IKIMBIENI ZINAA
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu libarikiwe.
Karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu.
Neno la Mungu linatuelekeza TUKIMBIE ZINAA na wala sio tukemee au tuiombee, maana yake kabla ya kuomba na kuombewa kwa habari ya maroho ya zinaa, ni sisi kwanza tunapaswa tukimbie kabisa kwa miguu yetu mbali na hiyo dhambi inayowapeleka wengi kuzimu.
1Wakorintho 6:18 IKIMBIENI ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.
Sababu ya watu wengi kuanguka kwenye hii dhambi ya zinaa, ni wao wenyewe kuruhusu mazingira yanayochawishi kutendeka kwa jambo hilo, na baada ya hapo.. wanabaki kumtupia shetani lawama kwamba ni yeye ndiye chanzo.…lakini kumbe ni wao..Shetani, anachokifanya yeye ni kupalilia tu hiyo njia ya hiyo dhambi, ndio maana biblia inasema “mtu anayefanya zinaa anatenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe” maana yake ni yeye mwenyewe kakusudia kutenda jambo hilo baya juu mwili wake na wala hajapitiwa na sio shetani ni yeye mwenyewe.
Kwahiyo mtu anayekwenda kufanya uasherati leo, ni yeye mwenyewe amechagua uovu kwa ushawishi wa nguvu za shetani…zingati hili (Ni huyo mtu kafanya na sio shetani kafanya kwa niaba yake)…Kwahiyo hapo anayestahili kulaumiwa wa kwanza ni huyo mtu, kwasababu kachagua kufanya mabaya…
Ni sawa leo uende sokoni kununua nguo, ukute maduka mawili mbele yako, moja linauza nguo nyeupe lingine jeusi…na ndani kila mmoja anakushawishi ununue kwenye duka lake…maamuzi ya mwisho yanatoka kwako wewe, na sio kwa mwenye duka…hapo kama utachagua nyeusi au nyeupe na kwenda nyumbani kukuta kasoro, hapo anayestahili kulaumiwa wa kwanza sio muuzaji bali ni wewe ambaye ulikwenda kuchagua…ulipaswa ukague nguo yote kwa makini kabla ya kuinunua, sio kusikiliza tu maneno ya wauzaji na kuamini!
Na ndivyo ilivyo sasa hivi duniani kuna maduka mawili, moja linauza mavazi meupe(ya uzima wa milele), na lingine meusi ni jukumu lako wewe kuchagua lipi linakufaa…kila moja lina watu ndani yake wanaokushawishi na kukuvutia, maamuzi ya mwisho unatoa wewe..sio muuzaji!…Muuzaji anakazi tu ya kukudalalia basi! Mambo mengine unafanya wewe, uchaguzi unafanya wewe na gharama unaingia wewe.
Leo utasikia mtu anakwenda kuzini, halafu anakwambia ni shetani kafanya vile, atakuambia shetani kanipitia tu!… hajakupitia ndugu ni wewe umechagua mwenyewe uovu, kwa kukubali ushawishi wake…Kama ingekuwa ni shetani, basi Mungu asingesema “siku ile kila mtu atasimama mbele ya kiti cha hukumu kutoa hesabu ya mambo yake”…asingesema hivyo, badala yake angesema “shetani atasimama kueleza ni kwanini kawaingia watu na kuwalazimisha wafanye dhambi”…Lakini siku ile kila mtu atahukumiwa kwa aliyoyatenda…kwanini? kwasababu si shetani aliwalazimisha watu kutenda, bali ni watu kwa uchaguzi wao wenyewe walichagua uasi…
Yohana 3: 19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”.
Kwahiyo mtu yeyote anayefanya zinaa, ni kakusudia kufanya kwa idhini yake mwenyewe baada ya kuzidiwa na ushawishi wa shetani kufanya hilo jambo..na atahukumiwa yeye peke yake kwasababu alikusudia..sio bahati mbaya.
Ndio maana katika Agano la kale Mungu alitoa sheria hii, hebu tusome hii habari…
Kumbukumbu la Torati 22:23-27 Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye;
[24]watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa HAKUPIGA UKELELE, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
[25]Lakini yule mtu mume kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee;
[26]lakini yule kijana usimfanye neno; hana dhambi yule kijana ipasayo kuuawa, kwa kuwa ni mfano wa mtu kumwondokea mwenzake akamwua, ni vivyo lilivyo jambo hili;
[27]kwani alimkuta kondeni; yule kijana aliyeposwa akalia, pasiwe na mtu wa kumwokoa.
Hapo mstari wa 24 anasema “huyo kijana afe kwa kupigwa mawe kwasababu alikutwa ndani ya mji lakini HAKUPIGA KELELE ili apate msaada, na mjini kuna watu wengi asingekosa kusaidiwa, lakini yule mwingine alikutwa jangwani akapiga kelele asipate msaada” umeona..huyo wa kwanza alikusudia kutenda jambo hilo.
Na ndivyo, hata sasa hali za watu wengi ilivyo, utamkuta kijana yupo na girl friend/boyfriend na wote wanaishi nyumba moja, wanakutana porini wenyewe, wanaishi kama mke na mume.. halafu wanatarajia wasiangukie kwenye zinaa!! Na baada ya kufanya huo uchafu wanasema wamepitiwa au wanamsingizia shetani.
Kaka/Dada biblia inasema ikimbieni zinaa, unaelewa maana ya KUKIMBIA?
Kukimbia maana yake ni kuondoka bila HIARI ya hiyo dhambi. Maana yake ni kwamba kama ulikuwa unaishi na mwanamke/mwanamume ambaye mnafanya naye uasherati ni KUMKIMBIA GHAFLA! Na Kukata mazoea!…Akikutafuta kwenye simu mwambie mara moja tu kwamba umeokoka na hivyo tunapaswa tutubu kwa yote tuliyokuwa tunayatenda na kumrudia Mungu. Ukiona hakuelewi wewe jiokoe nafsi yako usitazame nyuma wala usiwe na huruma, usipokee simu zake, …Usianze kushauriana naye huku bado mnakutana kutana na kuzungumza zungumza, akikutafuta kwenye simu usijibu meseji yake hata moja, hata akilia kwa machozi ya damu kwamba mrudiane usiwe na huruma jiokoe nafsi yako na yake, kwa kuukimbia zinaa ikiwezekana block hiyo namba …Usizungumze naye hata kidogo. Mfano wa Yusufu. Mke wa Potifa alimtamani na Yusufu baada ya kulijua hilo, aliacha kuongea na mke wa Potifa..
Mwanzo 39:10 “Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye”.
Utasemaje unataka kuacha uzinzi na bado unaongea na unajibu meseji za watu unaozini nao?..utasemaje unataka kuacha uasherati na huku unamazoea zoea na wanawake wa mtaani na wanaume wa mtaani?, na huku bado unafuatilia vitamthilia na vi-movie vya kipepo vyenye maudhui ya kizinzi ndani yake kwenye Tv yako vinavyochochea uzinzi tu na wala si kitu kingine?..utasemaje unataka kuacha kutazama picha za ngono na huku kwenye simu yako bado zipo?, bado umejiunga whatsapp na facebook makundi ya mambo hayo?, utasemaje unatamani kuacha zinaa na wakati ndani ya begi lako kuna nguo za kizinzi, ndani mwako kuna picha za wanaume unaozini nao? Na dhambi nyingine zote ni hivyo hivyo…dawa ya kuziacha ni KUZIKIMBIA!!…Ondoka! Dhambi nyingine ili uweze kuziepuka zinakugharimu kuhama hata hapo ulipo, hama hata mtaa..hamia mwingine.. ondoa vyanzo vyote vya hiyo dhambi. Hizo ndio gharama za kuacha dhambi!..
Usipotaka kuzikimbia namna hiyo na kutafuta kuombewa, au kuwekewa mikono, kirahisi rahisi tu hivyo…Utajikuta unaombewa na kila mtu na hata kuwekewa maroho mengine mabaya hata kuliko hayo uliyonayo sasa. Hali yako kila siku itazidi kuwa mbaya kwasababu umekosa maarifa ya kutosha!.
Dhambi ya zinaa ambayo ndani yake inajumuisha uasherati, uzinzi, ulawiti, ufiraji, na usagaji na hata utazamaji wa picha chafu za ngono na kujichua, na masturbation…Dhambi hii haimtoki mtu kwa Kuombewa!!..Usimfuate mtumishi wa Mungu na kumwambia niombee niache dhambi hii au dhambi ile..Hakuna maombi ya namna hiyo!..Nakuambia hivyo kwasababu na sisi wengine tulikuwa namna hiyo hiyo..tukadhani kuombewa ndio suluhisho..tukafunga muda mrefu na kujiombea na hakuna kilichobadilika ndani yetu, mpaka tulipoyasoma maandiko, tukaifahamu kweli nayo hiyo kweli ikatuweka huru. Hivyo ndugu mpendwa usipoteze muda kufanya utafiti ambao tayari umeshasaidiwa kuufanya utazunguka na kuzunguka na mwisho wa siku utarudi pale pale.
Suluhisho la kuacha dhambi ya uasherati na zinaa kwa ujumla ni KUUKIMBIA!. Kumbuka Neno hili..
Mithali 26:20 “Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.”
Ndugu umeyasikia/umeyasoma haya..hutasema siku ile hukuambiwa…kama utamtii Roho Mtakatifu leo, basi yeye mwenyewe atahakikisha anakusaidia kuyatimiza maazimio yako..lakini pia kama hutatii uamuzi ni wako. Lakini natumaini utatii, na Bwana akusaidie.
Hivyo kama hujaokoka au kama wewe ni vuguvugu, upo hatarini kutapikwa hivyo kabla hujatapikwa hebu fanya mageuzi haraka..Mtii leo Roho Mtakatifu kwa kuacha dhambi kwa Lazima.. baada ya kuziacha, nenda katafute ubatizo sahihi wa kuzama mwili wote katika maji na kwa jina la Bwana Yesu kulingana na Matendo 2:38, na Yule Roho Mtakatifu ambaye aliishaianza kazi njema moyoni mwako atakusaidia kufanya yale ambayo peke yako ilikuwa ni ngumu kuyatimiza, na dhambi kwako itakuwa sio kitu kigumu kukishinda kwasababu Nira ya Kristo siku zote ni laini na utapata furaha, na amani isiyoelezeka, na utaona siku zote ulikuwa wapi kuingia ndani ya Kristo…kwa raha utakayoipata na furaha..wala dhambi haitakuwa ni kitu kinachokusisimua hata kidogo.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.