Iweke sadaka yako juu ya mwamba halisi.

Biblia kwa kina No Comments

Iweke sadaka yako juu ya mwamba halisi.

Shalom mtu wa Mungu.. Bwana Yesu Kristo asifiwe. Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema ya kuendelea kuona jua lake.. utukufu na heshima ni zake milele.

Karibu tujifunze Neno lake ambalo ni mwanga wa njia zetu. Na siku ya leo tutajifunza somo linalohusu sadaka, ikiwa utahitaji kufahamu zaidi kuhusu maana ya sadaka, aina za sadaka mbali mbali katika biblia,  umuhimu wa kutoa sadaka, na jinsi sadaka inavyotenda kazi..na maswali mengi hayusuyo sadaka, basi tembelea tovuti zetu utakutana na masomo mengi yanayohusu sadaka au unaweza ukatutafuta inbox kwa namba zilizoko chini ya makala hii nasi tutakusaidia.

Basi siku ya leo tutajifunza umuhimu wa kuweka sadaka juu ya mwamba halisi, tunaweza tukawa tunatoa sadaka lakini hatuoni matokeo.. kwasababu huwenda hatuweki mahali sahihi panapopaswa. Na biblia inasema…

Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;

[14]bali katika mahali atakapopachagua BWANA…” (Kumb12:13-14)

Sadaka sio matoleo kwamba unaweza ukatoa mahali popote upaonapo wewe.. mfano ukatoa barabarani kwa maskini, au ukaenda kwenye vituo vya yatima ukatoa … kufanya hivyo ni sawa kabisa na kuna baraka za Mungu ukifanya hivyo.. Lakini hiyo haitwi tena sadaka bali itabaki kuwa matoleo au changizo, Ili iitwe sadaka ni lazima itolewe mahali maalumu iliyochaguliwa na Mungu..na mahali hapo panaitwa madhabahuni pa Bwana..ndio maana Bwana aliwakemea wale viongozi vipofu akiwaambia..

Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.

[17]Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?

[18]Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga.

[19]Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka?” (Mathayo 23:16-19),

Hii inatuonyesha kuwa kuna mahusiano kati ya sadaka na madhabahu..hivyo ni lazima sadaka ipelekwe madhabahuni vinginevyo itakuwa ni kitu kingine na sio madhabahu tu ilimradi madhabahu, hapana, ni madhabahu iyojengwa juu ya mwamba imara.

Gideoni alipotokewa na malaika wa Mungu, Bwana alimpa maelekezo ya namna ya kutoa sadaka ile, kwamba aweke juu ya mwamba na ndipo baada ya kufanya hivyo alimuona Bwana uso kwa uso.

Waamuzi 6:19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa.

[20]Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, UIWEKE JUU YA MWAMBA HUU, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo.

[21]Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake.

[22]Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso.

[23]BWANA akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa.

Na sio Gideoni tu alifanya hivyo, hebu tumwangalie mtu mwingine..

Waamuzi 13:15 Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.

[16]Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea BWANA. KWA KUWA MANOA HAKUJUA YA KWAMBA YEYE NI MALAIKA WA BWANA.

[17]Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?

[18]Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?

[19]Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, AKAMTOLEA BWANA HAPO JUU YA MWAMBA; HUYO MALAIKA AKATENDA LA AJABU; Manoa na mkewe wakaangalia.

[20]Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.

[21]Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. NDIPO MANOA ALIPOJUA YA KWAMBA NDIYE MALAIKA WA BWANA. (Haleluya)

Sasa, hao ni mfano tu watu wachache.. lakini wapo wengi sana, kwa ujumla sadaka nyingi katika Agano la kale zilitolewa juu ya mwamba. Hivyo ukitaka kumuona Mungu uso kwa uso kama Gideoni kanuni ni kutoa sadaka juu ya mwamba (kumbuka kumuona Bwana uso kwa uso ni kumfahamu zaidi), ukitaka kutendewa maajabu kila siku..toa sadaka juu ya mwamba halisi.

Na katika Agano jipya, mwamba wetu si mwingine zaidi ya Yesu Kristo Mungu mwenye nguvu. Biblia inasema hivyo.

1 Wakorintho 10:1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

[2]wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

[3]wote wakala chakula kile kile cha roho;

[4]wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; KWA MAANA WALIUNYWEA MWAMBA WA ROHO ULIOWAFUATA; NA MWAMBA ULE ULIKUWA NI KRISTO.

Hakikisha sadaka zako unazitoa juu ya madhabahu ya Yesu Kristo ili sizae matunda yaliyokusudiwa, na madhabahu ya Yesu Kristo ni ile ambayo imejengwa juu ya msingi wa mitume wake..ikiwa na maana kwamba madhabahu yoyote isiyohusisha mafundisho ya Mitume wa Bwana Yesu..hiyo madhabahu haijajengwa juu ya mwamba halisi bali imejengwa juu ya msingi wa mitume wa ibilisi…hata kama inaonekana kwa nje ni halisi.

Na mafundisho ya mitume ni yale yanayosisitiza kutubu dhambi na kubatizwa kwa jina la Yesu aliye mwamba halisi..na mengine mengi ambayo yanamfanya mtu awe mtakatifu na aulekeze moyo wake katika ufalme wa mbinguni na sio hapa duniani, kinyume na hapo mafundisho mengine ni ya ibilisi.

Je! sadaka zako unazitoa wapi? Kumbuka Bwana amesema “Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;”

Na sadaka ya kwanza anayoikubali Mungu ni moyo wako, hii ikiwa na maana kama moyo wako haupo kwake.. basi sadaka zako huwenda zikawa hazimfikii yeye na hivyo kutoa kwako ikawa ni bure tu hata kama unatoa nyingi kiasi gani!

Moyo ulioelekea kwa Mungu ni ule ambao upo tayari kutii kila Neno litokalo katika kinywa cha Bwana, ni ule ambao upo tayari kutoa pasipo sharti, ni ule ambao una rehema kwa wengine, moyo ulio mnyoofu ndio Bwana anautaka na ndio anaungalia pale unapotoa sadaka zako.

Je umempokea Yesu? Je Unafahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho na Yesu yupo mlangoni kurudi?

Je Unafahamu ni nini kitakutokea pale utakapokosa mbingu?

Hebu leo fanya maamuzi sahihi ya kumpokea Yesu kama bado hujampokea ipasavyo, maanisha kutubu dhambi zako zote na kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Yesu ili upokee Roho Mtakatifu na uwe miongoni mwa wateule wa Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *