
JINSI YA KUFUNGUA MLANGO WA MAFANIKIO
UTANGULIZI: Ni muhimu kujua hili: lengo kuu au kiini cha Wokovu ulioletwa na BWANA YESU KRISTO sio sisi tuwe matajiri au tupate mafanikio ya huu ulimwengu!.
Mafanikio ya dunia hii ni moja ya faida za mwisho mwisho kabisa za kusudi la msalaba wa Bwana YESU kwasababu walikuwepomatajiri kabla ya Bwana YESU kuja duniani, hivyo KRISTO asingeweza kuja kutegua mtego aukutatua tatizo ambalo lilishatatuliwa huko nyuma.
Ingekuwa lengo lake ni ili tufanikiwe tuwe matajiri, angetuambia tu tusikilize hekima za Sulemani na tungefanikiwa, hakukuwa na haja ya kuja kumwaga damu yake.
Lakini suala la ondoleo la dhambi hilo halikuwahi kufanyika huko nyuma, hakuna aliyewahi kuondolewa dhambi, kwani dhambi zilikuwa zinafunikwa tu! (Soma Waebrani 10:3-4)..
Sasa hiko ambacho kilishindikana kutendeka huko nyuma (katika Agano la kale) ndicho kilichokuwa cha kwanza na cha msingi kilichomleta BWANA YESU duniani, na kitu hiko si kingine zaidi ya ONDOLEO LA DHAMBI.…kiasi kwamba mtu akikosa ondoleo la dhambi hata awe na vitu vyote ulimwenguni bado anayo hasara kubwa soma (Mathayo 16:26).
Kwahiyo ni muhimu kujua msingi huu, ili tunapokwenda kujifunza juu ya MAOMBI JUU YA KAZI au BIASHARA, Usiweke moyo wako wote huko!.. Yatumie tu maarifa haya kama sehemu ya maisha, lakini jali zaidi hatima ya roho yako, kupitia damu ya YESU na UTAKATIFU.
Sasa tukirudi katika kiini cha somo letu, ikiwa unataka Mungu akupe mali, utajiri n.k, usiwekeze muda wako mwingi kumuomba Mungu akupe mahitaji hayo ya mwilini.. zaidi wekeza muda wako kuomba neema ya wokovu kwa familia yako, majirani zako na watu wote, tumia muda wako kumuomba Mungu akuongezee neema katika kumjua yeye, wekeza muda wako kumuomba Mungu akupe hekima, ufahamu, maarifa katika kuujua ufalme wake.
Tumia muda wako kuombea kazi ya Mungu (Injili) iende mbele na watu waokolewe, maombi ya namna hii ndiyo yanayomguza moyo wa Mungu, na ndiyo kanuni ya kufungua mlango wa Mungu kukufanikisha katika vitu vingine usivyoviomba.
Ndicho alichokifanya Sulemani mpaka Mungu kumpa utajiri mkuu namna ile kiasi kwamba hakuna tajiri aliyewahi kumfikia Sulemani kwa jinsi alivyokuwa na mali nyingi.
Sulemani hakukesha kumuomba Mungu ampe ule utajiri!, yeye alipoambiwa na Mungu aombe lolote, hakuomba maisha marefu, hakuomba mali, japokuwa alikuwa anauhitaji nayo, hakuomba maadui zake waangamizwe. Bali aliomba hekima ya kuwahukumu watu wote, na Mungu akumpatia hekima izidiyo hekima za watu wote duniani, na zaidi akampa na yale mengine asiyoyaomba kama utajiri na ukuu.Tunasoma
“2Mambo ya Nyakati 1:7-12
[7]Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe.
[8]Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake.
[9]Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi.
[10]Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?
[11]Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, WALA HUKUJITAKIA MALI, WALA UTAJIRI, WALA UTUKUFU, WALA MAISHA ZA WAKUCHUKIAO, WALA HUKUJITAKIA MAISHA YA SIKU NYINGI; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;
[12] BASI HEKIMA NA MAARIFA UMEPEWA; NAMI NITAKUPA MALI, NA UTAJIRI, NA UTUKUFU, KUPITA WALIVYOKUWA NAVYO WAFALME WOTE waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.”
Umeona njia rahisi ya kuufungua mlango wa mafanikio yako, hauhitaji kutumia nguvu nyingi kumuomba na kumlilia Mungu akupe utajiri au akupe mafanikio Fulani, Kumbuka ikiwa we ni mwana wake, anajua yale unayoyahitaji..hivyo we tumia muda wako mwingi kuomba mapenzi yake yafanyike yaani watu waokolewe, wamjue Yesu Kristo.
Badala ya kuombea bidhaa zako, kama sabuni unazouza, au dawa unazouza, au kingine chochote kwamba kiwe na mvuto, kuanzia leo punguza kuomba maombi ya namna hiyo, badala yake omba maombi yafuatayo.
– Kila mteja anayekuja kwako mwombee neema ya Wokovu, ikiwa bado hajampokea YESU, maombi ya namna hiyo yanamtoa yule mtu kutoka katika vifungo vya ibilisi na hatimaye kumfungua kabisa, na anapofunguliwa aweza kuwa mteja wako wa ajabu sana, au akawaleta na wengine wengi mahali ulipo.
– Ikiwa tayari ameshampokea YESU mwombee azidi kusimama katika imani, na mwombee akawe Nuru kwa wengine wengi, ombea na familia yake kama unaijua, hiyo ndio njia bora ya kuombea kazi yako au biashara yako na kufungua mlango wa mafanikio.
– Unafanya biashara ya chakula, na wateja wako ni watu wa kidunia, badala ya kuombea madishi na chakula unachokipika kwamba wakipende, hebu waombee wampende YESU, halafu uone kama hiko chakula chako hawatakipenda, zaidi ya vyakula vya wengine wote.
– Pale ofisini acha kuombea uso wako kwamba upate kibali, sawa waweza kuomba hivyo, lakini isizidi sana kiasi kwamba hujui kitu kingine cha kuomba zaidi ya hicho, badala yake anza kuomba watu wa ofisini kwako wamjue MUNGU, wakimjua MUNGU wewe utapata kibali tu!, wala hutatumia nguvu nyingi.
–Pale shuleni acha kuombea walimu wakupende, hebu waombee wamjue YESU na kumpenda, halafu uone kama hawatakupenda na wewe.
Ukitaka kufunga kwaajili ya biashara yako!, Funga kwa maombi ya kuwaombea wateja wako wokovu na Neema zaidi, kama unayo list, anza mmoja baada ya mwingine, wapatanishe na KRISTO hivyo uone kama KRISTO pia hatakupatanisha nao, utaona kazi zako zinaenda, shule yako inaenda, biashara yako inaenda, kazi yako inaenda.
Lakini ukijikita tu kuziombea bidhaa kama vile waganga wanavyotoa dawa za kwaajili ya biashara, matokeo yake yatakuwa ni madogo sana.
Hivyo OMBA lakini omba kwa shabaha/target.
1Wafalme 3:11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;
[12]basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.
[13]Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.