Kila mtu kwa mkono mmoja alifanya kazi na kwa mkono wa pili alishika silaha.

Biblia kwa kina No Comments

Kila mtu kwa mkono mmoja alifanya kazi na kwa mkono wa pili alishika silaha.

Hii ni habari ambayo tunaipata katika ujenzi wa lile hekalu la pili ambalo lilijengwa na akina Zerubabeli, Yoshua, Ezra na Nehemia baada ya kumobolewa na kuharibiwa na mfalme Nebukadreza.

Kama tunavyofahamu ule ujenzi ulikuwa ni wa shida sana, ulikuwa ni wenye vikwanzo vingi sana, vilevile uliozungukwa na maadui wengi, ili kukwamishwa tu Hekalu lile lisijengwe.

Ni kawaida ya shetani huwa akishajua jambo fulani au ujenzi fulani unafanyika, ambao utaleta madhara makubwa katika ufalme wake huko mbeleni, au utakuwa na utukufu mkubwa Zaidi wa Mungu ni lazima alete vipingamizi vingi..Na ndivyo ilivyokuwa katika ujenzi huu, Mungu aliwaambia wayahudi kuwa utukufu wa nyumba hiyo ya pili utakuwa ni mkuu kuliko ule wa nyumba ya kwanza (Hagai 2:9). Hivyo shetani kulijua hilo akanyanyua vipingamizi vingi sana.

Hivyo Zeruababeli na Yoshua walipooanza kuijenga nyumba, mwanzoni tu wakakumbana na mikono ya maadui zao, wakawatisha wasiijenge, mpaka wakaenda kuomba kibali kutoka kwa mfalme, kazi hiyo isiendelee, mpaka baada ya miaka mingi kupita Mungu anawanyanyua tena mioyo yao na kuwaambia waanze kazi wasiogope.,Ndipo Mungu akawa pamoja nao na kuimaliza.

Lakini baadaye tena muda mrefu kupita hapo tayari hekalu limeshakamilika,shetani hakupumzika alilivamia tena hekalu, na kuharibu kuta zake, hapo ndipo tunaona Mungu akimnyanyua mtu mwingine aliyeitwa Nehemia, ili kuzisimamisha tena kuta za mji na kulikarabati hekalu, lakini mambo hayakuwa maraisi kama ilivyokuwa.

Maadui waliwalemea wakina Nehemia, ukipata nafasi pitia mwenyewe kitabu cha Nehemia usome jinsi walivyopata tabu..Mpaka ikafikia wakati sasa, kila mjenzi anabidi ajifunze na ujuzi mwingine wa ziada..Kwamba sio tu kujenga,

Bali pia kulinda..Kila mjenzi alilazimika kubeba silaha zake mgongoni, na wakati huo huo alikuwa anajenga..ili kwamba ikitokea tu maadui zao wamewavamia wakati wowote, basi wawezi kupambana nao. Na wengine walikuwa wakipokezana..wakati wanajenga wengine wanalinda.

Nehemia 4:16 “Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.

17 Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, KILA MTU ALIFANYA KAZI KWA MKONO MMOJA,NA KWA MKONO WAKE WA PILI ALISHIKA SILAHA YAKE;

18 nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.

19 Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;

20 basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania

21 Hivyo tukajitia katika kazi hiyo; na nusu yao waliishika mikuki, tangu alfajiri hata nyota zikatokea.

22 Kadhalika, wakati ule ule, nikawaambia watu, Kila mtu na akae ndani ya Yerusalemu pamoja na mtumishi wake, wapate kuwa walinzi wetu wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.

23 Basi mimi, na ndugu zangu, na watumishi wangu, na watu waulinzi walionifuata, hatukuvua nguo zetu hata mmoja; kila mtu alikwenda kuteka maji akichukua silaha yake.”

Sasa hilo lilikuwa ni hekalu la mwilini, vipi kuhusu hekalu la rohoni ambalo ni kanisa, yaani mimi na wewe tuliomwamini Bwana YESU.

Biblia imetuagiza tuvae silaha zote za Mungu ili tuweze kuzipinga hila za shetani.

Waefeso 6:10-13 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

[11]Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

[12]Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

[13]Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”

Hii ikiwa na maana ukiwa kazini ni lazima uvae hizi silaha, huna budi kufanya kazi kwa mkono mmoja na mkono wa pili unashikilia silaha, ukiwa shuleni ni hivyo hivyo, ukiwa kwenye utumishi ni vivyo hivyo. Kila mahali ulipo ni lazima kama mkristo ushikilie silaha zote kwasababu adui wetu kama simba angurumaye anazunguka zunguka amtafute mtu ambaye amesimama imara kwenye wokovu ammeze (1Petro5:8), Kumbuka sio Mkristo vuguvugu.

Usidhani shetani anafurahia wokovu wako, anafanya kila mbinu akuangushe, hivyo shikilia silaha zote za Mungu vyema, lakini ukiweka akili yako yote kwenye mambo ya dunia hii, hautajua saa ambayo adui atakumeza. Hatuna budi kuwa kama wale mashujaa mia tatu wa Gideoni ambao kwa mkono mmoja walikunywa maji na mkono wa pili ukaushikilia silaha. (Waamuzi 7:6)

Na silaha mojawapo ya kuangusha hila za shetani ni MAOMBI. Hivyo ni lazima tuwe waombaji kila siku tena wa masafa marefu (kiwango cha chini angalau kiwe ni lisaa limoja kila siku). Na pia tusiache kuombea kazi ya Mungu na watumishi wake wanaojitaabisha kwa ajili ya injili.

Waefeso 6:18 ‘kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

19 pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;

20 ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena’.

Hakuna silaha nyingine tutakayoweza kumshinda shetani Zaidi ya maombi.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *