
FUMBUA MACHO YAKO UONE
Biblia ilitabiri kuwa katika siku za mwisho watakuja watu wenye kudhihaki wakisema kurudi kwa Bwana YESU ni habari za kutunga tu, wanasema dunia hii itakuwepo milele, hakuna hukumu; lakini watu hawa biblia inasema “wanafumba macho yao wasione” wasione kuwa hii dunia iliwahi kuangamizwa kwa gharika na sasa imewekewa akiba kuangamizwa kwa moto!!, kumbuka hawajafumbwa na mtu au shetani bali wao wenyewe wanafumba makusudi, kwa lugha rahisi tunaweza kusema wanajitoa ufahamu. Tunasoma..
2Petro 3:1 “Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,
[2]mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.
[3]Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,
[4]na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.
[5] MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
[6]kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.
[7]Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.”
Kufumba macho maana yake ni kujua ukweli lakini unajifanya kama hujui!
Watu wengi wanajua kabisa wanayoyafanya gizani ni mambo ambayo yatawapeleka jehanumu lakini wanafumba macho wasione..ndio maana wanaendelea kufanya.
Umesikia na umejua kuwa waasherati, wazinzi, waabuduo sanamu, wafiraji, walawiti, wezi, walevi, watukanaji, wachawi, wala rushwa, wafisadi, na watendao mambo jinsi hiyo na yanayofanana na hayo hawataurithi ufalme wa Mungu sawa sawa na Wagalatia 5:19, lakini bado unaendelea na mambo hayo, huko ndiko kufumba macho..unajitoa ufahamu.
Na neno la Nabii Isaya litatimia kwako, likisema..
“Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona”.
Mathayo 13:15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, NA MACHO YAO WAMEYAFUMBA; WASIJE WAKAONA kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.”
Umesikia na umefahamu kabisa mwanamke kuvaa suruali na nguo za kubana ni machukizo kwa Mungu (kumb.22:5), lakini bado hutaki kuacha kuvaa mavazi hayo ya kikahaba, Neno la Mungu linakuambia vaa kwa kujistiri (1Timotheo2:9), lakini bado unaendelea kuvaa vimini vyako, Neno linakuambia..
“Kujipamba kwenu KUSIWE kwa nje” (1Petro3:3) lakini bado unajipodoa, unasuka, unavaa mahereni, kucha bandia, unapaka wanja na kupamba kichwa kama Yezebeli mama wa makahaba (2Wafalme9:30), unafumba macho ili uende kuzimu mzima mzima.
Unatazama picha chafu/pornography, unapiga punyeto/unajichua, unasikiliza miziki za kidunia, movies, mipira, una beti, unacheza magemu ya kipepo na umehubiriwa na kujulishwa kuwa njia hiyo itakupeleka jehanumu, lakini UNAFUMBA MACHO, hutaki kuelewa.
Lakini Bwana anakusihii tena leo FUMBUA MACHO YAKO uokoke na jehanamu ya moto.
Watu wengi wanafahamu kabisa kuwa hizi ni siku za mwisho na Dalili zote zinaonyesha kuwa Kristo yupo mlangoni, lakini wanafumba macho yao wasione!
Kitendo cha kuendelea kuishi katika dhambi na huku umesikia injili ni kufumba macho.
Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.”
Hebu leo fumbua macho yako Kristo akuokoe.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.