JIFUNGE, KAVAE VIATU VYAKO.

Biblia kwa kina No Comments

JIFUNGE, KAVAE VIATU VYAKO.

Matendo ya Mitume 12:7-9 “Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.

[8]Malaika akamwambia, JIFUNGE, KAVAE VIATU VYAKO. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate.

[9]Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono.

Nakusalimu katika jina kuu la Yesu Kristo wa Nazareti. Karibu tujifunze hekima ya Mungu Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa njia zetu.

Moja ya silaha ambayo biblia imetuelekeza tuivae ili tuweze kuzipinga hila za yule adui ni utayari miguuni (kuhubiri injili).

Waefeso 6:14-15 “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

[15]na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

Kuhubiri injili ni silaha kuu ya kuangusha falme za giza.

Lakini pia ni agizo la Mungu tuenende ulimwenguni kote kuhubiri injili kwa kila kiumbe.

Hivyo baada ya kufunguliwa katika vifungo vya uovu na kutolewa kwenye gereza la Ibilisi (dhambi), unapaswa kuanzia wakati huo ufunge viatu vyako vizuri na kuanza kuhubiri injili.

Usisubiri Bwana Yesu akutokee na kukuambia nenda kahubiri!.. Tayari agizo lilishatoka miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita… kwamba nenda kahubiri injili.

Wengi leo hii wanaogopa kwenda kuhubiri injili, kwasababu hawana vitu vya kuhubiri.. Bwana Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wakanunue vyombo vya miziki kwanza, au spika au wapate nguo nzuri ndipo wakahubiri injili..hapana! kinyume chake aliwaambia wasibebe chochote kwasababu huko waendako watavipata vyote.

Na wewe unasubiri nini usiende kuhubiri injili? Ni wito gani unaoungoja?, ni sauti gani unayoingoja?.. na upako gani unaoungoja?…ni ujuzi gani unaousubiri?.. ukisubiri ufikie ujuzi Fulani au maarifa Fulani hutayafikia kwasababu kila siku tunakua kutoka utukufu hadi utukufu, hakuna siku tutasema tumeshajua!!.. kila siku tunajifunza..hivyo usiseme ngoja nifikia levo Fulani ndipo nikahubiri, hizo ni akili za kichanga!.. Nenda kahubiri injili..

Sasa unaanzia wapi kuhubiri injili?

Kabla ya kwenda mbali anza kuhubiri injili hapo hapo ulipo, kabla ya kufikiri kwenda nje ya mtaa anza katika mtaa wako, anza katika nyumba yako, anza katika ofisi yako, anza katika shule yako.. hakikisha hapo umemaliza kwanza na watu wameitii injili ndipo uende nje!.. na katika hatua hiyo ya awali kumbuka kuwa Kristo yupo na wewe, na kumbuka kuwa yeye amekabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani, kwahiyo hakuna nguvu zozote wala mamlaka yoyote unayoweza kushindana na hilo agizo la Bwana Yesu.

Bwana Yesu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *