Je mzizi wa dhambi umekatwa ndani yako?
Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo, Karibu tujifunze habari njema za uzima wa roho zetu.
Mzizi maana yake ni chanzo cha kuwepo kwa kitu fulani au jambo Fulani, au tatizo fulani.
Kwa mfano, ili mti uweze kustawi vizuri na kuzaa matunda ni lazima kuwe na mizizi inayoenda ndani kuvyonza virutubisho kutoka kwenye udongo, na iwapo utakata zile mizizi basi ule mti ni lazima tu utakauka… Vivyo hivyo na vitu vingine ili viweze kuzaa matunda ni lazima kuwe na chanzo chake…na kile chazo kikiondolewa yaani ule mzizi ukikatwa, kitu hicho hakiwezi kuzaa matunda. Biblia inasema katika..
Hosea 9:16 Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana.
Na kadri mzizi..tuchukulie labda mzizi wa mti, kwa kadri mizizi inavyoenda ndani sana kwenye ardhi ndivyo ule mti unakuwa na uhai hata wakati wa ukame, ndio maana miti yenye mizizi ya namna hiyo..mara nyingi huwa haipotezi maji.. hivyo wakati wa kiangazi huweza kuzaa matunda kama kawaida.. kwasababu mizizi yake imeenda ndani sana na kuchukua maji, Maandiko yanasema..
2 Wafalme 19:30 Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.
Ikiwa na maana kanisa kama taifa la Mungu ni lazima likite mizizi yake chini kabisa kwenye vilindi vya maji ya uzima (Roho Mtakatifu) ili liweze kuzaa matunda, mizizi hiyo ni pamoja na Kuomba pasipo kukoma, kusoma Neno kwa undani Zaidi, kufanya unjilisti, kukusanyika, n.k hivyo kila mwamini ni lazima ashughulikie mizizi hiyo mpaka ifike ndani kabisa ya mito ya maji.
Sasa, kwa leo hatutazungumizia mizizi hiyo ya kanisa katika kumzalia Mungu matunda, leo tutaangalia njia ya kukata au kuondoa mzizi wa dhambi.. kwakuwa dhambi ndio sababu ya mambo yote mabaya tunayoyaona leo na ndiyo inayompeleka mtu katika jehanum ya moto.
Na moja ya jambo kubwa ambalo lilimleta Yesu Kristo duniani ni kuja kukata ule mzizi wa dhambi (kuondoa kabisa), ambayo hapo mwanzo hakuna aliyewahi kufanya jambo hilo. Ndio maana siku ile wakati Bwana anatoa roho yake alisema..
Yohana 19:30 Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Ukiangalia hiyo sentensi vizuri, Bwana hajasema yamekwisha kana kwamba ni vingi..bali alisema imekwisha..ikimaanisha ule mzizi wa dhambi ndio ulikuwa mwisho pale, baada ya Bwana kukamilisha ile kazi aliyoifanya hapo kalvari ya kuondoa mzizi wa dhambi kuanzia hapo dhambi haikuwa na nguvu tena juu ya wale wote watakaomwamini kweli kweli.
Watu wengi ambao wanadai wameokoka na bado dhambi ina nguvu juu yao..ni kwasababu mzizi wa dhambi huwenda haikukatwa ndani yao.. hivyo dhambi inaendelea kumea na kuzaa matunda hata kama huyo mtu hataki.
Ukweli ni kwamba mtu akiokoka kweli kweli yaani akimwamini Bwana Yesu na akatubu dhambi zake kwa kumaniasha kuziacha kabisa na akabatizwa katika ubatizo sahihi, ni lazima tu mzizi wa dhambi ukatwe ndani yake.. kwasababu Bwana Yesu alimaliza kabisa ule mzizi wote wa dhambi pale Golgotha..na akasema imekwisha.
Hivyo ukiona umeokoka na bado dhambi ya uasherati, uzinzi, uongo, tamaa, n.k vinakushinda, Fahamu kuwa huwenda bado hujampokea Yesu kabisa kabisa, hivyo angalia jinsi ulivyosikia na kuamini.
Kwasababu maandiko yanasema..
“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.” (1Yohana 3:9)
Mtu aliyezaliwa mara ya pili yaani aliyemwamini Yesu Kristo sawa sawa na kubatizwa kisahihi..na Roho wa Mungu akakaa ndani yake katika ujazo wote, mtu huyu kutenda dhambi ni vigumu kwasababu mzizi wa dhambi umekatwa ndani yake, sio kwamba hatakutana na majaribu ya dhambi, hapana atakutananayo kwasababu ya huu mwili lakini dhambi haitamtawala/haitakuwa na nguvu juu yake.
Wakati mwingine atakasirika ndiyo, kama mwanadamu lakini hawezi kuzalia matunda hiyo hasira, na ni vigumu sana mtu aliyezaliwa mara ya pili kutenda dhambi za makusudi kama uongo, usengenyaji, uzinzi, wizi kwasababu hana mzizi wa dhambi.
Kuna mtu hataki kufanya uzinzi, au kutumia vilevi na madawa ya kulevya, au kusema uongo, kutukana, kusengenya, lakini kwakuwa mzizi wa dhambi haujakatwa ndani yake..anajikuta anafanya kile asichokipenda na kuacha kufanya kile anachokipenda.. ndiyo kilichomkuta Mtume Paulo kabla hajaokoka na mzizi wa dhambi kukatwa ndani yake.
Warumi 7:14-15,17-25 Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.
[15]Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.
[17]Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu
[18]Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.
[19]Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.
[20]Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
[21]Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya.
[22]Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani,
[23]lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.
[24]Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
[25] NAMSHUKURU MUNGU, KWA YESU KRISTO Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
Umeona hapo, kuna dhambi inakaa ndani ya mtu ambaye hajampokea Yesu kwa ukamilivu, na dhambi hiyo ndiyo inayomtumikisha huyo mtu kwa lazima kiasi kwamba mtu huyo anajikuta anafanya kile asichokipenda, sasa habari njema ni kwamba Mungu aliliona tatizo hilo toka mwanzo.. hivyo akaandaa mpango wa kutatua tatizo hilo..na mpango huo ulikamilishwa ndani ya Yesu Kristo..yeye ndiye suluhisho la dhambi na pasipo kumwamini yeye mtu ataendelea kuwa mtumwa wa dhambi na mwisho ataishia motoni . ndiyo maana anatuambia..
Yohana 8:24 Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.
Hakuna namna nyingine ya kuondoa mzizi wa dhambi isipokuwa umemwamini huyu Yesu na kumpokea kweli kweli, kumbuka zisungumzii kuacha dhambi kwa namna ile ya kimazoea, nazungumzia kukata mzizi wa dhambi, kwasababu unaweza ukasema umeacha leo hiyo dhambi na kesho ukarudia..hapo bado hujaacha, na mzizi wa dhambi kwa namna hiyo haiwezi kukatwa ndani yako, mpaka uamue kumfuata Yesu kweli kweli na kuacha yale mambo unayoshikilia hata kama vinakupa raha sasa, lazima uamue kuviacha kabisa na kuzama ndani ya Yesu kweli kweli..bila kufanya hivyo mzizi wa dhambi haiwezi kukatika kirahisi rahisi tu, kwa kusema kwa mdomo nimeokoka na kwenda kanisani..hapo dhambi itakutumikisha tu na mwisho itakulipa mshahara wa mauti.
Kwahivyo kwa hitimisho, mzizi wa dhambi unaondolewa kwa kumwamini Yesu ipasavyo na kubatizwa ubatizo sahihi na kujazwa Roho Mtakatifu.
Matendo ya Mitume 2:37-38 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Dawa ya kuondoa dhambi ni kutubu kwa kumaanisha kabisa kujikana nafsi na kuacha dhambi zote unazozifanya kwa siri na kwa wazi pasipo kurudia tena na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Bwana Yesu, ukichukua hayo maamuzi ndipo Roho wa Mungu ataingia ndani mwako na kukata ule mzizi wa dhambi. Na hapo dhambi haitakutawala tena, ile dhambi ambayo ilikuwa inakutumikisha kuanzia hapo utaona ni kawaida tu kuishi bila kufanya, ule uasherati, na ulevi ambao ulikuwa unashindwa kuacha kuanzia hapo utashuhudia mwenyewe kuwa kuishi pasipo kufanya hayo mambo inawezekana kabisa, kuishi bila kuvaa vimini, na kutumia mikorogo na mapambo yote ya kidunia inawezekana kabisa, kuishi bila kusengenya, kudanganya, kuiba, kutukana ni maisha ya kawaida sana…hiyo yote ni kwasababu mzizi wa dhambi umekatwa ndani yako.
Je mzizi wa dhambi umekatwa ndani yako?
Hebu jitathimini maisha yako ya wokovu ikiwa yanaendana na wokovu wenyewe. Na ikiwa wewe mwenyewe Unaona bado kuna dhambi inakutumikisha, basi ni wazi kuwa unahitaji kufanya toba ya kweli. Hivyo saa ya wokovu ni sasa kwa maana hakuna anayejua kesho yake na kuna hatari kubwa ukifa na dhambi, Ndio maana ni huzuni kwa Mungu pale mwenye dhambi anapokufa.(Ezekieli 18:23)
Na vilevile tunaishi ukiongoni mwa siku za mwisho.. unyakuo wa kanisa umekaribia sana.. yawezekana hata ni leo kwani dalili zote zimekwisha timia siku nyingi na ishara zote zinaonyesha kuwa Yesu yupo mlangoni. Na hata kama hatakuja mwaka huu, je wewe unauhakika gani kuwa utaamka kesho? Na je utaenda kuwa mgeni wa nani kule ikiwa leo umesikia injili na ukapuuzia.
Ndugu kwanini hayo yakukute ikiwa bado unayo nafasi, hebu leo amua kumgeukia Yesu na kumfuata kweli kweli.. kabla mlango wa neema haujafungwa kwako.
Ikiwa utapenda kupata msaada huo wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.