Karibu, tuyatafakari Maneno ya Uzima..
Ikiwa wewe ni mwanamke basi somo hili ni maalumu kwako kujifunza.
Yapo mambo ambayo Bwana anayafanya juu yako, mengine ulikuwa ukimwomba lakini mengi ni Bwana mwenyewe anakutendea kwa wema wake, embu jiulize baada ya kutendewa muujiza huo ulifanya nini, wengi wanaishia kushukuru baada ya hapo wanaendelea na mambo yao, nataka nikuambie lipo jambo Bwana anataka ulifanye baada ya kukufanyia muujiza, jifunze hapa..
Tujifunze kwa wanawake baadhi kwenye maandiko jinsi walivyofanya na kwa pamoja tutajifunza kitu, ni wanawake ambao hawakuwa na uongozi pengine wowote katika huduma hii ya Bwana Yesu lakini walifanya kitu kikubwa sana, walijua nafasi yao ni ipi na wakaitumia vema.
Tusome
Mathayo 27:55 “Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, HAO NDIO WALIOMFUATA YESU TOKA GALILAYA, NA KUMTUMIKIA.
56 Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo”.
Maandiko yametufunulia hapo kuwa ni wanawake waliokuwa wakimtumikia Bwana, hawa hawakuishia tu kusikiliza maneno ya Yesu, hawakwenda kwenye mikutano kutafuta uponyaji tu, hawakufuatana na Yesu ili waonekane na wao wapo kwenye msafara bali walifanya kitu cha kiutofauti,
Tuendelee kusoma..
Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye,
2 NA WANAWAKE KADHA WA KADHA ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,
3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, WALIOKUWA WAKIMHUDUMIA KWA MALI ZAO”.
Umeona, kumbe huduma ya kuipeleka injili Mbele kwa asilimia kubwa ilibebwa na hawa wanawake, WALIAMUA KUMTUMIKIA BWANA KWA MALI ZAO, na hawakuangalia wako wangapi, wingi wao au uchache, kwasababu maandiko hapo yametaja kama ni wanawake kadha wa kadha, yaani wa kila aina, aliyeguswa alijiunga, mwishowe kikawa kama kikundi,kikashirikiana kumsapoti Bwana na mitume wake,
Na kubwa lililowasukuma kumtumikia Mungu kwa mali zao ni miujiza waliotendewa na Bwana Yesu, wengi wao walitolewa mapepo mengi kama Mariamu Magdalene, na wengine waliponywa magonjwa makubwa, wakaona si sawa kusema Nashukuru Bwana ikatosha, na wao waanza kugharamika kwa ajili ya Mungu..
Jiulize mwanamke, ni mangapi Mungu amekutendea,na anazidi kukutendea, shukrani yako ni njema ila lipo la ziada Bwana anatamani kuliona kama kwa wanawake hawa..ulimwomba Bwana akupe mtoto, ulipata,alikuponya na magonjwa, amekupa wokovu, ulimwomba aimarishe ndoa yako, ulitamani mke au mume/amekupa kazi, tafakari ulimwomba Bwana mangapi na akayatenda kwako, kwanini usifanye jambo la kiutofauti?
Hawa wanawake hawakuishia kumshukuru tu na kuendelea kumtazama, walishtuka mapema wakaona wafanye na wao kwa matendo zaidi,
Walijitoa kwa mali zao, walivunja vibweta vyao ili Bwana Yesu asikose nauli ya kwenda kuhubiri, walitoa fedha zao ili injili isambae miji yote, mitume wasipungukiwe wala wasiteseke kwa njaa, pengine walikuwa wakiwaandalia na chakula kabisa, na ndo hao mashujaa ambao hawakujiangalia wao na maisha yao bali Bwana na ndo tunawasoma hadi leo..
Tunamwona na mamamkwe na Petro baada ya kuponywa homa kali akuendelea kukaa hapo, na yeye alimtumikia Bwana, maandiko yanasemaje, soma hapa.
Mathayo 8:14 “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.
15 Akamgusa mkono, homa ikamwacha; NAYE AKAONDOKA, AKAWATUMIKIA
Amka Katika usingizi, jiulize unamtumikiaje Bwana, kwa matendo yake makuu aliyokuonyesha,unatumikaje, usimtumikie Bwana kwa maneno tu bali onyesha na vitendo..
Unaweza usiwe na uongozi wowote,wa mwinjilist,nabii au Mchungaji lakini kujitoa kwako,kwa mali zako kukafanya kazi kubwa zaidi yao, kuwa mwaminifu kwa Bwana, ndivyo Mungu atakavyokuheshimu na kukufanya Mtumishi wake mana unaipeleka injili Mbele kwa kumtumikia kwa mali zako, anza sasa..
Bwana akubariki..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.