani kuanzia vyombo mpaka waimbaji na Washirika wote wanakuwa katika hali ya utulivu nk basi huko ndio kumwabudu Mungu ”
Ndugu yangu kuabudu si hivyo tu hiyo ni sehemu ndogo sana. Kuabudu ni zaidi ya hicho kitendo kuabudu ni maisha ya Mkristo yeyote na ni wakati wote wala sio tukio fulani tu.
Na ndio maana Bwana Yesu anamwambia Mwanamke Msamalia pale kisimani maneno haya…
Yohana 4:23
“Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”
Unaona hapo? Anasema “…. kwa Maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” Kwamba Mungu mwenyewe yupo katika mkakati wa kuwatafuta watu wa namna hii.
Maana yake watakaofanya hivyo siku zote..
Sasa nini maana halisi ya Kuabudu?
Kuabudu ni kujitoa kikamilifu kwa moyo, nafsi, na mwili mbele za Mungu kwa unyenyekevu ukiruhusu yeye atawale katika maisha yako, ukimtambua kuwa yeye ni wa pekee, wa thamani kuliko kila kitu, na anayestahili heshima yote .
Ni tendo la upendo wa ndani kabisa, linaloonyesha utiifu, hofu ya Mungu, na mshikamano wa rohoni kati ya aliyeumbwa na Muumba wake yaani (Mungu na wewe/ Yesu Kristo na wewe)
Si nyimbo tu au sala, bali ni mtindo wa maisha unaomtukuza Mungu hata katika ukimya(maisha ya sirini) na matendo ya kila siku.
Na ndio maana Yesu anasema sentensi kama ile kwa mwanamke yule watu wengi(mababa wa imani) walimwabudu Mungu katika maeneo mbali mbali ya maisha yao.
1.Ibrahimu
Wote tunajua kuwa huyu ndie baba wa imani Wakati Mungu alipomwambia akamtoe mwanae Isaka Ibrahimu alitii kwa kufahamu Mungu ni nani?,alimuamini Mungu,alikuwa na hofu ya Mungu,alijua Mungu ni wa thamani kuliko hata Isaka si kwamba alikuwa anamchukia Isaka, alijitoa kikamilifu kwa Mungu na ndio yalikuwa maisha yake.. Ibrahimu anawambia maneno haya wajakazi wake.
Mwanzo 22:5
“Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu , na kuwarudia tena.”Unaona hapo? Kitendo cha kwenda kumtoa Isaka Ibrahimu anakiita “ Kuabudu” hasemi ninakwenda kuimba na kufanya sara la! Ni zaidi ya hapo. Soma Mwanzo 22:12 Mungu anakiita kitendo hicho hivyo hivyo.
Kwamba anamcha kwa maana anamtii na kusikiliza kile anachotakiwa kufanya na kutekeleza.
Utii wa Ibrahimu haukuwa siku moja yalikuwa ni maisha ya Ibrahimu tangu anaambiwa atoke asijue aendako na atafanywa kuwa taifa kubwa.
2.Musa
Kutoka 34:8
“Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu .”
Ukisoma kwenye biblia za kiingereza tafasiri pana zaidi anasema Worshiped(kuabudu)
Exodus 34:8
[8]And Moses made haste to bow his head toward the earth and worshiped .
Haya yalikuwa maisha ya Musa tangu ajue kuwa yeye ni nani akawa tayari kuacha ufarao Misri na mwisho kutii kuja kuwatoa wana wa Israeli utumwani kwa mkono hodari wa Mungu.
Mtu mwingine ni Daudi alikuwa ni anamwabudu Mungu kikamilifu Zaburi 95:6.
Vivyo hivyo maandiko yanatutaka kuitoa miili yetu kuwa sadaka(ukishaokoka tambua Mwili wako ni sadaka kwa Mungu Mungu atautumia kufanya shuguli zake)
Warumi 12:1
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.”
Katika tafasiri ya Amplified anasema..
Romans 12:1
[1]I APPEAL to you therefore, brethren, and beg of you in view of [all] the mercies of God, to make a decisive dedication of your bodies [presenting all your members and faculties] as a living sacrifice, holy (devoted, consecrated) and well pleasing to God, which is your reasonable (rational, intelligent) service and spiritual worship.
Yaani kwa Lugha nyepesi anasema…
Warumi 12:1
“Nawasihi sana ndugu zangu, kwa sababu ya rehema nyingi za Mungu, mjitoe kikamilifu kwa Mungu yaani, miili yenu yote, mawazo yenu, na maisha yenu yote iwe kama dhabihu iliyo hai, takatifu, na inayompendeza Mungu. Hii ndiyo ibada ya kweli, ya kiroho, na yenye akili inayostahili kufanywa na kila aaminiye.”
Mungu hataki tu tumtolee Sadaka za fedha tu na wala si kwamba anavutiwa sana na sadaka zetu kanisani kutoa na kuendelea na mambo yetu la! Mungu anavutiwa na anataka kuyatoa maisha yetu wenyewe(kwa hiari baada ya kutambua) ikionyesha tunamtii na tunampa Heshima. (Si kwamba sadaka za vitu usitoe, toa sana lakini maisha yako zaidi Mungu ndio anataka umtolee.)
Na huu ndio msingi kamili wa kuabudu katika agano jipya kuishi maisha yanayoonyesha kuwa Mungu ni Bwana wa kila sehemu ya maisha yetu. Na huku ndio kuabudu halisi na hawa ndio Yesu alikuwa anamwambia msamaria pale kisimani Mungu anataka watu wa namna hii..
Je unamwabudu Mungu katika Roho na kweli? Umejitoa kikamilifu kwa Mungu wako? Kama bado anaza sasa hujachelewa.
Mtukuze Mungu katika maisha yako katika kila eneo kwa neema zake Mungu atakuwezesha.
Na hii ndio maana halisi ya Kuabudu ni zaidi ya kuimba nyimbo za taratibu,ni zaidi ya kuomba maombi mengi vyote hivi ni sehemu ya kuabudu lakini kuabudu fahamu ni maisha yako katika Kristo.
Ubarikiwe sana.
Maranatha.
Mawasiliano:0613079530.
@Nuru ya upendo.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.