
LABDA WATASIKIA NA KUGHAIRI NJIA ZAO MBAYA.
Jina la Bwana Yesu libarikiwe karibu tujifunze habari njema.
Kabla Mungu kuleta mabaya kwa mtu au taifa Fulani huwa anatanguliza kwanza kumuonya yule mtu au lile taifa, kwasababu ni Mungu mwenye huruma na upendo hapendi kuwatesa wanadamu.
Maombolezo 3:33 “Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu.Wala kuwahuzunisha”.
Kwasababu hiyo basi, anafanya kila namna aweze kumponya mwanadamu na mabaya yaliyo mbele yake, hamkatii mtu tamaa haraka, haijalishi huyo mtu amemchukiza kiasi gani.. bado huwa anatoaga nafasi nyingine zaidi na zaidi kwasababu ya upendo wake. Lakini mtu yule akikataa kugeuka na kuacha njia zake mbaya, basi atakuwa amechagua kupatwa na mabaya mwenyewe lakini sio mapenzi ya Mungu.
Tunasoma wana wa Israeli walimchukiza sana Mungu kwa muda mrefu, lakini Mungu akawa anatuma watumishi wake wakawaonye na kuwasihi wageuke na kuacha maovu yao, lakini tunasoma wana wa Israeli waliendelea kufanya mabaya na machukizo ya kila namna na zaidi wakawauwa watumishi wa Mungu waliokuwa wanawaonya kwa Neno la Mungu, wakawaua wakina Isaya na watumishi wengine wengi…wakawadhihaki na kuwacheka wengine.
2Mambo ya Nyakati 36:15 “Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;
[16]lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
Lakini kabla hayo mabaya, hiyo ghadhabu haijatukia.. Bwana alimtuma mtumishi wake kwa mara nyingine tena Nabii Yeremia aende kuwaonya.. kwani Bwana alisema huwenda labda watasikia na kuacha maovu yao, hii ni kuonyesha jinsi neema na huruma za Mungu zilivyokuwa nyingi kwa watu wake.
Yeremia 26:1 Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa BWANA, kusema,
[2]BWANA asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya BWANA, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya BWANA; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
[3] LABDA WATASIKIA, NA KUGHAIRI NA KUACHA KILA MTU NJIA YAKE MBAYA; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.
[4]Nawe utawaambia, BWANA asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
[5]kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
[6]basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.
Ndugu/Dada huwenda umesikia injili sana, Mungu amesema na wewe kupitia watumishi wake wa kweli uache njia zako mbaya, uache huo uasherati unaoufanya kila siku kana kwamba ndio chakula chako, umejichua kwa muda mrefu, umebobea kwenye ulevi, ukahaba, wizi, uchawi, usengenyaji, rushwa, uongo, na hutaki kusikia. Umewadharau na kuwadhihaki watumishi wa Mungu waliokuhubiria.
Lakini leo Bwana amenituma niseme na wewe kwa mara nyingine tena labda utasikia na kutubu/kumgeuki yeye, labda utasikia na kuacha kuvaa mavazi hayo ya kizinzi, labda utasikia na kuacha kumkosoa kwa kubadilisha muonekano wako aliyokuumbia.
Pengine hii ni nafasi ya mwisho kwako, hivyo amua kutii sauti ya Mungu maana kuna ghadhabu ipo mbele yako, fahamu kuwa Mungu hafurahii ufe katika hiyo hali uliyonayo, ndio maana anakupa tena hii nafasi japokuwa amekuonya mara nyingi.
Ezekieli 18:23 Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?
Sio mapenzi ya Mungu uende jehanumu, sio mapenzi yake ukatupwe kwenye ziwa la moto, lakini kama hutotaka kusikia basi utakuwa umechagua mwenyewe kwenda huko.
Hivyo hebu amua leo kutii na kufuata njia ya uzima, amua kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi zote, amua kuacha hayo mambo machafu unayoyafanya gizani Mungu anakuona na anakuhuzunikia. Mpe Yesu maisha yako kwa kumaanisha kabisa yeye atakupa nguvu ya kushinda dhambi zote na namna zote za udunia.
Hivyo kama upo tayari kuchukua uamuzi wa kumgeuki Yesu leo na unahitaji msaada zaidi basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii nasi tutakusaidia bure.
Maran atha.(Bwana Yesu anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.