Funga kutafuta njia iliyonyooka.

Maombi na sala No Comments

Funga kutafuta njia iliyonyooka.

Ezra 8:21 “Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote”.

Jina la Bwana YESU litukuzwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu. leo kwa neema za Mungu tutajifunza tena umuhimu wa kuomba na kufunga.

Kitendo cha kufunga hakikwepeki sasa kwa mkristo yeyote.

Lakini pia ni vizuri kufahamu kuwa hatufungi ili Mungu atusikie au atujibu maombi yetu, Mungu hasubiri kwanza tuteseke ndio atusikie hapana kwani alishaweka wazi katika Neno lake, kuwa yeye anajua tunachohitaji kabla hata hatujamwomba (Mathayo 6:8)…Lakini pamoja na hayo Kufunga kunasaidia kuongeza uwezekano wa wewe kupata majibu ya maombi yako au kupata unachokitafuta kwa haraka tofuati na yule asiyefunga. Ni sawa tu na mwanafunzi anayesomea maktaba na Yule anayesomea nyumbani, anayesomea maktaba anaongeza uwezekano mkubwa wa kufaulu mitihani kuliko Yule anayesomea nyumbani, kwasababu kule maktaba kunakuwa na utulivu mkubwa na mazingira mazuri ya kujisomea kuliko nyumbani..Lakini hiyo haimfanyi afaulu mtihani moja kwa moja Yule wa nyumbani anaweza kufanya vizuri kushinda hata yeye..Lakini itampasa awe mtu wa kujitambua sana.

Vivyo hivyo na katika kufunga, Mtu mwenye desturi ya kuomba kwa kufunga anajijengea daraja zuri la yeye kuwasiliana na Mungu kuliko Yule apelekaye dua zake kwa Mungu bila kufunga, Kwasababu Kufunga kunampa utulivu Fulani wa Roho tofauti na mtu asiyefunga.

Na tunaposema kufunga hatulengi tu ile kuacha kula hapana, unafunga pia na mambo mengine yanayoweza kukusonga usiisikie sauti ya Mungu.

Ufunuo wowote Mungu anaompa mwanadamu, hampi akiwa katika mazingira ya usumbufu wa akili, Usijidanganye kuwa Mungu atakupa ufunuo wowote katika hali ya masumbufu, kama utaisoma biblia na huku unasikiliza miziki ya kidunia, au huku una chat, au huku unafanya mambo mengine, Ni heri uifunge uje usome baadaye usiku peke yako…. inahitaji utulivu wa fikra na mawazo..Na hapo ndipo inakupasa ufunge baadhi ya vitu unavyovifanya, au ulivyozoea kuvifanya..Na kwa jinsi unavyovifunga kwa muda mrefu zaidi ndivyo unavyoongezeka uwezekano wa Mungu kusema na wewe kwa haraka na kwa mara nyingi zaidi.

~Je! Unaona hali yako ya kiroho haiendi sawa, hauoni furaha ya wokovu, hauna amani n.k suluhisho ni kufunga na kuomba.

~Unataka njia zako zinyooke kwa Bwana usiache kufunga na kuomba.

~Unataka njia iliyonyooka katika familia yako na watoto wako funga na kuomba ili usikie sauti ya Mungu.

~Unataka njia iliyonyooka katika Elimu yako, mtafute Mungu kwa njia hii KUFUNGA NA KUOMBA.

Je! Umempokea Yesu?

Kumbuka kama hujampokea Yesu, yaani haujaokoka kikamilifu. Fahamu kuwa Elimu yako, kazi yako, mali zako, afya yako, sadaka zako, kufunga kwako, vyote hivyo ni bure. Kwasababu itakufaidia nini ukiwanavyo halafu mwisho ukakosa mbingu ukaenda jehanumu.

Ni heri umpokee Yesu leo ipasavyo ili upate kwanza uzima wa milele na hayo mengine yatafuata.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *