KUBALI KUMFUATA KRISTO KWELI ILI UWE BIBI ARUSI WAKE.
Jina la Bwana Yesu libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.
Kama wengi tunavyofahamu kuwa kanisa la Kristo linaitwa bibi arusi. Na tunajua kanisa sio jengo bali ni watu waliomwamini Yesu Kristo na kukubali kuingia gharama ya kumfuata..kama yeye mwenyewe alivyosema..
“…Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.” (Marko 8:34).
Sasa si kila mtu ambaye anajulikana kama mkristo ni bibi-arusi wa kristo, jambo ambalo wengi wetu hatulijui, Wakati huu wa mwisho maandiko yanatuonyesha wazi kuwa kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu wanaojiita wakristo.
Na hao wamezungumziwa kwa marefu sana katika kile kitabu cha Mathayo 25, kama wanawali werevu na wapumbavu. Hao kwa jina lingine ndio wanaojulikana kama bibi arusi na masuria. Suria ni mwanamke aliyetwaliwa tu na kuwekwa ndani, hana mkataba wala urithi wowote kwa mume wake, isipokuwa kupewa tu zawadi na kuondoka, lakini bibi arusi yeye ni mke, ambaye si tu kapokea zawadi, na urithi, kutoka kwa mume wake, bali amepewa kujua siri zote za mumuwe.
Sasa ili kuelewa vizuri, turudi katika kitabu cha Ruthu.
Kama wewe ni mwanafunzi wa Biblia utakuwa umeshawahi isoma habari ya Ruthu na Orpa (Kama hujasoma nakushauri ukakisome kwanza hicho kitabu, ndipo utaelewa vema, kiini cha somo hili, kwasababu hatutakichambua chote).Kitabu hichi kinaanzana na habari ya mtu anayeitwa Elimeleki, ambaye huyu alikuwa akiishi Israeli zamani kipindi cha Waamuzi, na biblia inatuambia siku njaa ilipokuja katika mji ule, Elimeleki alifunga safari kwenda nchi ya jirani kuishi huko yeye pamoja na mke wake aliyeitwa Naomi pamoja na wana wake wawili wa kiume..Lakini baada ya Muda kidogo mambo yalibadilika Elimeleki alikufa na kumwacha mke wake akiwa mjane na watoto wake wawili katika nchi ya ugenini..Na Baadaye kidogo watoto wake wote wawili walibahatika kupata wake wazuri tu, lakini kwa bahati mbaya, nao pia walifariki wakiwa bado hawajapata watoto na wale wanawake, Hivyo yule mwanamke mjane Naomi hakufanikiwa kuambulia chochote, si mume, si watoto, wala si wajukuu, na hapa sasa ameshakuwa mzee sana hawezi kubeba mimba tena, hata angesema azae asingeweza tena kwani muda umeshakwenda amekaa ugenini zaidi ya miaka 10, hata hana wa kumsaidia tena, nguvu zake zimeisha kilichobakia ni kurudi tu katika nchi yake Israeli kwenda kumalizia siku zake za kuishi.
Lakini tukiendelea kusoma habari tunaona Naomi sasa anakusudia kurudi katika nchi yake mpweke,mwenye uchungu mwingi, na hapa tunaona anawaambia wale wakwe zake, ambao mwanzoni walikuwa wameolewa na watoto wake wawili kwamba kila mmoja sasa awe na amani kurudi kwa jamaa zake wakaolewe na kufanikiwa na kuishi maisha ya furaha siku zote za maisha yao. Lakini tunaona wale wanawake wawili mwanzoni wote walikataa kumwacha Naomi peke yake, Lakini hilo halikumfanya Naomi aache kuwasihi wasifuatane naye, kwani hakutaka mtu yeyote abebe wake wowote kwa kulazimishwa, hivyo aliwabariki na kuwaomba warudi kwa jamaa zao wenyewe, lakini kama tunavyosoma habari, moyo wa Ruthu ulikuwa thabiti kuliko wa Orpa, Yeye Orpa baadaye alikubali kurudi kwa jamaa zake lakini Ruthu hakutaka kinyume chake alikuwa tayari kuambatana na Naomi popote aendapo kwa gharama zozote, alikubali kuchukuliana na gharama zote
Tunasoma:
Ruthu 1: 11 “Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?
12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;
13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu.
14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, LAKINI RUTHU AKAAMBATANA NAYE.
15 Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako.
16 Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
18 Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye”.
Sasa ukiendelea kusoma habari huko mbeleni utaona Ruthu alikubali kuondoka na Naomi katika umaskini wao, Ruthu asijue anapoelekea, asijue wakifika watapokelewa na nini, Ruthu akimtazama mwanamke yule kashakuwa mzee, na yeye bado ni binti kijana, ambaye anao uwezo wa kwenda kuolewa tena, ameacha vijana wazuri wenye mali katika nchi yake mwenyewe, pengine mabinti wenzake wanamkebehi wakimwambia hivi wewe umelogwa na kale kabibi? Kwani katakupa nini? mwangalie mwenzako Orpa, aliona mbele kuwa huko hakuna tena uelekeo wa maisha, zaidi ni kuzeeshwa tu akili za wazee na kuwahudumia tu, na mwisho wa siku kuwa kama mjakazi wao..Isitoshe anakwenda mahali asipopajua, wala hajawahi kuwafahamu watu wa huko, pengine walimwambia Unakwenda kupotea tu huko na mwisho wa siku utajuta..Wewe bado binti mdogo hata bado hujazaa, unakwenda wapi?
Lakini Ruthu hakujali kuipoteza nafsi yake kuwa ni kitu cha maana sana, kuliko kujitenga na mama wa mume wake marehemu, hivyo aliendelea kufuatana naye tu katika taabu zote kama alivyoapa.
Kumbuka ni sheria iliyokuwa imetolewa na Mungu katika Israeli, kwamba mtu yeyote aliye myahudi asioe mwanamke ambaye si myahudi, kadhalika ni mwiko pia kwa mwanamke wa Kiyahudi kuolewa na mtu wa mataifa, Lakini hapa tunaona Naomi akirudi katika nchi yake mwenyewe akiwa amemwambulia mtu mmoja tu.. Pengine wale ndugu zake waliokuwa wamebaki Israeli walitazamia Elimeleki pamoja na Naomi watarudi na mali nyingi, kondoo, mbuzi, ngamia pamoja wa watoto wao na wajukuu wengi, na wajakazi wengi. Lakini hapa anaonekana Naomi peke yake, na binti mmoja wa kimataifa, na tena kibaya zaidi ni heri angekuwa kijakazi wake, lakini kumbe ni mke wa mtoto wake, jambo ambalo ni machukizo makubwa kwa Israeli.
Lakini kwa jinsi Ruthu tabia yake ilivyokuwa njema, na ya kupendeza watu wote, na kwa ukarimu wake wote aliomfanyia Naomi bibi yake,basi habari zake zikasikika katikati ya jamaa za Naomi. Na siku moja alipokuwa anakwenda kuokota masazo ya nafaka kwenye mashamba ya watu matajiri, aliingia katika shamba la mtu mmoja mkuu sana wa mji huo jina lake Boazi, ndipo Boazi akamwona na kuulizia habari zake, na kuambiwa kuwa huyu ni binti wa Naomi. Wakati huo huo Boazi na Elimeleki mumewe Naomi walikuwa ni mtu na kaka yake. Hivyo ukiendelea kusoma habari hiyo mpaka mwisho kwa kuwa sasa hatuna nafasi ya kueleza habari yote, utaona kuwa mwisho wa siku Ruthu ambaye ni mwanamke wa kimataifa anakuja kuolewa na Boazi mtu mkuu wa Uzao wa kifalme, na ndiye kwa kupitia huyu Mfalme Daudi alitokea. Daudi ni kitukuu cha RUTHU.
Sasa kama tunavyojua mambo yote yanayotokea katika agano la kale ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika agano jipya, habari yote ya Naomi na Ruthu, ni habari ya Kristo na bibi-arusi wake ambayo Mungu alikuwa anaichora kwa kupitia maisha ya hawa watu.
Swali ni je! sisi tunaosema ni wakristo, tupo kwenye kundi lipi kati ya hao wanawake wawili, kundi la Ruthu au Orpa?
Kumbuka Ruthu anawakilisha bibi arusi safi wa Kristo aliyekubali kuacha vyote na kumfuata Naomi aliye kama Bwana wetu Yesu, na Orpa anawakilisha lile kundi la wale wanawali wapumbavu/Masuria ambaye hakukubali kuingia gharama ya kumfuata Naomi.
Ni vizuri leo kufahamu kuwa si kila mtu anayejihita mkristo ni bibi-arusi wa kristo!.
Huu ni wakati wa kupigania kwa bidii kuwa bibi arusi wa Kristo kwelikweli, kwasababu kama ukifa leo hii na sio bibi-arusi au unyakuo umekukuta na bado hujafanyika kuwa bibi arusi ujue kuwa unyakuo hautakuhusu hata kidogo, haijalishi utasema mimi ni mkristo wa miaka mingi, hutakwenda popote.
Mimi na wewe hatuna budi kuhakikisha tunakuwa bibi-arusi safi wa Kristo, na sio masuria, ili tupate kibali cha kukubaliwa na yeye siku ile ya mwisho.
Na tunafanyika bibi-arusi wa Kristo kwa kuacha vyote kama Ruthu alivyokubali kuacha vyote na kumfuata Naomi,
Maana ya kuacha vyote ni kuvitoa vile vitu ulivyo navyo ndani ya moyo wako…kila mtu anafahamu namna ya kukitoa kitu moyoni, hakuna haja ya kuelezea… “unapotoa kitu moyoni, unakuwa unakifuta ndani yako, kinakuwa sio kitu tena kinachokupa raha, kiwepo kisiwepo ni sawa tu” Wakati mwingine hiyo hali inaweza kuambatana na kuviacha vitu kwa nje kabisa wazi wazi…
Ulikuwa ni Tajiri unauacha utajiri wako unamfuata Yesu, maana yake…Hata mali zote zikipukutika katika safari yako ya kumfuata YESU hilo hujali, kwasababu hazipo tena moyoni mwako, Unamhisi Yesu moyoni kuliko utajiri ulionao…Na pia unakuwa humfuati Yesu ili akupe mali au azilinde mali zako, unamfuata kwasababu Moyoni mwako unaona una haja naye…Kuna upendo fulani ambao unamiminika ndani yako ambao hauwezi kuuelezea, Unajikuta tu unampenda tu Yesu bila sababu kama yeye anavyokupenda wewe bila sababu yoyote.
Kadhalika Ulikuwa ni MASKINI, unauacha Umaskini wako unamfuata YESU. Unauondoa umaskini moyoni mwako….Usimfuate Yesu kwasababu hauna gari! Au kwasababu umaskini unakutesa na kukuumiza… Hapo hujajikana nafsi ndugu! Usimfuate Yesu kwasababu unataka utajiri, au unataka heshima katika jamii, au kwasababu unataka kuwakomesha maadui..Unatakiwa Uuache umaskini wako ndipo unamfuata Yesu kiasi kwamba hata katika safari yako ya Imani, ukiongezekewa na kuwa Tajiri wa mambo ya kimwili, hilo kwako halina maana sana!…mali zikiongezeka ni kama vile moyoni mwako hakuna kilichoongezeka ni kama vile moyoni mwako hakuna kilichoongezeka…lakini uhusiano wako na Yesu unapoimarika ndipo unajihisi uchangamfu wa Ajabu unakuvaa….Inafikia mahali umasikini na Utajiri kwako ni sawasawa tu! Kama Ayubu, ilifika wakati hata mali zilipoongezeka hakufurahia (Soma Ayubu 31:25)..
Wapo watu ni maskini lakini hata katika huo umaskini wao, hawajawahi kumwomba Mungu katika sala zao utajiri, wameridhika na wana amani ya Ajabu mioyoni mwao..wawe nacho wasiwe nacho, hilo kwao halijalishi maadamu wanaye Yesu, hilo kwao ndio linalojalisha, huo ndio utajiri mkubwa kwao. Hivyo ni lazima kabla ya kumfuata Yesu kuuacha umaskini! Na kumfuata yeye wewe kama wewe.
Na pia baada ya kuacha vyote namna hiyo, kitakachofuatia ni kuchukiwa, kutengwa, kuonekana umerukwa na Akili, kuonekana mjinga katika jamii na kuonekana hufai…Na hivyo pia unapaswa uwe navyo tayari! Bwana Yesu hakutuficha kabisa alituambia ili tukikutana nayo tusiseme mbona hivi mbona vile..Upige gharama kabisa kabla ya kuanza kujenga Mnara! Usije ukafika katikati ukashindwa kumalizia…ndivyo Bwana alivyowaambia watu wote waliotaka kumfuata.
Luka 14:25 Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
[28]Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
[29]Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
[30]wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.
[31]Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?
[32]Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.
[33]Basi, KADHALIKA KILA MMOJA WENU ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.
Kabla ya kumfuata Yesu, piga hesabu kuwa kuna kuchekwa huko mbele, kuna kudharaulika, kuna kupungukiwa wakati mwingine hata kwa kipindi kirefu sana, wakati mwingine hata miaka kadhaa, hata miaka 5, au 10, hata 15, lakini haitadumu hivyo hata milele, kuna kutengwa na kuonekana mjinga, hata kwa miaka kadhaa…piga gharama zote hizo..Kama haupo tayari! Kuonekana mshamba kwa muda mrefu hivyo, au kuonekana mjinga kwa miaka kadhaa, au kudharaulika kwa miaka kadhaa, au kama haupo tayari kukosana na mama yako kuhusiana na Imani yako, au kukosana na Baba yako, au Watoto wako, au mke wako..kama unajua yatakushinda huko mbeleni…Biblia inasema tafuta sharti ya Amani mapema!…Usijiingize mahali ambapo hujajua yatakayokupata mbeleni, ukaja ukakutana na ambayo hukutegemea ukaanza kujuta na kulalamika.
Kwasababu Bwana Yesu anasema:
Luka 12: 51 “Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.
52 Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu.
53 Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”.
Je! Umejikana nafsi?..Umejitwika msalaba wako na kumfuata Yesu? Fahamu kuwa mtu yeyote anayeingia gharama kubwa kama hizo, Sio bure bure tu, Huyo anapelekwa katika viwango vya juu zaidi vya kuwa karibu na Kristo zaidi ya watu wengine wote..kama vile ile habari ya Ruthu na Naomi,..alipokubali kuingia ile gharama mwisho wake tunaujua, alikutana na Boazi ambaye alikuwa ni mtu mkuu sana.. akawa mke wake. Na sisi tunapokubali kuingia hiyo gharama ya kuacha vyote..tunafanyika kuwa bibi-arusi wa Kristo na hatimaye tutarudishiwa furaha yote na vyote tulivyopoteza mara dufu kama vile Ayubu.
Sasa uchaguzi ni wetu,..Je! tutaamua kuanza safari ya kwenda kwa BOAZI wetu mbinguni? Au tutataka kuwa kama Orpa, kuona kuwa Naomi hana faida yoyote kwetu, Yesu Kristo hana chochote cha kutugawia, tukimfuata tutaendelea kuwa maskini, tukimfuata tutakuwa washamba, tukimfuata kampani zetu za Disco na vilabuni zitatuacha, tukimfuata, vimini vyetu tutavitupa, tukimfuata, tutaonekana vibibi,. tukimfuata tutakwenda kupotea moja kwa moja na kuwa vichaa..
Hizi ni siku za mwisho, Ni heri ukakubali kuacha vyote ili uwe bibi arusi wa Kristo kabla mlango haujafungwa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.