
Je! vazi la suruali limeletwa na wazungu?
Yapo mahubiri mengi ambayo ibilisi ameyainua katika siku hizi za mwisho, baadhi ya mahubiri hayo ni yale yanayohuburi kuwa Mungu haangalii mwili bali anaangalia moyo tu, ikiwa na lengo la kuhalalisha wanawake na wanaume kubadili mionekano yao Mungu aliyowaumba nayo. (Kuwa makini sana na injili hiyo maana imetoka kuzimu moja kwa moja)
Mungu wetu anaangalia roho, nafsi na mwili, ni yeye ndiye aliyetuumba kwa sura na mfano wake. Tena miili yetu ni hekalu lake hivyo anaangalia sana hekalu lake, anasema mtu akiliharibu mtu huyo ataharibiwa, soma 1Wakorintho3:17 & 6:19.
Yapo maandiko mengi tu yanaonesha kuwa Mungu anaangalia utu wa ndani mpaka utu wa nje (mwili). Hatutaweza kusoma yote hapa, lakini soma 2Wathesalonike 5:23, 2Wakorintho 7:1, & Warumi 12:1.
Lakini mtazamo mwingine ambao ibilisi ameileta katika kizazi hiki ili kuwapeleka wanawake wengi jehanumu ni hili la wanawake kuvaa suruali. Huku wakipewa huu mtazamo kuwa vazi hili limeletwa na wazungu katika karne ya 20 na kwamba halikuwepo enzi za biblia.
Na kibaya zaidi ibilisi ameenda mbali hadi kubadilisha andiko hili ambalo linasema..”Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo, kwa BWANA, Mungu wako.” (Kumbukumbu 22:5)
Wahubiri wengi wa ibilisi wanasema andiko hili halilengi mavazi bali linalenga tabia fulani fulani jambo ambalo ni kupotosha ukweli kabisa.. kumbuka lengo ni ili wanawake waendelee kuvaa mavazi yasiyopasa jinsia zao (suruali) na mwisho waende kutupwa katika giza nene.
Biblia inasema je! hayo maumbile hayafundishi? We mwenyewe unapotazama maumbile ya mwanaume na mwanamke je! Unaona suruali ni vazi la kike? Jihukumuni ninyi wenyewe.
Vazi la suruali lilikuwepo tangu agano la kale.
Vazi la Suruali mara ya kwanza katika biblia lilivaliwa na Makuhani.
Mungu aliwapa amri makuhani watengeneze suruali ambazo zilitofautiana kimaumbile, waliambiwa watengeneze suruali fupi (yaani kaptula), Na vile vile walikuwa wanavaa zile ndefu ambazo zilifika kabisa mpaka chini kwenye viiko vya miguu.
Kutoka 28:41 “Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.
42 Nawe wafanyie SURUALI ZA NGUO YA KITANI, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;
43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake”.
Na katika Israeli hakukuwa na Kuhani Mwanamke!, Makuhani wote walikuwa ni wanaume. Hivyo lilikuwa ni vazi la kiume. (Soma pia Kutoka 39:27, na Walawi 6:10)
Vile vile tunaweza kulithibitisha hilo kipindi kile cha akina Shedraka, Meshaki na Abednego. Wakati Mfalme Nebukadneza alivyowatupa katika lile tanuru la moto, maandiko yanasema walitupwa kule hali wamevaa suruali zao na kanzu zao na joho zao.
Danieli 3:21 “Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa SURUALI ZAO, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
22 Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego”.
Sasa Shedraka, Meshaki na Abednego hawakuwa wanawake, bali wanaume!, na hakuna popote katika biblia panataja au kuonyesha mwanamke kavaa suruali, kama hawa wakina Shedraki au kaagizwa kuvaa suruali kama hawa Makuhani.Hakuna!!. Ikifunua kuwa hilo ni vazi la kiume!
Mwanamke yeyote kuvaa suruali ni machukizo mbele za Mungu, Suruali sio vazi la kumsitiri mwanamke, hakuna mwanamke yeyote anayevaa suruali na kuonekana kama kajisitiri, badala yake ataonekana kama kajidhalilisha au kajifunua..Na maandiko yanasema wanawake na wavae mavazi ya kujisitiri.
1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani”
Hivyo mwanamke yeyote hapaswi kuvaa suruali, wala vimini wala nguo zozote zinazochora maungo yake.
Sasa inawezekana ulikuwa hulijui hili kuwa hilo ni vazi la kiume, lakini leo umejua na ndani ya kabati lako kumejaa suruali, nataka nikuambie, usingoje kesho, leo leo zitoe kazichome moto!, wala usimpe mtu!.. zichome na tafuta magauni au sketi ndefu!, usiogope kuonekana mshamba mbele ya ulimwengu!. Ni heri uonekane mshamba lakini unakwenda mbinguni kuliko kuonekana wa kisasa lakini sehemu yako ni katika lile ziwa la moto!.
Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.