
Jifunze unyenyekevu katika kuwaombea wengine.
Jina kuu la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zab.119:105).
Unyenyekevu ni jambo linalompendeza sana moyo wa Mungu, na leo tutaangalia unyenyekevu katika kupeleka maombi yetu mbele za Mungu kwa ajili ya wengine.
Mara nyingi tumekuwa tukiomba maombi ya toba na rehema kwa ajili ya familia zetu, ndugu zetu, majirani zetu na hata taifa letu jambo ambalo ni jema sana na tunapaswa kufanya mara kwa mara… lakini je! tunaomba kwa namna inayompendeza Mungu (Kwa unyenyekevu)?
Hebu tuangalie maombi ya watumishi wa Mungu jinsi walivyokuwa wakiungama makosa ya watu wao na kuomba rehema kwa Mungu, ili na sisi tujifunze kwao. (Kumbuka si kunakili au kukariri maombi yao, lakini ni kujifunza ile njia waliyoitumia ya unyenyekevu).
MAOMBI YA DANIELI:
Tunasoma..
Danieli 9:2-23 “Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.
4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;
5 TUMEFANYA DHAMBI, TUMEFANYA UKAIDI, TUMETENDA MAOVU, TUMEASI, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;
6 wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi.
7 Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa.
8 Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu TUMEKUTENDA DHAMBI.
9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi;
10 wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
11]Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.
[12]Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu.
[13]Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo HATUKUMWOMBA BWANA, MUNGU WETU, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake.
[14]Basi BWANA ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake.
[15]Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; TUMEFANYA DHAMBI, TUMETENDA MAOVU.
[16]Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka.
[17]Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.
[18]Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; MAANA HATUKUTOLEI MAOMBI YETU KWA SABABU YA HAKI YETU, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.
[19]Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako”.

Danieli ijapokuwa alikuwa ni mtu mkamilifu aliyependwa na Mungu lakini alikuwa mnyenyekevu mbele za Mungu, alijihesabia kuwa ni mwenye makosa pamoja na watu wake, alitubu kwa kufunga na kuugua, japokuwa kuomba ilikuwa ni desturi yake lakini anasema HATUKUMUOMBA BWANA, na yeye anajihesabia kuwa hakuomba toba na hivyo anastahili adhabu. Na sio Danieli tu, hebu tuangalie pia maombi ya Ezra mtumishi wa Mungu.
MAOMBI YA EZRA
Ezra 9:5 “Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za BWANA, Mungu wangu;
[6]nikasema, EE MUNGU WANGU, NIMETAHAYARI, NAONA HAYA KUINUA USO WANGU MBELE ZAKO, MUNGU WANGU; KWA MAANA MAOVU YETU NI MENGI, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni.
[7]Tangu siku za baba zetu TUMEKUWA NA HATIA KUPITA KIASI hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo.
[8]Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu.
[9]Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.
[10]Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? MAANA TUMEZIACHA AMRI ZAKO,
[11]ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao.
[12]Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele.
[13]Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, tena umetupa mabaki;
[14]je! Tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yo yote, wala mtu wa kuokoka?
[15]Ee BWANA, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili.”
MAOMBI YA NEHEMIA
Nehemia 1:4 “Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni;
[5]nikasema, Nakusihi, Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake;
[6]tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, TULIZOZIFANYA JUU YAKO; NAAM, MIMI NA NYUMBA YA BABA YANGU TUMEFANYA DHAMBI.
[7]TUMETENDA MAOVU MENGI JUU YAKO, WALA HATUKUZISHIKA AMRI, WALA SHERIA, WALA HUKUMU, ULIZOMWAMURU MUSA, MTUMISHI WAKO.
[8]Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa;
[9]bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo.
[10]Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari.
[11]Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme).”
Umeona maombi ya unyenyekevu anayoyataka Mungu. Watumishi wa Mungu japokuwa walikuwa wakamilifu lakini hawakwenda mbele za Mungu kama wasio na hatia, Nehemia hapa anasema ”mimi na nyumba yangu tumetenda dhambi” na sio familia yangu au taifa langu wametenda dhambi. Hapana huo sio unyenyekevu ni kujikweza.
Bwana wetu YESU KRISTO, ingawa alikuwa ni mkamilifu hakutenda dhambi hata moja, lakini alitubu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili yetu kwa kufunga na kuomba kwa dua nyingi pamoja na machozi.
Waebrania 5:7-10″ Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;
8 na, ingawa ni MWANA, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata;
9 naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;
10 kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki. “
Lakini wengi wetu inapotokea Bwana ametupa kibali fulani mbele zake, ndio wakati wa kujiinua na kujiona bora kuliko wengine wote, pengine kwasababu Mungu amekupa karama fulani aidha ya uchungaji, au unabii, au uponyaji, au lugha, au maono, au miujiza ukaanza kujiona bora mbele za Mungu kuliko wengine, hata maombi yako kwa Mungu unaomba kwa kujihesabia haki kama yule Farisayo. (Mathayo 18:11).
Watumishi wa kweli wa Mungu hawakuwa hivyo, licha ya kwamba walikuwa na vipawa vyote hivyo, lakini walijinyenyekeza. Hivyo na sisi hatuna budi kujifunza kwao.
Kuanzia leo nenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu hata kama unaona hauhusiki na hilo kosa, we jihesabu kuwa unahusika, lia na kuugua kwa kosa hilo, sio kwa unafiki kwa kumaanisha kabisa..na Mungu mwenye haki atakurehemu wewe na familia yako au ndugu zako.
Bwana atusaidie.
Lakini kama hujaokoka maombi yako yatakuwa ni kelele mbele za Mungu haijalishi utalia na kunyenyekea kwa namna gani. Unapaswa kwanza kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuacha na kutii Neno la Mungu, hapo ndipo utaweza kuwaombea na wengine kwa unyenyekevu na Mungu akakusikia.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.