Je mzigo wako umeondolewa begani mwako?
Shalom jina la Bwana libarikiwe. Karibu tujifunze maneno ya Mungu.
Biblia inasema katika..
Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, KWA SABABU YA KUTIWA MAFUTA”.
Hayo ni maneno ya faraja ambayo Mungu anasema na watu wake waliopelekwa utumwani huko Ashuru na Babeli kwasababu ya makosa yao. Hivyo huu ni unabii uliotolewa na nabii Isaya kwa Neno la BWANA kabla wana wa Israeli kupelekwa utumwani, na ulikuja kutimia baada ya wana wa Israeli kukaa takribani miaka 70 utumwani, ijapokuwa ni mabaki tu waliorudi..hao waliorudi BWANA aliwaondolea ule mzigo mzito waliokuwa wamebebeshwa na mfalme wa Ashuru na mfalme wa Babeli.
Neno la Mungu linasema..
Isaya 10:22-27 Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki.
[23]Kwa maana Bwana, BWANA wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote.
[24]Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri.
[25]Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza.
[26]Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.
[27]Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.
Hata na sisi kabla hatujakombolewa..tunakuwa utumwani na tunakuwa tumefungwa nira na adui na kubebeshwa mzigo mzito sana
Mtu yeyote ambaye hajaokoka, haijalishi atakuwa na mafanikio makubwa kiasi gani, tayari yupo chini ya kongwa la shetani, na anaongozwa kuelekea kuzimu. Lakini aliyemwamini Yesu na kuoshwa dhambi zake, yupo chini ya kongwa/Nira ya Kristo, akiongozwa kuelekea uzimani (Mathayo 28:11).
Unaelewa maana ya Nira/Kongwa?
Nira ni kifungo Fulani ambacho mnyama kama ng’ombe anavikwa shingoni, kama nyenzo ya kuvuta mzigo ulio nyuma yake..
Hivyo katika imani, ipo nira ya adui na nira ya Kristo.
Nira ya adui shetani ni ulevi unaoutumainia ambao unakufanya kuwa mtumwa wa pombe na sigara!.. Nira ya shetani ni uzinzi na ukahaba unaoufanya ambao huwezi kuishi bila huo.. Nira ya adui shetani ni ushabiki wa mpira unaokufanya uwe mtumwa wa huo mpira.. Nira ya adui shetani ni tamaa zote za macho ambazo zimekufanya kuwa mtumwa..Nira hiyo huwezi kujivua mwenyewe, kwasababu aliyekufunga hukuwa na nia ya wewe kukuacha huru siku moja! Hivyo unahitaji kuondolewa hiyo mizigo ya dhambi zilizokulemea na hiyo nira iliyokufunga iharibiwe kabisa. Lakini itaharibiwaje? Sio kwa njia nyingine isipokuwa kwa KUTIWA MAFUTA, hebu turejee tena hili andiko..
Isaya 10:27 Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, KWA SABABU YA KUTIWA MAFUTA.
Ahaa, kumbe mzigo wa dhambi na nira ya shetani itaondolewa kwasababu ya kutiwa mafuta? Kumbe sio kwa kuombewa au kwa kutoa sadaka! Maana yake ukitiwa tu mafuta, basi mzigo wote iwe ni ule uasherati ambao unashindikana sasa kuacha..pindi utakapotiwa hayo mafuta, huo uasherati na dhambi zingine zote zinazoleta utumwa zinaondoka zenyewe kabisa na huyo mtu anakuwa huru, ile hamu ya kufanya hayo mambo mabaya inaondoka kabisa ndani mwake.
Sasa hayo mafuta ni yapi na tunayapataje?
Mafuta kibiblia yanawakilisha Roho Mtakatifu, ndio maana kila mara watu waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, maandiko yanatumia neno “wakajazwa”, na sio neno kama ‘wakavikwa’ au labda ‘wakalishwa’. Kwasababu tukisema wakavishwa maana yake tunamfanya yeye kuwa kama nguo, au tukisema wakalishwa tunamfanya yeye kuwa kama chakula. Lakini tukisema wakajazwa tunamfanya yeye kuwa kama kimiminika, na hicho si kingine zaidi ya MAFUTA. Roho Mtakatifu anakuja kwetu kama MAFUTA.
Na akija juu yako, anaharibu ule mzizi wa dhambi ndani yako..hiyo nira inayokubebesha mzigo wa dhambi anauharibu kabisa..na hapo ndipo neno hili la Isaya 10:27 litatimia juu yako, kwamba..
“itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.”
Swali ni je! umetiwa mafuta? Je! umejazwa kabisa katika kiwango kinachotakiwa?
Kumbuka, pasipo kujazwa mafuta (Roho Mtakatifu), hauwezi kamwe kutoka katika utumwa wa dhambi? Hiyo dhambi itaendelea kukutumikisha na mwisho wake utakulipa mauti, kwa maana..
“.. mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”(Warumi 6:23)
Sasa, utatiwaje mafuta? Au utampokeaje Roho Mtakatifu? Biblia imetoa muongozo katika..
Matendo ya Mitume 2:38-39 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Umeona kanuni ya kumpokea Roho Mtakatifu? Ni kutubu na kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo.
Na kutubu ni kudhamiria kuacha dhambi kabisa kwa vitendo na kwenda kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, zingatia ni kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 10:48)
Kumbuka kama bado hujampokea Yesu, basi fahamu kuwa bado unayo nira ya adui shetani mwako, na upo kwenye utumwa wa dhambi hata kama hujijui, Hivyo mgeukie leo Kristo akuweke huru,Yeye mwenyewe alisema ” Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli ( Yohana 8:36)”,
Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote unazozitenda kwa siri na kwa wazi, na kisha tafuta ubatizo sahihi, ubatizwe kwaajili ya ondoleo la dhambi zako, Na baada ya hapo amua kujitia Nira ya Kristo, kwa kudhamiria kumtumikia yeye kwa gharama zozote zile, na Bwana mwenyewe atakufanya kuwa mtumwa wake.. na thawabu yako itakuwa kumbwa hapa duniani na utakapofika mbinguni.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.