Fahamu mamlaka uliyonayo baada ya kuzaliwa mara ya pili.

Biblia kwa kina No Comments

Fahamu mamlaka uliyonayo baada ya kuzaliwa mara ya pili.

Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe.. karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Pindi tunapozaliwa mara ya pili tunakuwa ni watu wa tofauti kabisa na kipindi tukiwa bado hatujazaliwa mara ya pili.

Tunapozaliwa mara ya pili tunapokea nguvu/mamlaka ndani yetu ambayo hapo kabla hatukuwa nayo kama maandiko yanavyosema..

Yohana 1:12
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”

Unaona hapo anasema “….Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu..” kwa maana nyingine uwezo huo hawakuwa nao kabla hawajampokea.. na waliompokea ni wakina na nani? ni mimi na wewe tuliemwamini Yesu Kristo ili atawale maisha yetu.

Sasa Wakristo wengi waliomwamini Yesu Kristo kweli kweli tayari wamepokea mamlaka makubwa sana ndani yao. Tambua kuwa Kristo kakupa mamlaka makubwa sana ndani yako.

Sasa Wakristo wengi hawajui mamlaka waliyonayo ndani yao na wanajikuta wanaishi maisha ya chini ya kiwango katika eneo la rohoni mpaka mwilini.. wanajikuta ni wale wale tu hawabadiriki kwa sababu hawajui wao ni wakina na nani baada ya kuzaliwa mara ya pili.

Watoto wa Mungu tumepokea mamlaka kubwa/uwezo/nguvu ndani yetu lakini hatujui namna ya kuitumia ili ilete matokeo chanya katika maisha yetu.

Ukweli ni kwamba Mungu anataka kuona matokeo ama tunatumia mamlaka tuliyonayo ndani yetu ili itusaidie sisi na wengine pia.

Ukweli ni kwamba mamlaka/nguvu tuliyonayo ndani yetu ni kubwa zaidi ya Nguvu aliyonayo Shetani.. yaani katika suala la nguvu basi Shetani kwetu ni dhaifu hawezi chochote  na ndio maana maandiko yanasema mtiini Mungu na mpigeni Shetani yaani unauwezo wa kumpinga shetani na ikawa lakini yeye hawezi kukupinga ikawa na akakushinda haiwezekani.

Nguvu ya Shetani ni ndogo sana ukiringanisha na ile tuliyonayo sisi.

Utajiuliza kivipi au kwa namna gani maandiko yameweka wazi.. Haleluya.

1 Yohana 4:17
“Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.”

Unaona hapo mwisho? Anasema “…. _kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo ulimwenguni humu.”_

_Maana yake tumefanana na yeye hakuwa anamaanisha kwa sura la! Bali kwa uwezo na mamlaka yaliyokuwa kwake Yesu ndio yaliyoko kwetu.. Haleluya_

Warumi 8:17
“na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

Maana yake ukuu na mamlaka yaliyokuwa katika Kristo temerithi na sisi vivyo hivyo kama Yesu Kristo (ni lazima ulielewe hili na uliamini ndani yako na litafakari kila siku likae moyoni mwako litakusaidia sana).

Maandiko yanasema…

2 Petro 1:3
“Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.”

Akimaanisha kuwa Mungu anaweza kutubadilisha na kutupa vitu vikuu ili tufanane na yeye na ndivyo ilivyo..

Unaweza ukajiuliza tumekirimiwa vitu gani?

Vipo vikuu vinne ambayo sitavielezea sana..

Tumekirimiwa/kupewa Yesu Kristo  ambapo pasipo yeye tusingepata ondoleo la dhambi wala uzima wa milele.. pia tumekirimiwa Roho Mtakatifu ambaye anatuongoza katika kweli yote na kutupa nguvu ya kuishi maisha matakatifu.  Lakini tumekirimiwa biblia ambayo hii ndio inatupa muongozo wote tunatakiwa tuishije na inatupa kalenda ya mwisho wa dunia hii. lakini tumekirimiwa kanisa.

Ambalo katika hili likidhirisha mwili wa Kristo na tunalindana na kujengana na kuonyana..

Mamlaka makubwa ndani yako maandiko bado yanasema…

1 Petro 2:9
“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;”

Una huduma ya upatanisho kama Yesu Kristo maana wewe ni kuhani wa Kifalme.. unaweza kuwaombea wengine rehema na wakasamehewa ķama Kristo alivyofaya pale msalabani.

Mamlaka uliyonayo ni kuu lakini kwa kushindwa kujua unakuwa na hofu ndani yako ya wachawi,waganga,mapepo, majini,kifo, vibwengo nk .

Lakini tuwatazame mitume je walikuwa na hofu ya vitu hivyo? La kwa sababu walifahamu wao ni wakina na nani.. yaani mamlaka waliokuwa nayo ni kubwa kiasi gani na wakaelewa namna ya kuitumia na kuleta matokeo chanya katika ulimwengu wote.

Unakuwa na wasiwasi kuwa utakuwa umerogwa, au una mikosi au roho ya kukataliwa nk.

Tangu lini mtu wa Mungu akarogwa au akawa na mikosi. na uganga/uchawi ukafanya kazi ndani yake? Au tunaliona hilo jambo katika maandiko sehemu gani?

Maandiko yanasema..

Hesabu 23:23
“Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!”

Ikiwa maandiko yanasema hapana uganga wala uchawi ya nini unapoteza Muda kupigana katika maombi kwa kuhisi umerogwa au umefungwa na wachawi?

Hatupigani na wachawi katika maombi hao tunawakemea tu kama jinsi mitume wanavyofanya maana kazi yao ni kuzuia injili na wala sio kukuroga wewe. Wakikuroga maana yake wamemroga pia Kristo ndani yako je inawezekana Kristo akarogwa? Jibu ni la!.

Maandiko yanasema…

Luka 10:19
“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

Anasema “..na nguvu zote za yule adui,..”
Umepewa nguvu ya kufukuza pepo,kuponya wagonjwa nk lakini je unaamini kuwa haya yote yako ndani yako??

Ukweli haya mambo si ya watu maalumu bali ni kwa wote. Bali ni kwa kila mtu aliemwamini Kristo Yesu. Ikiwa unataka kuona mamlaka hiyo ikidhirika kwako lazima ukubali kwanza iko ndani yako kisha anza kufanya haya. Kiri kuwa mamlaka hiyo iko ndani yako,kuwa muombaji, kuwa mtu wa kufunga ili urahisishe utendaji kazi wa nguvu za Mungu ndani yako.

Wahubirie watu injili, waombee, watamkie maneno ya baraka(maana kinywa chako ni tofauti na cha mpagani) neno unalotamka ni hai kabisa na itakuwa.. sikiliza sauti ya Mungu kwa kusoma neno,kusikiliza mahubiri na kisha itii.

Zaidi sana kiri wewe ni mshindi maana uko ndani ya alieushinda ulimwengu..hujazaliwa mara ya pili ili ushindwe bali ushinde. Baki na neno hili moyoni mwako na litendee kazi..

Maranatha.

Mawasiliano:0613079530
@Nuru ya Upendo.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *