Je! unakunywa maji kwa namna gani?

Biblia kwa kina No Comments

Je! unakunywa maji kwa namna gani?

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu liwezalo kutupa uzima tele.

Tukisoma kitabu cha Waamuzi 7 na ule mstari wa 4, Mungu anamwambia Gideoni..

BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.

[5]Basi akawaleta watu chini majini. BWANA AKAMWAMBIA GIDEONI, KILA MTU ATAKAYERAMBA MAJI KWA ULIMI WAKE, KAMA VILE ARAMBAVYO MBWA, HUYO UTAMWEKA KANDO; KADHALIKA KILA MTU APIGAYE MAGOTI KUNYWA.

[6]Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.

[7]BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake.” (Waamuzi 7:4-7)

Hapo, tunasoma Bwana anamwambia Gideoni awatenge watu pande mbili, wale ambao watakunywa maji kama vile mbwa arambavyo kwa ulimi awaweke kando, na wale wapigao magoti kunywa vivyo hivyo wakae pembeni. Na tukiendelea kusoma tunaona wale waliokunywa maji kwa kuyaramba kama mbwa walikuwa watu mia tatu, na wengine wote walikunywa kwa kupiga magoti, hivyo Bwana akamwambia Gideoni kwa watu hao mia tatu atawaokoa Israeli.

Nini Bwana anataka tujifunze hapo? Pamoja na mengi ambayo tunaweza kujifunza kulingana na hiyo habari. Lakini leo tutajifunza jambo moja kubwa la msingi sana.

Ulimwengu huu unafananishwa na maji, tena maji mengi (bahari), biblia inasema hivyo katika..

Ufunuo wa Yohana 17:15 Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”. (ulimwengu)

Maana yake ni nini?

Sisi kama wasafiri katika ulimwengu huu, tunajua makao yetu sio hapa, hivyo tunapaswa kuwa makini sana tunapotumia maji haya… yaani huu ulimwengu, pamoja na kwamba wakati mwingine tutahisi kiu tukiwa safarini, lakini tunapaswa tunywe maji haya kwa ungalivu, hatupaswi kuzama kabisa kabisa na kujisahau, tunapaswa tunywe kwa namna ile ya kuramba kama vile walivyofanya wale watu mia tatu ambao Bwana aliwachagua kuwatumia. Ndivyo biblia inavyotufundisha kwamba tutumie huu ulimwengu kwa kiasi… kwasababu muda tuliobakiwa nao ni mfupi. Hivi punde tutaingia katika makao yetu ya milele huko ndiko tutazima kiu ya mambo yote.

1Wakorintho 7:29 “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;

30 na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.

31 NA WALE WAUTUMIAO ULIMWENGU HUU, KAMA HAWAUTUMII SANA; KWA MAANA MAMBO YA ULIMWENGU HUU YANAPITA.

32 Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;

33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.

34 Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.

35 Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”.

Ni kweli tupo katika huu ulimwengu, hatuna budi kuutumia kwa sehemu, lakini tumeaswa, tuwe kama vile hatuutumii, tuwe kama tumejiegesha tu, tusizame huko moja kwa moja, kiasi cha kutufanya tusahau kama sisi ni wapitaji, wenyeje wetu upo mbinguni.

Tuishi kama wale mashujaa 300 wa Gideoni, ambao wenyewe, walipopelekwa mtoni kunywa maji, hawakunywa kama Ng’ombe kwa kupeleka midomo yao moja kwa moja kwenye maji, bali walikunywa kwa kuchota kwa mikono yao na kuyalamba kama mbwa midomoni,. Ikiwa na maana kuwa hata maadui zao wangeweza kuja wakati wanakunywa maji yao wasingeweza kuwaua kwa haraka kwasababu wangewaona tokea mbali , tofauti na wale wengine ambao midomo yao ilielekea kwenye maji moja kwa moja, hawaelewi kitu kingine.

Kumbuka baharini/majini ndiko aliko yule mnyama hatari ambaye moja ya siku hizi atatoka na kuwatawala watu na kuwatia chapa ya kwenda motoni.

Ufunuo 13:1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.

[2]Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.

Sasa, ukizama moja kwa moja kunywa maji kama ng’ombe utaachaje kunaswa na huyo mnyama, ni lazima tu akumeze. Hivyo kama umeokoka kweli kweli, yaani umeamua kuwa msafiri, basi hekima ya Mungu leo inakufundisha ujue kuutumia huu ulimwengu kwa kiasi, maana ipo hatari kubwa itakutokea utakapozama moja kwa moja kwenye ulimwengu.

Ndiyo tunaishi duniani kuna vitu hatuwezi kuviacha moja kwa moja kuvitumia, lakini tunapaswa tuishi kwa kuchukulia kawaida kila kitu, ili tusimpe shetani nafasi ya kutuvuta katika mambo mengine, tusizame moja kwa moja kwenye ulimwengu, tunapaswa tupate na nafasi kwa Mungu, kama ni shule, kama ni biashara, kama ni kazi, kama ni ndoa, kama ni sherehe, kama ni jambo lolote lile, sio la kuliumizia kichwa chako sana, au kulisumbukia, au kuliwazia kupitiliza, au kulifurahia sana.

Tukifanya Hivyo biblia inatuambia tutapata muda pia kwa Bwana. Na matokeo yake, hata siku ile ikifika haitatujilia kwa ghafla kama vile mwizi usiku. Maana biblia inasema ndivyo itakavyoujilia ulimwengu mzima. Na hiyo yote ni kwasababu watakuwa bizey katika mambo ya mwilini wakati huo.

Luka 31: 34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;

35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”.

Kwahiyo kila siku tulifahamu hili, kuwa sikumoja inapopita, ndivyo tunavyoikaribia ile siku Kuu ya Unyakuo. Hivyo ni wajibu wetu na sisi kuhakikisha ni kwa namna gani tunampendeza Mungu wetu katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho.

Wafilipi 4: 6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu”.

Bwana akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *