JE! UMEBATIZWA UBATIZO ALIOBATIZWA YESU?.

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Luka 12:50
“Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! “

Umewahi kulitafakari jambo hili kwa undani zaidi kuhusu ubatizo aliobatizwa Yesu Kristo pamoja kikombe alichokinywea Yesu Kristo?

Wengi wetu huwa tunaishia tu pale kwenye ubatizo wa Pale Yordani ule Bwana Yesu aliobatizwa na Yohana Mbatizaji, (aliokuwa akibatizwa Yesu Kristo). Lakini leo tutaangalia ubatizo aliobatizwa Yesu Kristo ambao kila Mkristo ni lazima abatizwe kwa namna yake. Maadamu amemuamini Yesu Kristo.

Tofauti na ule ubatizo wa maji(ni wa muhimu sana kwa Mkristo pia wa maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo.)  Ubatizo huu yeyote anaweza akabatizwa hata manabii wa uongo,majini,Mashetani nayo yanabatizwa ule ubatizo wa Yordani Lakini uko ubatizo ambao si kila anaesema ni Mkristo anaweza kukubaliana nao. Hebu tusome kidogo maandiko.

Marko 10
38 Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?

39 Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa;

Ukisoma kuanzia juu utaona hapo wana wa Zebedayo(Yakobo na Yohana) waliomba katika utukufu wake mmoja akae mkono wa kuume mwingine mkono wa kushoto.

Lakini sasa tuangalie jibu analolijibu Bwana  Yesu Kristo. Anasema…. “Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?

Unaona hapo!, hasemi “HAIWEZEKANI ” lakini anawauliza je? Wataweza kubeba gharama ya kukipata kile wanachokiomba/wanachokitaka?

Lakini wakajibu wakamwambia kuwa wanaweza. Yesu aliona wamejibu kwa kudhamilia kabisa ijapokuwa hawakujua gharama halisi na uhalisia wote wa kile wanachokiomba. Lakini walikuwa tayari.

Sasa tukirudi kwenye mstari wetu hapo juu kabisa Bwana Yesu anasema…..

Luka 12:50
“Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! “

Unaona hapo? Ni tofauti na ule wa kwanza ambao kila mtu anasema amebatizwa! Ila upo ambao alitakiwa kuutimiliza tena kwa dhiki nyingi sana. Tutakwenda kuona ubatizo upi huo!!

UBATIZO AMBAO ALIBATIZWA YESU NA KILA ANAEMWAMINI LAZIMA AUPITIE NI UPI HUO?.

Kila aliemwamini Yesu Kristo kweli kweli lazima apite katika ubatizo huo. Ili kufikia kile Mungu alichokusudia Kuna gharama za kuingia kwetu kama waamini na sio ngumu wala kubwa kama tukitambua kuwa “kilichoko mbele ni kizuri na kikubwa sana kuliko kitu chochote

Mungu kuweka vitu hivi si kutukomoa bali ni kutuandaa na kutukamilisha. “Hakuna maandalizi yoyote yasiyokuwa na gharama

1. DHIKI/MATESO.
Hili ni jambo ambalo Mwokozi wetu alipitia kama vile alivyopita katika dhiki na majaribu ni lazima na sisi tuliomwamini Yesu kupita katika ubatizo huu kila mmoja kwa namna yake kila mmoja mmoja kwa njia yake tunaona hata Mtume Yohana alipitia ubatizo huu(dhiki).

Ufunuo wa Yohana 1:9
“Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye KUSHIRIKI pamoja nanyi katika MATESO na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. ”


Unaona hapo anasema “….kushiriki pamoja nayi katika mateso..” hasemi  “mwenyewe kuangalia/kutazama au kusikia. lakini anasema MWENYE KUSHIRIKI. Watu wengi wanapopita katika ubatizo huu huanza kulalamika na kukata tamaa hivyo wanaishia kunaswa na adui. na kuishia kuwatazama wengine tu ambao wanapita na watakwenda kupata utukufu mkubwa sana.

2.KUKATALIWA NA KUONEKANA UMERUKWA NA AKILI.

Luka 9:22
“akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. ”

Huu ni ubatizo/kikombe ambacho kila Mkristo lazima abatizwe kwa ubatizo huu kwa namna yake yeye mwenyewe.

kama vile Bwana wetu alivyofanyiwa vivyo hivyo hata kwetu. katika maisha ya Ukristo lielewe hili jambo usije ukakata tamaa na kuona Mungu amekuacha. upo wakati utakataliwa kama huoni hiki kitu kitakuja kama hakitakuja basi hujatembea kweli kweli katika maisha ya Kikristo fanya hima.


Maandiko yanasema mwokozi mwenyewe alionekana amerukwa na akili yaani MUNGU mwenyewe. Ni jambo la kutisha sana.

Marko 3:21
“Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, AMERUKWA NA AKILI. ”

Unaona hapo? Huu ndio ubatizo ambao Yesu aliwauliza Yakobo na Yohana kwamba wataweza? Na wakasema “Tutaweza”. Ukisoma pia…

Yohana 10:20
“Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza? ”

Umewahi kufikili kuwa “anaeambiwa maneno haya anapepo ni Mungu mwenyewe alieziumba mbingu na nchi yaani Elohimu mwenyewe. Ni jambo la kuogopa sana.”

Sasa kama Mungu mweyewe anaambiwa maneno kama hayo vipi mimi na wewe??.

Tunaona jambo hili pia linajitokeza kwa Paulo. Hebu tusome….

Matendo ya Mitume 26:24 
“Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una WAZIMU, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. ”

Je na wewe umebatizwa ubatizo huu?  Umekinywea kikombe hiki? Kama bado ziangalie njia zako vyema.

3.KUCHUKIWA.
Huu ubatizo ni lazima kila Mkristo aupitie kwa sehemu yake. Usifikiri wala kudhani kuwa ukiokoka utapendwa ndugu litoe kwenye akili yako jiandae kuchukiwa na ndugu zako,rafiki zako, na ulimwengu wote.maana utakuwa kinyume nao usidhani utapendwa maandiko yameshasema….

Mathayo 24:9
“Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa KUCHUKIWA na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. ”


Unaona hapo! Anasema “…watu wa kuchukiwa na mataifa yote”  hasemi  “..mtapendwa na mataifa yote” Bali kuchukiwa tena sio na mataifa machache bali yote.

ikiwa wewe ni mchungaji,nabii,muombaji wa Kwaya muinjilisti nk tegemea hata katika huduma hiyo kusalitiwa na kuchukiwa hata na wapendwa wenzako.

4.KUJITOA KWA AJILI YA WENGINE.
Hiki ni kitu ambacho kila Mkristo lazima awenacho(ubatizo) kujitoa kwa ajili ya wengine sio karama ndugu yangu. Kama Bwana Yesu alivyojitoa na mitume wake walifanya hivyo hivyo walikuwa tayari hata kufa. Maisha ya Ukristo ni kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Lakzima ifikie hatua tuyaone maisha yetu si kitu kabisa tujihesabu kama kondoo wa kuchinjwa.

Warumi 8:36.
“Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. ”

Je ubatizo kama huu tumebatizwa nao?, tunakubali kubeba gharama ili kukipata kile tunachokihitaji? Fanya hima ndugu yangu leo.

Tupo katika nyakati za Mwisho hizi ndugu yangu muda na wakati wowote Yesu atakuja. Je umebatizwa ubatizo huu? Maandiko yanasema…

Matendo ya Mitume 14:22.
“wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.

Si kwamba ni ngumu ni rahisi sana kama tukiamua kumfata Kweli Yesu Kristo kwa kudhamiria ni rahisi Mungu anaachilia neema yake badala uwe na huzuni katika nyakati nzito inageuka kuwa ni Furaha na Amani ndani yetu. JE CHAPA ZA YESU UNAZO NDANI YAKO?.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *