Je! Unayo akili?

Biblia kwa kina No Comments

Je! Unayo akili?

Kumbukumbu la Torati 32:29 Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao.

Mtu mwenye akili ni mtu mwenye uwezo wa kufikiri/kupambanua vema na kufanya maamuzi sahihi katika maeneo mbalimbali ya maisha yake.

Lakini, je biblia inasemaje kuhusu mtu mwenye akili, biblia inasema..

.. mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini”. Mithali 15:24

Hapo biblia inatueleza wazi, mtu mwenye akili, huwaza ni jinsi gani atakavyoepukana na kuzimu iliyo chini, huwaza kwenda mbinguni, huwaza kuepukana na ziwa la moto. Lakini kinyume chake ni kweli, mtu asiyewaza hatma ya maisha yake baada ya kufa itakuwaje, badala yake yupo tu, anachowaza ni ajengeje magorofa hapa duniani, ukimweleza habari za kuzimu hata hashtuki, huyo kwa Bwana hana akili, na ndio maana Bwana anasema..

“Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao”.

Lakini sio hilo tu, kibiblia mtu mwenye akili ni yule ambaye akipokea agizo lolote kutoka kwa Bwana anaweka moyoni mwake na anatii bila shuruti. Ndivyo biblia inavyosema…

Mithali 10:8 “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka”

Lakini ukiwa ni mtu wa kupinga maagizo mema, unayopewa, bali unajiona upo sawa machoni pako mwenyewe, ukielezwa, uvaaji vimini, masuruali na kaptula kwa wanawake ni dhambi, unasema hatupo agano la kale, unapoelezwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ni lazima, unasema sisi hatuamini hilo. Ujue kuwa unajiangamiza mwenyewe na ni ishara kuwa umepungikiwa kabisa na akili. Kila agizo lililo kwenye Neno la Mungu linapaswa lipokelewe na kukubaliwa kama lilivyo pasipo kuuliza uliza.

Kwa tafsiri za kidunia mtu asiye na akili ni mtu ambaye hawezi kufiriki, kuelewa, kuwasiliana, kupanga au kutatua matatizo. Hivyo, mwanadamu mwenye mtindio wa ubongo, anajulikana kama hana akili, mtu anayefeli darasani, anajulikana kama hana akili, mtu anayeshindwa na wenzake katika maisha anajulikana pia kama asiye na akili,

Lakini je! biblia inasemaje kwa mtu asiye na akili? Kibiblia mtu asiye na akili ni yule ambaye haweki sheria za Mungu ndani ya moyo wake..akisikia kwa sikio hili linatoka kwenye sikio la pili…na kinyume chake Mtu mwenye akili kibiblia ni yule anayetembea na sheria za Mungu na kuishi siku zote bila kusahau hata moja.

Mithali 10:14 “Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu”.

Ukiwa mtu wa kutozingatia, au kutotendea kazi kile unachoambiwa au kukisikia, kuhusiana na mafundisho ya adili, yaani unasahau sahau, amri au fadhili za Mungu, unakuwa mwepesi kuanguka ovyo katika dhambi, ni uthibitisho kuwa huna akili kwa mujibu wa kibiblia. Tunapaswa tuwe watu wa kuzitafakari sheria za Mungu wakati wote, kama vile mwanafunzi akaririvyo kila siku masomo yake, ili yamsaidie kufaulu mitihani yake ya mwisho. Biblia inasema…

Mithali 3:3 “Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu”.

Kwa hayo machache, hebu mimi na wewe tujitathimi, je tunayo akili kulingana na tafsiri ya akili kibiblia.

Ikiwa ni mtu wa kuwadharau wengine..unajiona we ni bora kuliko mtu mwingine..tambua kuwa akili yako inashida, kwani biblia inasema..

Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza”. (Mithali 11:12)

Vilevile, ikiwa kufanya uzinzi kwako ni kawaida, kutamani tamani na kuwaza mawazo mabaya kila wakati ni jambo la kawaida kwako, basi kulingana na biblia.. hauna akili kabisa.. haijalishi unajiona kuwa una elimu kubwa kiasi gani, au unajiona ni mjanja kiasi gani… kulingana na biblia hauna hata akili kidogo mbele za Mungu.. kwasababu unafanya jambo litakalokuangamiza.

Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Je! Unayo akili? Na iwapo unahitaji msaada, je ufanyaje ili uwe na akili mbele za Mungu, Maandiko yanasema..

Mithali 3:3 “Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu”.

“Rehema na kweli” ndiyo mlango wa kupata akili nzuri mbele za Mungu!

Na hayo mawili yanapatikana kwa mmoja tu ambaye amejaa rehema na kweli yote, na huyo sio mwingine zaidi ya Mfalme wa Wafalme YESU KRISTO Bwana wetu, yeye ndiye njia na Kweli.

Ukimpata Bwana Yesu..utaifahamu kweli yote nayo hiyo kweli itakuweka huru..na ndivyo utakapopata akili nzuri mbele za Mungu…na kinyume chake pasipo kumpata Yesu Kristo huwezi kamwe kuwa na akili mbele za Mungu.. labda mbele za wanadamu tu utajisifia lakini Mungu anakuona kuwa unamtindio wa ubongo.

Lakini swali la msingi ni hili; huyu Yesu tunampataje? Hakuna njia ya shoti (short cut), njia moja tu ambayo ipo wazi ni hii..

Matendo ya Mitume 2:37-38 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Ili Yesu Kristo aingie kwako na akupe akili unapaswa kutubu kwanza dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa kisha unajikana nafsi na kuchukua msalaba wako na kumfuata yeye..halafu unatafuta ubatizo wa maji na Roho..huko ndiko kumpokea Yesu.

Je umempokea Yesu ipasavyo?

Je Unafahamu ni nini kitakutokea endapo utakufa bila kumpokea Yesu na umesikia injili? je unahabari kuwa tunaishi ukingoni kabisa mwa siku za mwishoni?

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *