Huwezi kutoa kitu kisafi katika kitu kichafu.

Biblia kwa kina No Comments

Huwezi kutoa kitu kisafi katika kitu kichafu.

Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe milele. Karibu tujifunze biblia Neno la Mungu.

Kuna mambo ambayo bila kufuata kanuni fulani hatoweza kupata. Mfano mwanafunzi akitaka kufaulu mtihani hana budi kusoma kwa bidii sana hiyo ndio kanuni, lakini akiingia kwenye chumba cha mtihani, huku hajasoma kabisa ni wazi ataambulia tu kufeli kwasababu hajafuata kanuni.

Halikadhalika mkulima akitaka kupata mazao mengi shambani ni lazima afuate kanuni bora za kilimo mfano kuwa na mbegu bora, kuandaa shamba, kuwa na mbolea , kupalilia n.k kinyume na hapo ataambulia kupata mazao kidogo au asipate kabisa. Vivyo hivyo na mambo mengine yote ikiwemo ya rohoni yana kanuni zake.

Lakini leo nataka tuangalie kanuni za kupata utakatifu kwasababu biblia imetuambia pasipo huo hatuwezi kumuona Mungu (Waebrania 12:14).

Misemo mingi zimeibuka katika siku hizi za mwisho juu ya swala hili la utakatifu. Wengine wanasema tunaishi katika neema, wengine wanasema Mungu haangalii mwili anatazama roho.

Lakini leo nataka niseme na wewe uliye na huo mtazamo kwamba Mungu anaangalia moyo haangalii mwili. Nataka nikuakikishie kwa Neno la Mungu kuwa huo moyo ambao unasema Mungu anaangalia… fahamu kuwa kama moyo wako sio safi, kamwe usidhani mwili wako unaweza kuwa safi. Kile unachokifanya nje ni matokea ya yale uliyoyajaza ndani ya moyo wako. Uchafu unaofanya katika mwili wako ikiwemo kujipodoa, kuvaa mavazi ya kizinzi umeanzia ndani ya moyo wako.

Huko ndiko ulikoanzia kutengeneza mawazo ya kuvaa mavazi hayo kwasababu zako, huko ndiko ulikoanzia kutamani kujipamba ili uonekane.

Marko 7:20 “Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

[21]Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

[22]wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

[23]Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

Kwahiyo acha kujidanganya kuwa Mungu anaangalia moyo wakati moyo wako umejaa tamaa mbaya na mawazo mabaya, Mungu hawezi kutazama moyo mchafu namna hiyo.

Ili mwili wako uwe safi huna budi kusafisha ndani yako kwanza, ndivyo hata mwili wako utakuwa safi pia..hiyo ndio kanuni.

Mathayo 23:26 Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.

Hata macho yako ya ndani yasipotakasika, macho yako ya nje nayo hayawezi kuwa safi

Mathayo 6:22 “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.

[23]Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!

Ndio maana huoni shida kutazama picha chafu, huoni shida kutazama filamu zenye maudhui ya uasherati, hauoni shida kusikiliza miziki ya kidunia iliyojaa maudhui ya uzinzi..ni kwasababu macho yako ya ndani na masikio yako ni mabovu hivyo mwili wako wote ni giza.

Ndani yako ikiwa safi, nje pia itakuwa safi. Huwezi kutoa kitu kisafi katika kitu kichafu. (Hiyo ni kanuni)

Ayubu 14:4 “Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye”.

Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu hauwezi kuzaa matunda mazuri hiyo ni kanuni (Mathayo 7:18)

Kwahiyo Kaka/Dada unayechafua mwili wako kwa kuweka vitu bandia ambavyo Mungu hajakuumbia navyo, kwa kigezo kuwa Mungu haangalii nje anaangalia ndani, fahamu kuwa ndani yako ni vivyo hivyo kama nje ilivyo. hayo mapambo uliyoweka masikioni mwako, mdomoni mwako, kichwani, usoni, ndiyo yaliyojaa ndani yako. Hivyo anza kusafisha moyo wako ili mwili wako uwe safi.

Na kanuni ya kusafisha moyo ni kwa kutubu kwa kumaanisha kabisa kujikana na kwenda kubatizwa kwa jina la Yesu na kwa Roho Matakatifu. (Matendo 2:38).

Kumbuka utakatifu ni wa nje na ndani na haiwezekani kuwa na upande mmoja kama vile isivyowezekana muembe kutoa machungwa.

2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *