Je vipofu hawana dhambi kulingana na Yohana 9:41.
Tusome..
Yohana 9:41 “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa”.
Awali ya yote tufahamu kuwa vipofu ambao Bwana anawazungumzia hapo sio vipofu wa mwilini bali ni wa rohoni, maana yake ni watu wasioona, wasiojua mambo ya rohoni hao ndio vipofu.
Sasa swali ni je! watu wa namna hiyo hawana dhambi? yaani watu wasioona/wasiojua mambo ya rohoni.
Hebu turejee kusoma kuanzia juu kidogo.
Yohana 9:39-41 “Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ILI WAO WASIOONA WAONE, NAO WANAOONA WAWE VIPOFU.
[40]Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
[41]Yesu akawaambia, Kama mgekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; LAKINI SASA MWASEMA, TWAONA; BASI DHAMBI YENU INAKAA.
Umeona hapo, watu wasioona, watu wasiojua mambo ya rohoni, wasiojua maandiko, wasiojua dhambi ni nini, kwa ufupi watu vipofu ndio hawana dhambi, kwasababu gani? Kwasababu Yesu alikuja kwa ajili ya watu kama hao… hivyo walikuwa tayari kumwamini na kuacha dhambi, Lakini wengine ambao walikuwa wanaona, walikuwa wanajua maandiko, hawakumwamini na hiyo ndiyo dhambi kubwa. Ndio maana aliwaambia dhambi yenu inakaa, kumbuka sio dhambi zenu. Ni dhambi yenu, hiyo ya kutomwamini.
Lakini haimanishi kuwa mtu akiwa hajui mambo ya rohoni hana dhambi, hapana, ina maana kuwa mtu ambaye ni kipofu wa mambo ya rohoni akihubiriwa maneno ya kweli ya Mungu ni rahisi kuamini na kubadilika, kuliko yule ambaye anajiona anajua sana, akihubiriwa injili ya kweli ni vigumu kuamini na kubadilika kwasababu anaona… hivyo dhambi inakaa kwake.
Lakini yule kipofu, utaona Bwana alimwambia tu..
”Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?[36]Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?
[37]Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.
[38]Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia”.
Lakini wale Waandishi, na Mafarisayo ambao walijiona wao ni watu wa kidini, wana madhehebu makubwa, wanajua sheria sana, waliishia kuwa vipofu, kwasababu walikuwa wanaenda kinyume na Nuru, na tunajua siku zote mtu anayetembea gizani na tochi yake mkononi, ule mwanga wa tochi akiutumia kumulika mbele yake katika njia anayoiendea utamfanya aone gizani, lakini akiigeuza ile tochi na kuyamulika macho yake, ule mwanga utamuathiri, utamfanya asione..
Ndivyo Mafarisayo na Masadukayo kilichowapata, walikuwa wanaenda kinyume na Nuru na maandiko yanasema Yesu ndiye Nuru ya ulimwengu (Yohana 8:12).Hivyo ile nuru ikawapofusha macho.
Hata leo kuna watu ambao wanaishia kuwa vipofu kwasababu wanajiona kuwa wanaona, hawataki kuamini maneno ya Mungu yanayohubiriwa kila siku masikioni mwao, wanajiona wameokoka hivyo hawana tena haja ya kubadilika, wakiambiwa biblia imesema “mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume kwa maana kila afanye mambo hayo ni machukizo” (kumbu 22:5)…wanasema neno hilo limepitwa na wakati..tunaishi katika zama za kisasa, wakihubiriwa kuwa mapambo ni dhambi wanakuambia Mungu anaangalia moyo haangalii mwili, lakini biblia imesema “kujipamba kwenu kusiwe kwa nje” (1Petro 3:3).
Hivyo ndugu, hebu jichunguze leo, upo katika kundi lipi? Wanaoona au wasioona?
Huwenda umeokoka, na unahudhuria kanisani kila wiki, unajua biblia, unafanya huduma ya kiroho ni vizuri, lakini kama upo kinyume na Neno la Mungu, basi unapaswa leo kujishusha na kuweka huduma yako pembeni, weka ujuaji wako pembeni, weka dhehebu lako pembeni, kubali kuwa kipofu ili uponywe, amini Neno la Mungu lote na kubali kubadilika. Neno la Mungu linakuambia vaa mavazi ya kujistiri, hebu kubali kuliishi hilo Neno, ondoa mavazi yote yasiyomtukuza Mungu yachome zote wala usimpe mtu mwingine, ondoa na hizo nywele bandia na kucha bandia na hizo cheni na vyuma ulizoweka masikioni mwako, kwa maana ni machukizo kwa Mungu, biblia inasema miili yetu ni Hekalu la Mungu (1Wakorintho3:16), hivyo usiangalie wingi wa watu kanisani, angalia Neno la Mungu na uliamini.
Biblia imesema mwanamke afunike kichwa chake akiwa kanisani au akiwa anafanya ibada (1Wakorintho11:5), hebu amini na ukubali kulitii hilo Neno, wala usione kuwa unajua au unaelewa zaidi kwa kuwa watu wanaoona, dhambi inakaa juu yao.
Yohana 9:41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.