HATARI YA KIU BAADA KUKOSA MAJI YA UZIMA
Shalom: Nakusalimu kwa jina kuu lipitalo majina yote..jina la Bwana Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.
Na leo tutaangalia hatari ya kupatwa na kiu ya kukosa maji ya uzima, yapo maji ya kawaida na pia yapo maji ya uzima ambayo Bwana alisema “yeyote atakayekunywa maji hayo hataona kiu milele” (Yohana 4:14). Sasa kabla hatujaangalia hatari ya kiu ya kukosa hayo maji ya uzima..hebu tuangalie kiu ya kukosa maji ya kawaida.
Asilimia kubwa zaidi ya 60 ya uzito wa miili yetu ni maji, hivyo mtu akikosa maji kwa muda mrefu na huku anatumia chakula kikavu..kuna uwezekano akapatwa na hatari ya kiu. Na hatari ya kiu ni mtu yule kuishia kunywa maji machafu au hata vimiminika vyenye sumu, kama umewahi kupatwa na kiu bila shaka utakuwa unaelewa vizuri hatari ya kiu, ni heri uumwe na njaa ya kukosa chakula kuliko kiu ya kukosa maji japokuwa vyote vina umuhimu.
Sasa katika biblia.. maandiko yalitabiri kuwa siku za mwisho kutakuwa na njaa na kiu ya watu kukosa maji ya Uzima (Neno la Mungu).
Amosi 8:11-13 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA.
[12]Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione.
[13]Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.
Umeona hapo njaa na kiu iliyopo sasahivi ni kubwa sana, na ili tuweze kuhakiki hili vizuri..hebu tuendelee kuangalia hatari ya njaa na kiu ya mwilini.
Sikuzote ili kujipima kama upo katika njaa au haupo, ni uwezo wa kutambua ubora wa chakula unachokula, jaribu kufanya uchunguzi kaa siku mbili bila kula usiku na mchana halafu uletewe maharage ya juzi uambiwe ule, nakuambia utauona ni mtamu kweli, lakini subiri njaa ile iwe imeshapoa halafu uletewe maharage yale yale ule, moja kwa moja utaanza kuona kasoro nyingi zilizopo katika yale maharage ambazo hapo mwanzo hukuziona, pengine utasema maharage gani haya hayana ladha, hajaungwa vizuri kwanza yamechacha, na yamezidi chumvi hayafai kuliwa yataniletea kiungulia..
Husemi hivyo kwasababu ya dharau ya shibe hapana lakini unazungumza ukweli wake kuwa sio bora, Sasa hapo ni kwasababu ile Njaa mwanzoni ilikudanganya hata kwa vitu visivyokuwa na manufaa kwa mwili wako kuviona vinafaa. Biblia inasema:
Mithali 27:7 “Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.”
Na hata kiu pia ni hivyo hivyo, ukikosa maji ukaumwa na kiu ile ya kukaukiwa kabisa, nakuambia hata ukipata maji ya matope, au yale ya barabarani yanayochafuliwa na magari utakunywa bila kuuliuliza, hata kama kwa nje yanaonekana kabisa kuwa na uchafu.. wakati huo hautaona huo uchafu..hiyo ni kwasababu ya ile kiu.
Ndivyo ilivyo katika hizi siku ambazo kila mtu anajua kuwa ni za mwisho, Mungu alisema ataleta njaa duniani kote, si njaa ya kukosa chakula cha kimwili, bali njaa ya watu kukosa kuyasikia maneno yake..Na kiu ya watu kukosa maji ya uzima.
Sababu hiyo basi kiu hiyo na njaa inawatafuna watu leo hii kiasi cha kufikia hatua ya kuoana hata yale mafundisho manyonge kuwa ni yenye nguvu..yale mafundisho ya uongo kuwa ni ya kweli.
Kila ufunuo, kila unabii unaokuja hata kama haumjengi mtu, basi utapokelewa tu kwa moyo wote,na watu wanashukuru Mungu kwa huo, hiyo yote ni kwasababu ya njaa. Hata mtu akisema mimi ni YESU au Mungu, huku akitoa maandiko yake machache yanayothibitisha anachokisimamia bado watu wataona ni Neno la Mungu lililo hai …Kusingekuwa na njaa, manabii wa uongo na waalimu wa uongo wasingepata sehemu ya kupelekea mafundisho yao manyonge, lakini kwasababu uhitaji upo mkubwa hata vile feki navyo vinapata soko..kama tu vile simu za kichina.
Ndugu, leo unayadharau hichi chakula cha kweli na haya maji ya uzima ambayo unayapata bure kila siku, hii ni kwasababu bado hujapatwa na njaa na kiu ambayo inawapata wengine, ni vizuri ufahamu kuwa injili ya kweli haipatikani kila mahali..tambua kuwa ni neema ya Mungu wewe kufikiwa na injili hii ambayo inakurudisha kwenye wokovu wa kweli.
Upo wakati ambao utapatwa na kiu kali..utatamani upate hata tone ya haya maji ya uzima ambayo unayachezea sasa, lakini wakati huo utatafuta hata tone usipate.
Kumbuka Bwana alipokuwa amesimama katikati ya makutano ya watu wengi akipaza sauti yake kwa nguvu nyingi sana na kwa bidii kuwaambia watu waende kwake wanywe MAJI YA UZIMA yanayotoka kwake hakuwa anatania au anasema mambo ambayo hayana maana sana katika maisha ya mtu, hapana ndugu yangu, Alijua kabisa upo wakati roho za watu zitalia na kuugua kusikoweza kunenwa zikitafuta walau hata tone moja tu ya hayo maji wasilipate…Embu sikiliza Bwana Yesu alivyopaza sauti yake kwa bidii kuwasii watu katikati ya makutano siku ile kwenye sikukuu..
Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, MTU AKIONA KIU, NA AJE KWANGU ANYWE.
38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, MITO YA MAJI YALIYO HAI ITATOKA NDANI YAKE.
Sasa kumbuka haya maji faida yake sio kukupa uzima wa roho yako hapa duniani tu, hapana bali hii inaendelea hata baada ya kufa, lakini watu ambao hawajataka kuyanywa haya Maji sasa hivi, wakati yanapatikana kwa wingi na bure, utafika wakati karibia na kufa au baada ya kufa watatambua umuhimu wa haya maji, na pale watakapoyatafuta watayakosa..wakizitazama roho zao zinaenda kufa kwa kukosa maji, watahangaika kwa namna isiyoelezeka wakiyatafuta hayo maji ya uzima wasiyapate…Ndio tunarudi kwenye ule mfano wa Lazaro Bwana Yesu alioutoa katika..
Luka 16:19 “Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.
20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,
21 naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.
22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro ACHOVYE NCHA YA KIDOLE CHAKE MAJINI, AUBURUDISHE ULIMI WANGU; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.
31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”.
Tukisoma habari hiyo, tunaona kabisa wakati unaozungumziwa hapo ni wakati ambao watu wanaishi duniani na wengine wapo katika upande wa pili; aidha kuzimu au mahali pa starehe, Ni wazi kuwa mtu anapokufa bado anaendelea kuishi, mwili wake unabaki hapa hapa duniani lakini roho yake inaendelea kuishi mahali Fulani.
Sasa moja ya jambo liliokuwa linamtesa yule tajiri kule kuzimu ni KIU.. Hakuwa na kiu ya maji haya ya kisimani, kwasababu kule kuzimu mwili haupo alishauacha makaburini..na kama tunavyojua roho hauhitaji haya maji na chakula cha mwili. Kwahiyo huyo tajiri alikuwa na KIU YA MAJI YA UZIMA YAUPAO ROHO YAKE UZIMA. Alitamani apate walau tone moja la yale maji, apate uzima kidogo wa roho yake utakaomfanya angalau aishi kidogo, lakini hakupata,.. Alitamani apate nafasi ya pili ya kutubu dhambi zake, ili apate uzima lakini alikuwa ameshachelewa, alitamani abatizwe akitumaini hata siku ile atakayohukumiwa apate neema lakini alishachelewa, alitamani hata afanye ushirika na wakristo lakini muda ulishapita, alitamani akawashuhudie wengine habari njema lakini mlango ulikuwa umefungwa n.k.
Alipokuwa duniani aliikata ile KIU ya kutafuta UZIMA kwa mambo mengine, kwasababu ya utajiri wake akaikata kwa mali akiamini kuwa mali zinaweza kumpa uzima badala ya YESU KRISTO, hatuoni hata watu leo hii wakisema ukipata pesa umepata kila kitu,? Hawajui ya kwamba pesa haimpi mtu uzima, isipokuwa yale maji yanayotoka kwa Bwana YESU mwenyewe. Utajiri wa AFYA ulimdanganya akidhani kuwa afya yake itadumu, kwa lishe bora aliyokuwa akiizingatia na kwa wingi wa matabibu aliokuwa nao hakuna haja ya kumtafuta mwingine wa kumpa uzima, hao wanatosha kukata kiu yake..
Kwa wingi wa ANASA alizozitumainia, akaona zinatosha kumpa amani na furaha na raha, hivyo akapuuzia Amani idumuyo inayotoka kwa Bwana. Utajiri wake wa mambo yote, marafiki, ndugu, jamii, mali, afya, n.k. hakuna hata moja baada ya kufa vilifanikiwa kukatisha KIU iliyokuwa ndani yake..Jambo hilo alikuja kulingundua baada ya kufa.Na ndio maana hapo analia akitaka TONE moja tu la MAJI YA UZIMA.? Ndugu HAYO MAJI yalivyo na thamani kubwa baada ya kufa…Utatamani tone moja tu utakosa.
Leo hii unaweza kuona mtu baada ya kupatwa na mabaya, aidha kaambiwa na madaktari ugonjwa alionao anao mwezi mmoja tu wa kuishi, utaona mtu huyo kama alikuwa sio mkristo anaanza kuhangaika kumtafuta Mungu, lakini hapo kwanza wakati ni mzima alikuwa anaudhihaki wokovu,..Sasa hiyo ndio dalili ya ile KIU HALISI inaanza kuja ndani yake, hapo ndio unaanza kuona mtu anamtafuta mchungaji, anapigia watumishi simu wamuombee, au wamuhubiri n.k.. Sasa akishakufa katika dhambi zake, huko anakokwenda hiyo KIU inajizidisha mara nyingi sana zisizoweza kuelezeka ndipo majuto yasiyokuwa ya kawaida yatamjia.
Hivyo ndugu kumbuka usifanye makosa kujiona ni TAJIRI na kuyadharau MAJI YA UZIMA kwasababu afya yako ni nzuri, au una mali ya kukutosha, au familia nzuri, au una ulinzi, n.k. hayo yote ipo siku yataondoka lakini KIU itabaki pale pale isipoikata leo hii, hautaweza kuikata kule..Usipumbazike na mambo ya ulimwengu huu yanayopita yakakupa kiburi kwamba Kristo hana faida yoyote katika maisha yako..
Na haya ndiyo Maneno aliyomalizia Bwana YESU katika kitabu cha biblia:
Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.
17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! NAYE MWENYE KIU NA AJE; NA YEYE ATAKAYE, NA AYATWAE MAJI YA UZIMA BURE.”
Tubu ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, na uuishie utakatifu angali muda upo.
Ubarikiwe.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.